
KLABU ya Arsenal imemtambulisha rasmi kiungo mwenye asili ya Tanzania, Lisa Baum, kuwa mchezaji wake mpya katika dirisha hili la usajili, baada ya kufikia makubaliano ya kumsajili kutoka RB Leipzig ya Ujerumani.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 19 amesaini mkataba wa miaka mitatu wenye chaguo la kuongeza mwaka mmoja.
Baum alizaliwa Dar es Salaam, Tanzania Novemba 25, 2006 akiwa na baba Mjerumani na mama Mtanzania. Familia yake ilihamia Ujerumani alipokuwa na umri wa miaka minne, ambako alikulia na kuanza safari yake ya soka iliyomfikisha kwenye moja ya klabu kubwa zaidi barani Ulaya.
Akizungumza baada ya kutambulishwa, Baum alisema amefurahishwa na hatua hiyo, akieleza kuwa Arsenal ni sehemu sahihi kwake kuendelea kukua kisoka na kupambania mataji.
“Nina furaha kubwa kujiunga na Arsenal na siwezi kusubiri kuanza. Ligi hii ina ushindani mkubwa na Arsenal ni klabu kubwa sana. Nataka kushinda mataji na kuendelea kuimarisha kiwango changu, na nahisi Arsenal ndiyo sehemu sahihi ya kufanikisha malengo hayo,” alisema Baum
Kocha wa Arsenal Women, Renée Slegers, alisema kiungo huyo mwenye uwezo wa kucheza kama winga ana kasi, uthubutu na uwezo mkubwa wa kushambulia, akiamini bado ana nafasi kubwa ya kuendelea kuimarika.
“Lisa ni mshambuliaji wa pembeni mwenye umri mdogo ambaye ataleta kasi, nguvu na uamuzi wa kushambulia moja kwa moja kwenye safu yetu ya ushambuliaji. Akiwa na miaka 19 bado anaendelea kukua, na tunaamini ana uwezo mkubwa sana ambao tutamsaidia kuufikia. Tunamkaribisha Arsenal na tunatarajia safari nzuri pamoja naye.”
Kabla ya Arsenal kumtambulisha nyota huyo aliwahi kuhusishwa na klabu nyingine za Ulaya ikiwemo Man United, Barcelona na klabu nyingine.
Baum alianza kucheza soka katika klabu za vijana za MTV Ahrensbök na baadaye TSV Pansdorf kabla ya kujiunga na akademi ya Hamburger SV mwaka 2021.
Akiwa HSV alisaidia timu ya vijana kutwaa ubingwa wa Ujerumani, kisha akapandishwa kikosi cha wakubwa na kuchangia kupanda kutoka Regionalliga hadi 2. Bundesliga na baadaye kufuzu Bundesliga ya wanawake.
Mwaka 2025 alijiunga na RB Leipzig, ambako alipata nafasi ya kucheza Bundesliga kwa mara ya kwanza.
Katika msimu wake wa kwanza aliichezea Leipzig mechi 25 za ligi na kufunga mabao sita, kiwango kilichovutia vigogo kadhaa wa Ulaya wakiwemo Barcelona, Bayern Munich na Manchester United kabla Arsenal kukamilisha dili hilo.
Mbali na ngazi ya klabu, Baum ameichezea Ujerumani katika timu mbalimbali za vijana kuanzia U16 hadi U20. Alikuwa sehemu ya kikosi cha Ujerumani kilichoshiriki Kombe la Dunia la Wanawake chini ya miaka 20 mwaka 2024, lakini bado hajaitwa katika timu ya taifa ya wakubwa ya Ujerumani.
Usajili wa Baum unaendelea kuonyesha mchango wa vipaji vyenye asili ya Tanzania katika soka la kimataifa. Kwa kujiunga na mabingwa wa Ulaya Watanzania watakuwa wakimtazama kuona kama ataendeleza kiwango kilichomfanya kuwa mmoja wa wachezaji vijana wanaotajwa kuwa na mustakabali mkubwa zaidi katika soka la wanawake barani Ulaya.
Nyota huyo anakwenda kuungana na Aisha Masaka aliyesajiliwa Brighton ambaye amekuwa nje akiuguza majeraha.