.

Wanafunzi wanane wa shule ya upili ya wasichana ya Utumishi, eneo la Gilgil nchini Kenya wanazuiliwa na polisi kuhusiana na mkasa wa moto wa bweni ambao ulisababisha vifo vya wanafunzi 16 usiku wa kuamkia Alhamisi wiki hii.

Baadhi ya wazazi bado wanahangaika kujua kuhusu walipo watoto wao, huku serikali ikijitahidi kuonyesha kuwa imechukua hatua licha ya kuendelea kukosolewa vikali.

Moto ulisababishwa na nini?

.

Chanzo cha picha, Shutterstock

Uchunguzi wa awali unaashiria kwamba moto huo uliwashwa kimakusudi, kwa mujibu wa taarifa ya wizara ya elimu.

Kwa mujibu wa polisi, moto huo ulianza majira ya saa saba usiku kwa saa za Afrika Mashariki na kuteketeza bweni lililokuwa na takribani wanafunzi 220.

Zaidi ya wanafunzi 800 walikuwa katika shule hiyo wakati wa tukio hilo.

Waziri wa Elimu Julius Ogamba alisema moto huo ulianzia katika ghorofa ya kwanza ya bweni hilo, ambalo liliharibiwa kabisa.

Kamanda wa polisi Masoud Mwinyi alisema baadhi ya wanafunzi walikimbia kuelekea maeneo ya karibu kutokana na hofu na mshtuko.

Wanafunzi 16 walifariki kutokana na mkasa huo, huku 79 wakiuguza majeraha.

Ni nani wa kulaumiwa?

.

“Watakaopatikana na hatia, watashtakiwa kulingana na sheria za nchi… Usimamizi wa shule haukufuatilia kanuni za usalama kama zilivyonakiliwa katika sheria za usalama shuleni, na vilevile sheria za kimsingi za elimu. Kwa mfano, bweni lililoathirika lilikuwa na wanafunzi kupita kiasi na mlango mmoja ulikuwa umefungwa, kinyume na sheria za usalama,” alisema Waziri Ogamba.

Aliongeza kwamba waalimu wawili walikuwa wamepata habari za awali kuhusu njama ya baadhi ya wanafunzi wa kidato cha tatu ila hawakuchukua hatua yoyote.

Bodi ya usimamizi wa shule ya utumishi imevunjwa, huku tume ya kuwaajiri waalimu TSC ikichukua hatua za kumuadhibu mwalimu mkuu wa shule hiyo kwa tuhuma za kutoangazia kanuni za usalama shuleni.

Kwanini Kenya ina historia mbaya ya kutofuatwa kwa kanuni za usalama shuleni?

Mojawapo ya kanuni muhimu ni kwamba kila bweni katika shule nchini Kenya linafaa kuwa na milango miwili katika kila upande, na mwingine wa dharura katika eneo la katikati, huku kila njia ya mlango ikiwa na upana wa futi 5.

Aidha milango inafaa kufunguka kuelekea nje, na madirisha yanafaa kufunguka kwa urahisi kwa nje na hayafai kuwa na vyuma (grills).

Mtaalamu wa masuala ya elimu Emmanuel Manyasa anasema kwamba kanuni zilizopo pia zinatumiwa kuzuia uwajibikaji.

“Kanuni moja kati ya zile zilizowekwa ni kwamba hakuna mgeni anayeruhusiwa kuingia kwenye bweni. Kwa njia moja hiyo ni kanuni nzuri. Lakini shule nyingi zinatumia kanuni hii kuzuia hata wazazi wanaozuru shule kuonyeshwa ni wapi watoto wao wanapolala,” anasema Manyasa.

.

Moto katika shule za bweni si jambo geni nchini Kenya.

Mwaka 2001, wanafunzi 67 walifariki katika shule ya Kyanguli katika eneo la Machakos baada ya bweni kuteketekea kwa moto, tukio ambalo linatajwa kuwa baya zaidi katika historia ya shule nchini humo.

Mnamo 2017, wasichana kumi walikufa kutokana na moto katika bweni la shule ya Moi Girls jijini Nairobi.

Mwaka 2024, watoto 21 walikufa kutokana na moto katika bweni la Hillside Endarasha katika eneo la kati mwa Kenya.

Baada ya tukio hilo, tathmini ya Wizara ya Elimu ilibaini kuwa shule nyingi zilikuwa na mabweni yenye madirisha ya nondo, milango michache ya kutokea na milango iliyokuwa ikifunguka kuelekea ndani, hali iliyokuwa ikihatarisha usalama wa wanafunzi wakati wa dharura.

Msongamano mkubwa wa wanafunzi mabwenini pia ulitajwa kuwa moja ya sababu zinazochangia idadi kubwa ya vifo wakati wa majanga ya moto.

Mwaka 2021, Wizara ya Elimu nchini Kenya ilisema kulikuwa na matukio 126 ya uchomaji moto mashuleni kati ya Januari na Novemba 2020 pekee.

Wakosoaji wanasema kwamba baada ya visa hivi, maisha huendelea kama kawaida na masuala ya usalama shuleni kutupwa katika kaburi la sahau hadi pale janga lingine litakapotokea.

“Ni sharti nchi ya Kenya ikome kuchukulia visa hivi vya moto shuleni kama ajali za kawaida. Visa hivi ni dalili ya jambo nzito zaidi – utepetevu uliokithiri. Kenya haikabiliwi na tatizo la ukosefu wa tume za uchunguzi, inakabiliwa na ukosefu wa uwajibikaji,” anasema Mutinda Musyimi, Mkuu wa masuala ya wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Daystar.

Shule za bweni zinafaa kufutwa kabisa?

Baadhi wamehoji kwamba shule za bweni hazifai, na zinafaa kufutwa maana visa vya moto vimeongezeka katika shule za aina hii.

Lakini wataalamu wa elimu wanasema hiyo sio suluhu, kwani shule hizo zina nafasi yake.

“Kuna sehemu za taifa hili letu ambapo watoto hawawezi kusomea katika shule za kutwa kwasababu za kiusalama, umbali kati ya shule na nyumbani wanakotoka, na kadhalika,” anasema Manyasa.

Aidha wanasema serikali inafaa kuonyesha kuwa inaweza kuadhibu wale wanaosababisha maafa shuleni, na kuwahakikishia watoto usalama wakiwa shuleni, njiani na hata nyumbani.

Imehaririwa na Asha Juma

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *