
Dar es Salaam. Waombolezaji mbalimbali aliyekuwa Ofisa Uhusiano Mkuu na Mkuu wa Itifaki wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Jackson Isdory, wamemwelezea namna alivyojitoa katika utumishi na kuwa msaada kwa wengine wakati wa enzi za uhai wake.
Shughuli hiyo ya wanajumuiya wa UDSM iliongozwa na Mkuu wa Chuo hicho na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, Spika Mstaafu Dk Tulia Ackson na viongozi wengine wa Serikali.
“Alikuwa mtu ambaye mara nyingi hakusikika akizungumza kwenye vipaza sauti wala kuonekana kwenye picha za mbele za matukio makubwa, lakini nyuma ya pazia ndiye aliyekuwa akihakikisha kila kitu kinaenda sawa.”
Hayo ni maneno yaliyojirudia mara kwa mara kutoka kwenye vinywa vya watu waliopata nafasi ya kuzungumza wakati wa kutoa salamu za rambirambi katika misa ya kumuaga.
Kifo cha Isdory kilichotokea Mei 27, 2026 kutokana na ajali ya gari kimeibua simulizi za viongozi mbalimbali ambao wamekiri hadharani kuwa wamepoteza mtu aliyekuwa kiungo muhimu katika kazi, ushauri na mahusiano ya taasisi.
Akizungumza kwenye misa ya kumuaga iliyofanyika katika Ukumbi wa Nkrumah UDSM, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema Isdory alikuwa miongoni mwa watumishi wachache waliokuwa wakifanya kazi kubwa kwa weledi wa hali ya juu huku wakibaki nyuma ya pazia.
“Tulimuona Isdory kama mtu mwenye weledi wa hali ya juu. Alifanya kazi ya uratibu na itifaki lakini tukio linapotokea huwezi kumuona,” amesema Mkenda.
Amesema uwezo wake ulimfanya afikirie kumhamishia Wizara ya Elimu, lakini hata viongozi wa UDSM hawakuwa tayari kumpoteza.
“Mara ya mwisho nilivyokuja chuo kikuu nilimwambia Profesa Anangisye kwa nini nisimchukue Isdory aende wizarani. Akanijibu, kama unataka kumchukua naomba usubiri muda wangu wa utumishi hapa uishe,” amesema.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo, amesema kwa miaka mingi Isdory alikuwa mtu aliyemsaidia kutambua namna kauli na matendo yake yalivyopokelewa na viongozi wa chuo.
“Nikiwa mwenyekiti wa UDASA, nimefanya kazi kwa nyakati mbalimbali nikifanya mikutano na wanahabari au kutoa matamko. Nikitaka kujua Makamu Mkuu wa Chuo ameipokeaje, nilikuwa namsogelea Isdory. Kwa kifupi alikuwa kioo changu, niishie wapi au wapi niko vizuri.”
Mkumbo amesema hata baada ya yeye kuwa waziri, Isdory aliendelea kusimamia misingi ya kazi yake kwa kumkumbusha umuhimu wa kufuata taratibu za itifaki.
Katika jumuiya ya kidiplomasia, Balozi Mbelwa Kairuki amesema kifo hicho kimeondoa kiungo muhimu kati ya UDSM na wadau wa sekta ya diplomasia.
“Isdory alikuwa mtu wa kutumainiwa katika jumuiya ya kidiplomasia. Alikuwa daraja kati ya chuo kikuu na wadau waliopo kwenye sekta ya diplomasia,” amesema.
Kairuki amesema wakati wote Isdory alikuwa tayari kusaidia na kuwezesha utekelezaji wa shughuli mbalimbali za ushirikiano.
“Tumeondokewa na daraja muhimu na kiungo muhimu katika utekelezaji wa majukumu yetu.”
Ndani ya Kanisa Katoliki, Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Toma wa Akwino, Padri Dk Joseph Mosha, amesema Isdory alitambulika kwa imani yake, utumishi na moyo wa kujitoa.
“Alikuwa tayari wakati wote kutimiza wajibu wake. Alijitoa bila kujibakiza na alifanya kazi bila kulalamika. Furaha yake ilikuwa kuona kila mtu amehudumiwa,” amesema.
Padri Mosha amesema maisha ya marehemu yanapaswa kuwa fundisho kwa wengine.
“Uwepo wako hapa duniani uwe taa inayoangaza, mafuta ya taa hiyo ni matendo yako.”
Makamu Mkuu Mstaafu wa UDSM, Profesa Rwekaza Mukandala, amesema Isdory alikuwa mmoja wa wahitimu bora wa Shule ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC) na baadaye kuwa mtumishi muhimu wa chuo hicho.
Amesema marehemu alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakitumika kuunganisha makundi mbalimbali ndani ya chuo kwa busara na uaminifu.
“Alikuwa kiunganishi akipeleka taarifa muhimu kwa mchujo na uaminifu kwa lengo la kujenga na si kubomoa,” amesema.
Kwa mujibu wa Mukandala, Isdory alikuwa na mchango mkubwa katika kutatua changamoto na kupunguza misuguano ndani ya UDSM, akitumia uwezo wake wa kusikiliza, kuchambua na kushauri.
Kwa zaidi ya miaka 20 aliyomfahamu, amesema jambo lililomtofautisha Isdory ni upole, unyenyekevu, uchapakazi na uaminifu wake.