Mama afariki dunia kwa ajali akiwahi shuleni lilikoungua bweni la wanafunzi        Mama afariki dunia kwa ajali akiwahi shuleni lilikoungua bweni la wanafunzi        

Ni huzuni! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya mama wa mwanafunzi mmoja ambaye ni miongoni mwa waathirika wa ajali ya moto katika shule ya Utumishi Academy nchini Kenya kufariki dunia katika ajali ya barabarani alipokuwa akielekea shuleni kufuatilia mkasa huo.

Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, mwanamke huyo alipoteza maisha katika ajali iliyotokea kwenye barabara kuu ya Gilgil-Nakuru, wakati yeye na mumewe walipokuwa wakikimbilia shuleni baada ya kupokea taarifa za moto ulioteketeza bweni la shule hiyo.

Taarifa zinaeleza kuwa gari walilokuwa wakisafiria lilipata ajali katika eneo la Kariandusi, ambapo mama huyo alifariki dunia papo hapo huku mumewe akinusurika kifo lakini akijeruhiwa na kupelekwa hospitalini kwa matibabu.

Inadaiwa kuwa binti yao hakupoteza maisha katika tukio hilo la moto, lakini alijeruhiwa na anaendelea kupatiwa matibabu hospitalini.

Moto huo uliotokea katika shule ya Utumishi Academy ulisababisha vifo vya wanafunzi 16 na wengine 79 kujeruhiwa, kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Elimu nchini Kenya.

Tukio hilo lilitokea wakati wanafunzi wakiwa wamelala ndani ya moja ya mabweni ya shule hiyo.

Ripoti za awali zinaonyesha kuwa moja ya sababu zilizochangia ongezeko la vifo ni kutokana na bweni hilo kudaiwa kufungwa kwa ndani wakati moto ulipozuka.

Wanafunzi saba walioumia vibaya wamehamishiwa kwa ndege kwenda Nairobi kwa matibabu zaidi, huku wanafunzi wengine 61 wakiruhusiwa kurejea nyumbani baada ya kupatiwa matibabu.

Kufuatia mkasa huo, Waziri wa Elimu nchini Kenya, Julius Ogamba, ametangaza kufungwa kwa shule hiyo huku akiwataka wazazi kwenda kuwachukua watoto wao wakati uchunguzi kuhusu chanzo cha moto huo ukiendelea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *