Dodoma. Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limewaita vijana 60,000 waliomaliza kidato cha sita ili kujiunga na mafunzo ya lazima (kwa mujibu wa sheria).
Idadi hiyo imekuja kufuatia kauli ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa aliyotoa hivi karibuni kwenye bajeti yake akisema wameongeza kutoka washiriki 40,000 hadi 60,000.
Hata hivyo, JKT wamesema mwelekeo wa mbeleni ni kuhakikisha vijana wote wanaomaliza kidato cha sita wanakwenda moja kwa moja kwenye makambi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Mei 28, 2026 kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa Meja Jenerali Rajabu Mabele,
Mkuu wa Utawala tawi la JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena amesema vijana hao wataanza kuripoti Juni 1, 2026.
Brigedia Jenerali Mabena amesema mpango huo unagusa vijana waliohitimu elimu ya sekondari kidato cha sita mwaka 2026, kutoka shule zote za Tanzania Bara na visiwani.
“Sanjari na wito huo, JKT limewapangia makambi watakaokwenda kupatiwa mafunzo na wanatakiwa kuripoti kambini kuanzia Juni 1 hadi 7, 2026,” amesema Mabena.
Ametaja baadhi ya Makambi ya JKT waliyopangiwa ni Rwamkoma, Mara, Msange, Tabora, Ruvu, Kibiti, Mpwapwa, na Makutupora.
Makambi mengine ni Mafinga, Iringa, Male,Ruvuma, Mgambo, Maramba, Tanga, Makuyuni JKT na Oljoro, Arusha, Bulombora, Kagera, Kanembwa, Mtabila, Kigoma, Itaka, Songwe, Luwa, Milundikwa, Rukwa, Nachingwea, Lindi na Chuo cha Uongozi JKT (CUJKT) Kimbiji – Dar es Salaam.
“Wahitimu wenye ulemavu wa kuonekana kwa macho (Physical disabilities) waripoti katika Kambi ya Ruvu iliyo Mlandizi Mkoa wa Pwani ambako ina miundombinu ya kuwahudumia watu hao,” amesema.
Kuhusu vifaa vinavyotakiwa ni kaptura ya rangi ya bluu iliyokolea yenye mpira kiunoni (lastic) isiyo na mfuko nyuma, urefu unaofika magotini na fulana ya rangi ya kijani, raba za michezo zenye rangi ya kijani au bluu, shuka mbili zenye rangi ya bluu bahari na soksi nyeusi.
Nyingine ni nguo za kuzuia baridi kwa waliopangiwa makambi yenye baridi na nyaraka zote zinazohitajika katika udahili wa kujiunga na elimu ya juu, zikiwemo vyeti vya kuzaliwa na vyeti vya kuhitimu kidato cha nne.
Katika taarifa yao, JKT wamesema mafunzo hayo ni muhimu na vijana waliopata fursa hiyo waone fahari kujiunga na mafunzo kwani siyo wote watakwenda vyuo vikuu badala yake wengine watabaki, hivyo watakuwa na ujuzi utakaowasaidia kuendesha maisha.
Mafunzo ya JKT yalirejea rasmi 2013 baada ya muda mrefu kutokuwepo na kwa mara ya kwanza walichaguliwa vijana 5,000 jambo lililoleta maswali kwani baadhi ya shule hazikuguswa kabisa.
