Siku ya Kimataifa ya walinda amani wa UN yamulika dharura ya kuwekeza katika amaniSiku ya Kimataifa ya walinda amani wa UN yamulika dharura ya kuwekeza katika amani

Leo ikiwa ni siku ya kimataifa ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu António Guterres katika zama za sasa za ongezeko la mivutano na mizozo, ulinzi wa amani ni njia iliyothibitishwa na yenye gharama nafuu ya kurejesha utulivu na matumaini.

Ufadhili wa uhakika na utashi wa kisiasa unatakiwa

Katika ujumbe wake wa siku hii ambayo kauli mbiu ni wekeza katika amani,  Guterres amesema ili ulinzi wa amani uweze kufanikisha jukumu hilo, unapaswa uungwaji mkono endelevu kisiasa na ufadhili wa kifedha unaoaminika.

Ametumia ujumbe wake kukumbuka walinda amani wa zamani na wa sasa na kuthibitisha tena “wajibu wetu wa pamoja wa kuheshimu na kuimarisha kazi yao. Tunatoa heshima kwa takribani walinda amani 4,500 waliopoteza maisha tangu mwaka 1948, wakiwemo 59 waliofariki mwaka jana. “

Katibu Mkuu amesema hakuna mlinda amani anayepaswa kufa akiwa anahudumia ajenda ya amani na kwamba, “mashambulizi dhidi ya walinda amani ni ukiukwaji mkubwa wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu, na nchi wanachama zinapaswa kutekeleza wajibu wao wa kuhakikisha usalama na ulinzi wa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wakati wote.”

© UNMISS Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini, (UNMISS) ulianzishwa na kupatiwa majukumu yake na Baraza la Usalama la UN.

Usuli wa kuadhimisha mei 29

Siku hii huadhimishwa kukumbuka wanawake na wanaume wote wanaohudumu katika operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa, na kuwakumbuka wale waliopoteza maisha yao kwa ajili ya amani.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilianzisha siku hii mwaka 2002 na kuchagua tarehe 29 Mei kwa kuwa ndiyo siku ambayo mwaka 1948 Baraza la Usalama lilianzisha operesheni ya kwanza ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa, huko Mashariki ya Kati ikiwa na jukumu la kusimamia usitishaji vita eneo hilo.

Katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, maadhimisho ya mwaka huu yatafanyika Ijumaa, tarehe 5 Juni 2026.

Watakaopokea tuzo na nishani

Siku hiyo, Katibu Mkuu ataweka shada la maua kwa heshima ya walinda amani na kuongoza hafla ambayo Medali ya Dag Hammarskjöld itatolewa kwa walinda amani 68 wa kijeshi, polisi na raia waliopoteza maisha wakiwa kazini, wakiwemo 59 waliofariki dunia mwaka jana.

Umoja wa Mataifa Sejenti Matias Reyes wa Uruguay atapokea Tuzo ya Kapteni Mbaye Diagne kwa Ujasiri wa Kipekee.

Katika hafla maalum, Katibu Mkuu pia atatoa “Medali ya ujasiri wa kipeke ya Kapteni Mbaye Diagne, na mtunukiwa ni Koplo Matias Reyes wa Uruguay kwa kazi yake yake huko Goma, jimboni Kivu Kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wakati wa kilele cha mgogoro mwanzoni mwa mwaka 2025.

Halikadhalika marehemu Sergii Prykodko wa Ukraine aliyekuwa mkandarasi binafsi katika Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) ambaye aliuawa wakati wa operesheni ya kuwaokoa wanajeshi waliokuwa wamezingirwa mwezi Machi mwaka jana.

Katibu Mkuu pia atatoa tuzo kwa Mtetezi wa Kijeshi wa Masuala ya Kijinsia wa Mwaka 2025, Meja Abhilasha Barak wa India, anayehudumu katika Kikosi cha Muda cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon (UNIFIL), na kwa Afisa wa Polisi Mwanamke wa Mwaka wa Umoja wa Mataifa, Stephanie Königs wa Ujerumani, aliyekuwa akihudumu UNMISS.

Kauli ya Jean-Pierre Lacroix

Mkuu wa Idara ya Umoja wa Mataifa ya Ulinzi wa Amani, Jean-Pierre Lacroix akizungumzia siku hii amesema, “katika kipindi cha kuongezeka kwa migogoro na kupungua kwa rasilimali, walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanaendelea kulinda raia, kuzuia kuongezeka kwa vurugu, na kudumisha matumaini katika baadhi ya mazingira magumu zaidi duniani.”

© UNIFIL/Pasqual Gorriz Jean-Pierre Lacroix (katikati kulia), Naibu wa Katibu Mkuu na Mkuu wa Operesheni za Ulinzi wa Amani, akizungumza na walinda amani waliotumwa kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon, UNIFIL.

Hivyo amesema kuwekeza katika ulinzi wa amani ni kuwekeza katika utulivu, kinga dhidi ya migogoro, na uwezekano wa amani yenyewe.

Idadi ya walinda amani

Leo hii, zaidi ya walinda amani 50,000 wa kiraia, kijeshi na polisi wanahudumu chini ya bendera ya Umoja wa Mataifa katika baadhi ya mazingira magumu zaidi duniani, ambapo migogoro inazidi kuwa tata, ya muda mrefu, na kuathiriwa na vitisho vipya, ikiwa ni pamoja na matumizi mabaya ya zana za kidijitali na kusambazwa kwa taarifa hatarishi.

Jumla ya nchi 118 kwa sasa zinachangia maafisa wa kijeshi na polisi kwenye misheni 11 za kulinda amani.

Matukio yatarushwa moja kwa moja kupitia televisheni ya mtandaoni ya Umoja wa Mataifa https://webtv.un.org.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *