
TAYARI kocha wa Simba, Steve Barker ameanza kuona vitu vya kiufundi katika miguu ya beki chipukizi Vedastus Masinde, jambo linalomshawishi kuendelea kumpa nafasi zaidi ya kuonyesha kiwango alichonacho.
Hayo yamejiri baada ya Barker kumpa nafasi beki huyo kucheza ambapo alitumika kwa dakika tisini dhidi ya Tanzania Prisons, huku zingine akijumuishwa kikosini ni dhidi ya Dodoma Jiji na Mashujaa.
Chipukizi huyo aliyetua Simba msimu huu akitokea TMA Stars inayoshiriki Ligi ya Championship huku pia akiwa mchezaji wa timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 20, amekuwa akipata ujuzi kwa mabeki wa kati wanaocheza ndani ya Simba akiwemo Rushine De Reuck.
Mei 10, 2026 baada ya mechi dhidi ya Tanzania Prisons ambapo Simba ilishinda kwa mabao 4-0 kwenye Uwanja wa KMC Complex jijini Dar es Salaam huku Masinde akicheza kwa dakika tisini, alisema ndoto yake ya kucheza Ligi Kuu Bara imetimia.
“Kocha ananipa nafasi ya kucheza, natakiwa kuitumia vizuri, timu inaposhinda tunakuwa tumecheza kitimu na tumeshinda kwa pamoja, jambo la msingi naendelea kushikilia kile ninachokifanya,” amesema.
Akizungumzia kiwango cha Masinde, Barker amesema: “Namuona ana vitu vingi na talenti kubwa, katika mechi alizocheza kafanya kazi nzuri, hilo linaendelea kunishawishi kuendelea kumpa nafasi zaidi.
“Anatakiwa kuendelea kupata uzoefu, kadri siku zinavyokwenda atakuwa anafanya mambo makubwa
yatakayokuwa msaada kwa timu na timu ya taifa, kikubwa awe na nidhamu na bidii.”
Kiraka wa zamani wa Simba, Azam, Namungo na Taifa Stars, Erasto Nyoni, amemzungumzia Masinde akisema: “Unaposajiliwa katika kikosi ukakutana na wazoefu, kocha akikupa nafasi unapaswa kufanya vitu vikubwa vitakavyobakia akilini mwake, wote tulianzia chini baadaye tukaja kuwa tegemeo, hivyo naamini Masinde akiendelea kutunza nidhamu atafika mbali.”