
Dar es Salaam. Mahakama Kuu, Divisheni ya Biashara, imeyaamuru makampuni matatu ya uchimbaji madini hapa Tanzania, kuilipa kampuni ya Petrolube Tanzania Limited, Sh5.62 bilioni, kama malimbikizo ya madai ya bidhaa walizohudumiwa.
Makampuni hayo ambayo yameamriwa na Mahakama Kuu kulipa fedha hizo ni pamoja na kampuni ya Bulyanhulu Mining Limited, North Mara Gold Limited na Pangea Minerals ambayo linafahamika pia kwa jina la Buzwagi Goldmine.
Hukumu hiyo (default judgement), baada ya kampuni hizo kutowasilisha utetezi wao kwa maandishi, imetolewa Mei 22, 2026 na Jaji Abdallah Gonzi wa Masjala ya Dar es Salaam, na kuwekwa katika tovuti ya Mahakama Mei 26,2026.
Katika hukumu hiyo, Jaji Gozni alisema mahakama hiyo kupitia hati ya kiapo cha mdai na viambatanishi katika kuthibitisha madai yake, imeridhikia kuwa ameweza kuthibitisha kesi yake katika viwango vinavyokubalika katika kesi za madai.
Jaji amesema kutokana na ushahidi uliowekwa mbele yake, hususan makubaliano yaliyothibitishwa kupitia ankara na barua pepe, ni dhahiri kwamba kulikuwa na uhusiano wa kimkataba kati ya Mlalamikaji na makampuni hayo matatu.
Ushahidi huo ni pamoja na nakala za ankara zilizotolewa kwa wadaiwa na ushahidi wa usambazaji wa bidhaa kama ilivyoombwa na thamani yake.
“Kuhusu kama wadaiwa walikiuka majukumu ya kimkataba, Mdai ameonyesha kupitia ankara na barua pepe zilizoungwa mkono na ushahidi katika hati ya kiapo kwamba wameshindwa kulipa kiasi wanachodaiwa licha ya kupewa huduma”.
Jaji aliongeza kusema “Wadaiwa (makampuni hayo matatu) hawajawasilisha utetezi wowote kupinga madai ya Mdai. Hakuna utetezi uliowasilishwa na Wadaiwa katika shauri hili. Ushahidi wa mlalamikaji bado haujapingwa”.
“Nimeridhika kwa uwiano wa uwezekano (balance of probabilities) kwamba wadaiwa wanakiuka majukumu yao ya kimkataba dhidi ya Mdai,”alisema Jaji.
“Kuhusu uharibifu, Mdai amethibitisha uharibifu maalum (specific damages) kama inavyodaiwa kupitia ushahidi wa hali halisi katika mfumo wa ankara”
“Mlalamikaji alipata matatizo katika kufuatilia malipo yake hivyo inayojumuisha usumbufu, wasiwasi na mateso. Hii inampa haki kwa uharibifu wa jumla” alisema Jaji katika hukumu hiyo na kukubaliana na nafuu ambazo mdai aliziomba.
Malipo ya mabilioni
Katika kujibu maombi ya mdai, Jaji amekubaliana na ombi lake la kwanza na kutamka kuwa wadaiwa kwa pamoja walikiuka mkataba wa usambazaji wa bidhaa na huduma walizoingia kati ya mdai na walalamikaji hao watatu.
Halikadhalika Jaji aliwaamuru wadaiwa kwa pamoja kumlipa mdai Dola 186,574.48 za Marekani zikiwa ni malimbikizo ya ankara ambazo hazijalipwa inayotokana na bidhaa zilizotolewa na mdai na kuwasilishwa kwa wadaiwa.
Mbali na amri hiyo, wadaiwa hao wameamriwa kulipa Dola 1,938,797.38 za Marekani zikiwa malimbikizo ya bei (price for stocks) na bidhaa ambazo mdai aliziwasilisha kwa wadaiwa hao na hazikulipwa hadi anafungua shauri.
Kwa kiwango cha ubadilishaji fedha za kigeni cha Sh2,600 kwa Dola moja ya Marekani, fedha hizo ni sawa na Sh5.52 bilioni za Tanzania.
Mahakama pia imewaamuru wadaiwa kumlipa dai fidia ya jumla inayofikia Sh100 milioni za Tanzania kutokana na usumbufu waliomsababishia mdai kwa kuvunja mkataba baina yao wa kuwasambazia bidhaa pamoja na huduma mbalimbali.
Pia wameamriwa kulipa riba ya asilimia 7 kwa mwaka ya fedha zote hozo kuanzia tarehe ya kutolewa hukumu na hadi kukamilisha malipo lakini Jaji akaenda mbali zaidi na kuwataka wadaiwa hao kulipa pia gharama za shauri hilo la kibiashara.
Kiini cha mgogoro
Kulingana na uchambuzi wa hukumu hiyo, Jaji alisema mlalamikaji kama alivyoeleza katika kiapo chake, ni kampuni inayofanya biashara katika usambazaji wa vilainishi, bidhaa, bidhaa na huduma nyingine zinazohusiana na hizo.
Wadaiwa wao ni makampuni ya madini ambayo kwa nyakati tofautii, yaliweka maagizo ya kusambaziwa bidhaa na huduma mbalimbali kutoka kwa Mdai.
Ni kesi ya Mlalamikaji kwamba, kwa nyakati tofauti, wadaiwa hao waliagiza wapelekewe bidhaa na huduma kutoka kwa mdai ambapo alishughulikia kama alivyoagizwa na kusambaza na kuwasilisha bidhaa na huduma zilizoombwa.
Mlalamikaji alieleza kuwa mashirikiano ya kibiashara baina yao yaliegemea katika maagizo aliyokuwa akiyapokea kutoka kwa wadaiwa, ankara zilizotolewa na wadaiwa na ulikuwa ni wajibu wao kulipa kiasi cha ankra ndani ya muda.
Mlalamikaji alidai kuwa Julai 1, 2012, makampuni hayo kupitia kwa kampuni yao ya usimamizi iliyojulikana kama ACACIA, iliingia katika mkataba wa biashara tna mdai wa usambazaji wa vilainishi na huduma zinazohusiana na bidhaa hizo.
Chini ya makubaliano hayo, wadaiwa walikuwa na haki ya kutoa amri kupitia maagizo ya ununuzi au maagizo ya barua pepe na mlalaikaji au mdai aliwajibika kusambaza bidhaa alizotakiwa kusambaza na kutoa ankara ya malipo.
Kulingana na ushahidi wake, makampuni hayo yalitoa maagizo kwa nyakati tofauti ya kupewa huduma na bidhaa zenye thamani hiyo ya zaidi ya Sh5 bilioni na jitihada zake na kudai malimbikizo ya ankra hizo hayakuzaa matunda.
Baada ya kufunguliwa kwa shauri hilo namba 19539 la mwaka 2025, makampuni hayo yalitakiwa kuwasilisha utetezi wao kwa maandishi lakini hawakufanya hivyo, wakaomba kuongezewa muda wa kufanya hivyo, lakini maombi yalikataliwa.
Maombi hayo yalitupiliwa mbali na mahakama Desemba 24,2025 kwa kukosa mashiko hivyo ikamfanya mlalamikaji kuiomba mahakama itoe hukumu ya upande wake (default judgement) kama kanuni za mahakama hiyo zinavyoelekeza.
