Wakati Mbeya City ikifuta likizo kwa wachezaji ili kuendelea na mazoezi kujiandaa na mechi tano zilizobaki, vigogo wa juu wa timu hiyo wamefika mazoezini kuongeza hamasa, morali na nguvu kwa mastaa kuhakikisha wanafanya vizuri.

Viongozi waliofika katika uwanja wa mazoezi Isyesye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Justice Kijazi na Afisa Mtendaji Mkuu (CEO), John Kilua ambapo pamoja na mambo mengine, wamefanya mazungumzo na wachezaji na benchi la ufundi kwa takribani dakika 60.

Mbeya City inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya, haiko nafasi nzuri katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa imekusanya pointi 22 na kuwa nafasi ya 14, imebakiza dakika 450 sawa na mechi tano kujua hatma yake.

Katika michezo mitano iliyobakiza, itacheza tatu nyumbani ikianza Juni 13 dhidi ya Mtibwa Sugar, kisha kuivaa Simba (Juni 18), baadaye kwenda ugenini dhidi ya Pamba Jiji (Juni 24) na Dodoma Jiji (Juni 27) na kumalizia nyumbani dhidi ya TRA United (Juni 30).

Kwa sasa Ligi Kuu imesimama kupisha kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) ambapo itarejea Juni 12, 2026 kwa timu tatu kushuka uwanjani kuwania pointi tatu kujiweka pazuri kwenye msimamo.

Akizungumza katika mazoezi hayo, Kocha Mkuu wa Mbeya City, Salum Mayanga, amesema wameamua kuendelea na maandalizi kwa sababu hawako sehemu nzuri na presha ni kubwa.

Amesema kwa sasa hesabu zao ni kushinda kila mechi iliyo mbele yao akishukuru wadau na mashabiki kwa namna wanavyoendelea kuisapoti timu hiyo akiwahakikishia kubaki Ligi Kuu.

“Tunajua tunakutana na timu zenye malengo tofauti na sisi tunayo malengo yetu, hivyo tunaendelea kujipanga na ndio maana tumesitisha likizo ili kurekebisha tulipokosea tuweze kumaliza vyema mechi zilizobaki,” amesema Mayanga.

Nahodha wa timu hiyo, Eliud Ambokile, amesema wanafahamu kipindi walichopo hivi sasa lakini kinachotakiwa ni vitendo na si maneno kwa sasa akieleza kuwa wachezaji wote wako timamu na tayari kuinusuru City kutoshuka daraja.

“Kwa sasa inahitajika vitendo na siyo maneno, tumezungumza wachezaji na tunaendelea kujadiliana kuhakikisha morali inabaki vile vile ya kushinda michezo hii iliyobaki, hatujakata tamaa na bado tuna nafasi,” amesema straika huyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *