
KOCHA Mkuu wa Muembe Makumbi, Sheha Khamis amesema ushindani wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) msimu huu 2025-2026 umekuwa mgumu zaidi ikilinganishwa na misimu iliyopita na hiyo inatokana na kila timu kutokuwa tayari kupoteza.
Pia alisema licha ya timu tatu kukimbizana pale juu ya msimamo wa ligi hiyo ambazo ni KVZ inayoongoza na pointi 58, JKU (pointi 52) na Fufuni (pointi 48), bado hakuna yenye uhakika wa kuchukua ubingwa kutokana na tofauti ya alama zilizopishana.
“Ligi ya msimu huu ni ngumu sana kwa sababu timu zimepishana alama chache na kusababisha kila mechi kuwa na ushindani wa kupambana kupata pointi tatu kujiweka sawa kwenye msimamo,” alisema.
Katika mechi tatu zilizopita, Muembe Makumbi City imepata sare mbili mfululizo dhidi ya Polisi (1-1) na Zimamoto (0-0), ikiifunga Malindi mabao 3-1, huku Sheha akisema kushindwa kuondoka na ushindi dhidi ya Polisi na Zimamoto, ni kutofikia malengo yao.
Muembe Makumbi City imebakisha michezo mitatu kumaliza msimu huu wa Ligi Kuu Zanzibar dhidi ya Mafunzo, Fufuni na New Stone Town.