Prisons yakusanya ‘kijiji’ kubaki salama Ligi KuuPrisons yakusanya ‘kijiji’ kubaki salama Ligi Kuu

USHINDI wa mabao 3-2 walioupata Tanzania Prisons dhidi ya Pamba Jiji umeonekana kuwapa matumaini na nguvu mpya wachezaji, benchi la ufundi na mashabiki wa timu hiyo, wakitamba kuwa haijaisha hadi iishe.

Prisons ikiwa ugenini huko jijini Mwanza ilifanikiwa kupata pointi tatu na kufikia 20 na kubaki nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu, huku ikibakiza michezo mitano kujua hatma yake.

Katika michezo iliyobaki itacheza mitatu ugenini dhidi ya Singida Black Stars, JKT Tanzania na Mashujaa, huku nyumbani ikizileta Dodoma Jiji na Mtibwa Sugar, mpango ukiwa ni kuvuna pointi 15 ili kujihakikishia kubaki salama.

Timu hiyo haikuwa na mwanzo mzuri hadi kufikia uamuzi wa kumtema aliyekuwa kocha wake, Zedekiah Otieno raia wa Kenya na nafasi yake kuzibwa na Shedrack Nsajigwa ambaye amefikisha ushindi wa pili katika michezo 10 alizoongoza.

Straika wa timu hiyo, Oscar Mwajanga amesema kwa sasa mkakati ni kuendelea kusaka pointi tatu bila kujali wanacheza nyumbani au ugenini kuhakikisha Prisons inabaki salama Ligi Kuu.

“Ushindi huu ni wa timu kwa ujumla, hatuko sehemu nzuri lakini kwakuwa ligi haijaisha, lolote linawezekana, kimsingi kila mmoja lazima aipambanie timu ili kuona tunakwepa aibu ya kushuka daraja” amesema Mwajanga mwenye mabao manne.

Kwa upande wake shabiki wa timu hiyo, Julius Mwasa amesema kwa sasa ni muda wa wadau na mashabiki wote jijini Mbeya kuunganisha nguvu ya pamoja kuipambania Prisons iweze kubaki Ligi Kuu.

“Lolote linawezekana, tumenusurika sana kushuka daraja na tunaweza kubaki salama hata msimu huu, niombe kila mmoja ajitolee kwa ari na mali timu ishinde mechi zote zilizobaki na uwezekano upo,” alisema Mwasa.

Prisons inatarajia kurejea uwanjani Juni 14 kuwakaribisha Dodoma Jiji, mchezo ambao utapigwa uwanja wa Sokoine jijini humo, huku hesabu zikiwa ni kushinda mechi hiyo ili kujinasua mkiani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *