
Dar es Salaam. Wakati juhudi za kudhibiti dawa za kulevya zikiendelea kuzaa matunda nchini, takwimu mpya zimeibua sura nyingine ya tatizo hilo baada ya kuonyesha kuwa Watanzania 28 walikamatwa katika nchi mbalimbali duniani mwaka 2025 kwa tuhuma za kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Ripoti ya Hali ya Dawa za Kulevya nchini Tanzania ya mwaka 2025 inaonyesha kuwa Zambia ndiyo nchi iliyoongoza kwa kuwakamata Watanzania wengi zaidi, ikiwa na watuhumiwa 20.
Nchi nyingine zilizoripoti kuwakamata Watanzania ni Botswana waliokamata wawili, Msumbiji wawili, huku Mauritius, Japan, Ufaransa na Shelisheli kila moja ikimkamata Mtanzania mmoja.
Mbali na Watanzania wanaokamatwa nje ya nchi, raia wa kigeni 14 walikamatwa nchini mwaka 2025 kwa tuhuma za kujihusisha na dawa za kulevya.
Waliokamatwa wanatoka China wawili, Sri Lanka wawili, Uingereza wawili, huku Lebanon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Marekani, Nigeria, Ujerumani, Kenya, Msumbiji na Uganda kila nchi ikiwakilishwa na mtuhumiwa mmoja.
Takwimu hizo zinakuja wakati mamlaka nchini zikieleza kuendelea kuimarika kwa juhudi za kudhibiti biashara ya dawa za kulevya, hatua iliyochangia kuongezeka kwa kiasi cha dawa hizo kinachokamatwa.
Akizungumza na Mwananchi Kamishna Jenerali wa Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Aretas Lyimo amesema Watanzania hao watahukumiwa kulingana na sheria za nchi walizokamatwa.
“Hawa watakuhukumiwa kulingana na sheria za nchi walizokamatwa, kila nchi ina adhabu yake kwa makosa ya dawa za kulevya na inawezekana huko walikokamatwa ni nafuu kuliko Tanzania maana hapa kwa sheria yetu ukikamatwa na dawa za kulevya ni kifungo cha maisha.
“Halafu ukitolea mfano nchi ya Zambia ambayo wamekamatwa wengi, huko adhabu sio kubwa ndiyo maana wengi wanakimbilia huko kufanya biashara hiyo haramu wakiamini wakikamatwa watafungwa muda mfupi kisha watatoka,” amesema Lyimo.
Kuhusu aina ya watuhumiwa waliokamatwa nje amesema wengi wao ni wasafirishaji wadogo wadogo ambao wanabebeshwa mizigo kutoka eneo moja kwenda lingine.
Kamisha Jenerali Lyimo amesema kutokana na udhibiti mkubwa wa biashara hiyo, sasa hivi vigogo wa dawa za kulevya wanajificha kwa kufanya biashara hiyo kwa fedha mtandao.
“Watu wanaweza kuwasiliana na wauzaji kwa siri “dark webs”, kuagiza dawa mtandaoni na kuzipata bila kutambulika kwa urahisi. Majukwaa haya hutumia mifumo ya mawasiliano ya kificho na malipo kupitia sarafu za kidijitali (crypto currencies) ili kupunguza ufuatiliaji wa kifedha.
“Kitu kinachotusumbua kwa sasa ni hili, wanajificha kwenye dark web, ila tumeshawabaini na hivi karibuni tutaweka wazi maana tumewashawakamata huko huko,” amesema.
Kamishna Jenerali Lyimo amewataka Watanzania kujiweka kando na biashara ya dawa za kulevya kwa sababu mamlaka hiyo imeweka mtandao mathubuti kuhakikisha kila anayejihusisha anakamatwa.
“Hata dunia inakubali jitihada zinazofanywa na Tanzania katika kudhibiti biashara hii haramu, tuna vifaa na mitandao madhubuti kujua kila inapofanyika biashara ya dawa za kulevya hivyo ukiingia huko jiandae utakamatwa.
“Sasa hivi asilimia 70 hadi 80 ya kesi zinazoendelea mahakama ya mafisadi zinahusu dawa za kulevya, kule tumewapeleka wale wafanyabiashara wakubwa. Tumejidhatiti kweli kweli ndiyo maana sasa hivi huwezi kuona Heroin wala Cocaine mtaani,” amesema Lyimo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, jumla ya kilogramu 672.23 za heroin zilikamatwa nchini mwaka 2025, zikihusisha watuhumiwa 63, kati yao wanaume 54 na wanawake tisa.
Kiasi hicho ni kikubwa zaidi ikilinganishwa na kilogramu 433.16 zilizokamatwa mwaka 2024.
Kwa upande wa cocaine, kilogramu 4.89 zilikamatwa mwaka 2025 zikihusisha watuhumiwa 10, wakiwemo wanaume tisa na mwanamke mmoja.
Mwaka 2024, kiasi cha cocaine kilichokamatwa kilikuwa kilogramu 0.85 pekee, jambo linaloonyesha ongezeko kubwa la ukamataji ndani ya mwaka mmoja.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa ongezeko la heroin na cocaine zilizokamatwa limetokana na kuimarika kwa operesheni za ukamataji pamoja na elimu kwa jamii iliyochochea wananchi kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na biashara hiyo haramu.
Katika hatua nyingine, mashauri 1,124 ya dawa za kulevya yalifunguliwa katika mahakama mbalimbali nchini mwaka 2025.
Aidha, mashauri 1,373 yalimalizika katika kipindi hicho, yakiwemo yaliyokuwa yamefunguliwa miaka ya nyuma.
Kati ya mashauri hayo, Jamhuri ilishinda mashauri 1,058, ambapo watuhumiwa walitiwa hatiani na kuhukumiwa vifungo mbalimbali kwa mujibu wa sheria.
Wadau wanasemaje?
Mhadhiri wa Sosholojia katika, Dk Asha Mwakalobo, amesema kukamatwa kwa Watanzania katika mataifa mbalimbali ni ishara kuwa biashara ya dawa za kulevya imeendelea kutumia mitandao ya kimataifa inayowalenga zaidi vijana.
“Tunapaswa kuangalia si tu upande wa ukamataji, bali pia sababu zinazowasukuma baadhi ya vijana kuingia katika biashara hizi. Changamoto za ajira, tamaa ya kupata utajiri wa haraka na ushawishi wa makundi ya kihalifu ni mambo yanayohitaji kushughulikiwa,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha Ushauri kwa Vijana, John Mrema, amesema takwimu hizo zinapaswa kuwa onyo kwa jamii na familia kuongeza uangalizi kwa vijana wanaosafiri nje ya nchi kwa ahadi za kazi au biashara zisizoeleweka.
“Tumekuwa tukiona watu wakitumiwa kama wasafirishaji wa dawa bila kufahamu madhara ya kisheria yanayowakabili. Elimu ya kinga inapaswa kuanzia nyumbani, shuleni na katika maeneo ya kazi,” amesema.
Naye mchambuzi wa masuala ya usalama, Salum Khatib, amesema ongezeko la kiasi cha heroin na cocaine kinachokamatwa linaonyesha mafanikio ya vyombo vya dola, lakini pia linaashiria kuwa mitandao ya usafirishaji wa dawa hizo bado ipo na inaendelea kufanya majaribio ya kupenyeza mizigo nchini.
“Ushirikiano wa kikanda na kimataifa unapaswa kuongezwa zaidi. Dawa za kulevya ni uhalifu unaovuka mipaka, hivyo mapambano yake hayawezi kufanyika kwa nchi moja pekee,” amesema.
Wadau hao wamezitaka mamlaka kuendelea kuimarisha operesheni za kudhibiti dawa za kulevya huku zikiongeza uwekezaji katika elimu ya kinga, uundaji wa ajira na huduma za ushauri kwa vijana ili kupunguza uwezekano wa kuingia katika biashara hiyo haramu.