
Matokeo hayo yamechapishwa kwenye ripoti ya kila mwaka ya Umoja wa Mataifa inayohusu kipindi cha Januari hadi Desemba 2025, iliyoandaliwa kwa mujibu wa Azimio namba 2467 la mwaka 2019 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ikiangazia nchi 21 ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Sudan Kusini, Sudan, Yemen na Colombia.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, matukio yaliyothibitishwa na Umoja wa Mataifa yaliongezeka kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na mwaka 2024 na yalihusisha ukatili wa hali ya juu. Ukatili huo ulitokea katika maeneo yenye migogoro katika kanda mbalimbali ambapo vita, ukosefu wa usalama na migogoro ya kibinadamu iliendelea kuongezeka.
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC)
Kwa mujibu wa ripoti, mwaka 2025, taarifa za ukatili wa kingono zilijitokeza wakati mapigano yalipozidi kati ya vikosi vya Jeshi la DRC, (FARDC) na makundi mbalimbali yaliyojihami, ikiwemo wakati wa mapigano makali mashariki mwa DRC yaliyofanywa na kundi la M23 kwa “msaada wa moja kwa moja na ushiriki wa vikosi vya ulinzi vya Rwanda.”
Taarifa za ukatili wa kingono pia ziliripotiwa baada ya mji wa Uvira ulioko jimbo la Kivu Kusini kutekwa na wapiganaji wa M23 mwezi Desemba 2025.
Katika majimbo ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini, Ituri, Maniema na Tanganyika, kati ya Januari na Septemba, watoa huduma walirekodi matukio 90,199 ya ukatili wa kingono, ikiwemo ubakaji, yaliyotekelezwa na makundi yaliyojihami.
Mapendekezo kwa DRC
Katibu Mkuu anatoa wito kwa pande zote zinazohusika katika migogoro kusitisha vitendo vyote vya ukatili wa kingono unaohusiana na migogoro na kuhakikisha hatua za kuzuia na kukabiliana na vitendo hivyo zinajumuishwa katika michakato yote ya upatanishi na amani.
“Ninaipongeza hatua kubwa iliyofikiwa katika kutoa fidia kwa manusura kwa mujibu wa maamuzi ya mahakama za ndani ya nchi. Na ninakaribisha kuandaliwa kwa ramani maalumu za utekelezaji kwa ajili ya polisi na jeshi katika mfumo wa nyongeza ya taarifa ya pamoja ya mwaka 2019, na ninatoa wito wa utekelezaji wake wa haraka,” amesema Katibu Mkuu
Vikwazo vya ufuatiliaji ukiukwaji wa haki
Ripoti hiyo imeeleza kuwa migogoro ya kivita inayoendelea, vikwazo vya upatikanaji wa misaada ya kibinadamu na mashambulizi yanayoongezeka dhidi ya haki za wanawake vilifanya iwe vigumu zaidi kwa Umoja wa Mataifa na mashirika ya misaada kufuatilia ukiukwaji wa haki na kusaidia manusura.
Washauri wa ulinzi wa wanawake na wahudumu walio mstari wa mbele walikabiliwa na hatari kubwa zaidi, huku huduma nyingi kwa manusura zikifungwa au kupunguzwa kutokana na upungufu mkubwa wa fedha.
“Umoja wa Mataifa umeonya kuwa kuongezeka kwa matumizi ya kijeshi duniani na kupungua kwa bajeti za misaada ya kibinadamu kulidhoofisha uwezo wa serikali na taasisi kuzuia na kuchunguza ukatili wa kingono,” imesema ripoti hiyo.
Kutokana na hali hiyo, manusura wengi walipoteza imani kwa mamlaka na kuachwa bila huduma muhimu za kitabibu, kisaikolojia na ulinzi.
Mapendekezo ya jumla
Ripoti hiyo imetoa wito wa kuchukuliwa hatua madhubuti zaidi za kimataifa pamoja na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa fedha ili kulinda raia na kuwasaidia manusura wa ukatili wa kingono unaohusiana na migogoro.
Kauli ya Pramila Patten, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu Ukatili wa Kingono kwenye Mizozo
Punde baada ya ripoti kuchapishwa, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na Ukatili wa Kingono kwenye mizozo, Pramila Patten amezungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani na miongoni mwa aliyoyazungumza ni kama ifuatavyo:
-
UKATILI ULIOFANYIKA
- Mwaka 2025 Umoja wa Mataifa ulirekodi matukio 9,788 yaliyothibitishwa ya ukatili wa kingono kwenye mizozo, ikiwa ni zaidi ya mara mbili ya idadi ya mwaka uliotangulia wa 2024.
- Wanawake na wasichana waliendelea kuwa waathirika wakuu, ingawa wanaume na wavulana pia walilengwa, hasa katika maeneo ya vizuizini.
- Ukiukwaji huo ulijumuisha ubakaji, ubakaji wa kundi, utumwa wa kingono, ndoa za kulazimishwa, biashara haramu ya binadamu, mateso na utekaji nyara.
- Waathirika walikuwa na umri wa kati ya mwaka mmoja hadi miaka 70, wakiwemo watu wenye ulemavu.
- Kupunguzwa kwa ufadhili na kupungua kwa upatikanaji wa misaada ya kibinadamu kumedhoofisha huduma kwa manusura na kuathiri ufuatiliaji pamoja na utoaji wa taarifa.
Mifumo mikuu iliyobainika
• Ukatili wa kingono unaendelea kutumika kama mbinu ya vita, ugaidi, mateso, ukandamizaji na udhibiti wa maeneo.
• Makundi yenye silaha katika nchi zikiwemo Sudan, Sudan Kusini, DRC, Mali, Nigeria, Somalia, Syria, Haiti na Colombia yalitumia ukatili wa kingono sambamba na utekaji nyara, biashara haramu ya binadamu na ndoa za kulazimishwa.
• Ukatili wa kingono dhidi ya wafungwa, hasa wanaume na wavulana, uliripotiwa nchini Libya, Myanmar, Israel na maenoe ya Palestina yanayokaliwa na Israeli, Ukraine, Urusi na Yemen.
• Wakimbizi na wanawake pamoja na wasichana waliokimbia makazi yao wanaendelea kuwa katika hatari kubwa zaidi.
Kuorodheshwa kwa Israel |
|
Patten amesema kuorodheshwa huko kulitokana na mifumo iliyothibitishwa ya ubakaji na aina nyingine za ukatili wa kingono dhidi ya Wapalestina, hasa katika maeneo ya vizuizini, pamoja na vizuizi vinavyoendelea dhidi ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya ufuatiliaji.
|
Kuorodheshwa kwa Urusi |
|
Patten amesema vikosi vya jeshi na usalama vya Urusi viliorodheshwa baada ya Umoja wa Mataifa kuthibitisha matukio 310 ya ukatili wa kingono unaohusiana na migogoro, hasa dhidi ya wafungwa wa vita wa Ukraine na raia waliokuwa kizuizini.
|
Maendeleo chanya
Patten amebainisha kupungua kwa matukio yaliyothibitishwa yaliyohusishwa na Polisi wa Taifa wa Congo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, akieleza kuwa hali hiyo ilitokana na ushirikiano kati ya serikali ya DRC na Umoja wa Mataifa.
Kutokana na maendeleo hayo, Katibu Mkuu ameonesha nia ya kuzingatia kuiondoa polisi hiyo kwenye orodha ya viambatisho iwapo maendeleo yataendelea.
Hitimisho
Patten amewataka waandishi wa habari na nchi wanachama kutozingatia tu ni pande zipi zimeorodheshwa, bali kuwazingatia manusura wenyewe. “Ukatili wa kingono unaohusiana na migogoro bado ni janga la kimataifa linalohitaji uwajibikaji, msaada unaoweka manusura mbele, na umakini endelevu wa kimataifa.”
