BAADA ya Timu ya Taifa ya Wasichana chini ya miaka 17, Serengeti Girls kupoteza mechi ya kwanza ya raundi ya pili katika kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Afrika Kusini, Jumapili hii ina kibarua cha kujiuliza ugenini.

Serengeti Girls itashuka Uwanja wa Lucas Moripe, Afrika Kusini saa 10 jioni kujiuliza kwa wenyeji wao hao baada ya kupoteza mechi ya kwanza nyumbani kwa mabao 2-0 Mei 23, 2026, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Hii ni raundi ya pili ya kufuzu Kombe la Dunia na ili Serengeti Girls ifuzu kwenda raundi ya tatu inahitaji kushinda mabao matatu kwa bila.

Akizungumza na Mwanaspoti, nahodha wa timu hiyo, Elizabeth John alisema wamezingatia kile walichoagizwa na kocha Bakari Shime kilichobaki sasa ni kumaliza kwenye dakika 90 zilizosalia.

Aliwaomba mashabiki wa Tanzania kuiombea timu hiyo ili iweze kufanya vizuri na kufuzu raundi inayofuata ambayo itawawezesha kucheza Kombe la Dunia.

“Tunajua ugumu wa mechi hiyo na hii ni kutokana na kupoteza mechi ya kwanza lakini niwahakikishie Watanzania kuwa kile ambacho kocha ametuelekeza naamini tunaenda kukifanyia kazi,” alisema Elizabeth na kuongeza.

“Mechi ya kwanza hatukujua mpinzani wetu anachezaje, hivyo ilikuwa ngumu kwetu lakini tayari tumefahamu ubora wa Afrika Kusini na udhaifu wake, hivyo tutautumia.”

Pamoja na Serengeti Girls kucheza ugenini, ina nafasi ya kufuzu kama itajipanga na kuhakikisha inatumia vizuri nafasi itakazotengeneza.

Kwa mujibu wa muundo wa mashindano hayo, timu nne zitafuzu kucheza Fainali za Kombe la Dunia Wanawake U-17, zitakazofanyika Oktoba 17 hadi Novemba 7, 2026 nchini Morocco.

Timu hizo zitacheza raundi tatu, hivyo Serengeti Girls ilifika hatua hiyo baada ya kuichakaza Botswana kwa jumla ya mabao 6-2 na kutinga raundi ya pili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *