
Dar es Salaam. Wakati bei ya mafuta ghafi katika soko la dunia ikishuka hadi kufikia dola 87.3 kwa pipa leo Mei 30 kutoka zaidi 112.9 Aprili 7 mwaka huu, wachumi wamesema ni ngumu kuona mabadiliko hayo moja kwa moja katika soko la Tanzania ndani ya muda mfupi.
Hiyo ni kwa sababu biashara inapofanyika haiangalii bei ya bidhaa pekee bali hujumlisha gharama zote ikiwemo usafirishaji, bima na tozo nyingine za Serikali.
Tanzania ilianza kushuhudia ongezeko la bei za mafuta Aprili mwaka huu kufuatia mapigano ya Mashariki ya kati ambayo yalisababisha kushambuliwa kwa visima vya mafuta, maghala ya kuhifadhi mafuta na viwanda vya kusafisha mafuta.
Mapigano hayo yalileta athari za ongezeko la gharama za usafirishaji, bidhaa na huduma.
Hali hiyo iliifanya Serikali kutoa ruzuku ya Sh259 kwa kila lita moja ya mafuta ya dizeli ili kupunguza makali kutokana na umuhimu wake katika shughuli za kiuchumi ikiwemo uzalishaji viwandani, usafirishaji wa bidhaa na huduma za usafiri wa umma.
Akizungumzia suala hilo, Mtaalamu wa uchumi, Oscar Mkude amesema mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la dunia yanaweza yasiathiri moja kwa moja bei za rejareja kwa kiwango kinachoonekana mara moja kwa mlaji.
“Watu wengi wanaposhuhudia bei ya mafuta ghafi ikishuka duniani, hutegemea bei za mafuta kwenye vituo vya mafuta zipungue kwa kiwango kikubwa, lakini hali halisi si hivyo,” amesema.
Amesema bei ya mwisho anayolipa mlaji hutokana na mkusanyiko wa gharama mbalimbali, si bei ya mafuta pekee kwani mfanyabiashara huzingatia gharama za kununua mafuta, usafirishaji, bima ya magari yanayobeba mafuta, tozo mbalimbali za serikali na gharama nyingine za uendeshaji kabla ya kuamua bei ya kuuza.
“Ndiyo maana hata kama bei ya mafuta ghafi ikipungua kwa asilimia katika soko la dunia, si lazima mlaji aone punguzo la asilimia 10 au zaidi kwenye bei ya rejareja. Inawezekana gharama nyingine katika mnyororo wa usambazaji zimeongezeka na kufidia sehemu ya punguzo hilo,” amesema.
Alitolea mfano, kampuni za bima akisema huenda ziliongeza viwango vyao vya malipo jambo ambalo linalofanya gharama za usafirishaji kuongezeka au tozo nyingine zikabadilika.
“Hivyo, mfanyabiashara analazimika kuingiza gharama hizo zote katika hesabu yake ya mwisho ya bei. Kazi ya mfanyabiashara ni kufanya biashara kwa faida. Ikiwa atalazimishwa kuuza kwa kuzingatia bei ya mafuta duniani pekee bila kuhesabu gharama zake zote, anaweza kuendesha biashara kwa hasara,” amesema.
Na hapo ndiyo Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) huingia kwa kuangalia gharama ambazo mfanyabiashara ametumia hadi kufikisha mzigo na yeye kuzitumia kuweka bei kikomo katika namna ambayo haitamuathiri huku akimlinda mlaji kwa kuhakikisha bei anayopewa haimnyonyi.
Mkude anayasema haya wakati ambao kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma nchini kwa mwezi Aprili 2026 ulifikia asilimia 4.0 kutoka asilimia 3.2 kwa mwaka ulioishia mwezi Machi, 2026 ikichangiwa zaidi na kuongezeka kwa mfumuko wa bei wa usafiri na bidhaa za vyakula.
Mchambuzi wa Uchumi, DK Lutengano Mwinuka amesema kuna kanuni ambazo hutumika kukokotoa bei za mafuta nchini hivyo bei ya wiki ijayo inatokana na bei kioo iliyokuwapo mwezi mmoja nyuma.
“Kama ilishuka kwa mwezi mmoja nyuma inaweza kuwa na nafuu kidogo, kama muda waliochukua ni ule wa bei ilipokuwa juu inaweza kuwa tofauti. Hilo litatokana na kanuni inayotumika japokuwa kuna dalili za kuwapo na ahueni katika hili,” amesema.
Mtaalamu wa Uchumi na Biashara, Dk Eliaza Mkuna amesema mabadiliko ya bei ya mafuta katika soko la dunia hayawezi kutafsiriwa moja kwa moja kuwa mabadiliko ya haraka ya bei katika soko la ndani kwa sababu kuna mambo mengi ya kisera na kiuchumi yanayopaswa kuzingatiwa kabla ya maamuzi kufanyika.
Amesema moja ya mambo muhimu ambayo huangaliwa ni kiwango cha akiba ya mafuta kilichopo nchini akieleza kuwa ikiwa mafuta yaliyopo yalininuliwa kwa gharama kubwa, bei inaweza kuendelea kubaki juu hadi akiba hiyo itakapomalizika kabla ya mafuta mapya yaliyonunuliwa kwa bei ya chini kuanza kutumika sokoni.
“Serikali pia hulazimika kuangalia athari za mabadiliko hayo kwenye mapato ya kodi na tozo mbalimbali zinazohusiana na sekta ya mafuta katika baadhi ya mazingira, mabadiliko ya haraka ya bei yanaweza kuathiri makadirio ya mapato ya Serikali au mipango mingine ya kifedha inayotegemea sekta hiyo,” amesema.
Dk Mkuna amesema si kila mabadiliko ya bei yanayotokea katika soko la dunia huwa ya kudumu baadhi ni ya muda mfupi na mengine ya muda mrefu, hivyo yanahitaji uchambuzi wa kina ili kubaini kama ni mwenendo wa kudumu au ni mabadiliko ya mpito kabla ya kuchukua hatua za kisera.