Budapest, Hungary. Meneja wa Arsenal, Mikel Arteta, amesema walikuwa wamejiandaa mapema kwa uwezekano wa mchezo kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti, jambo lililosababisha beki Gabriel Magalhães kupewa jukumu la kupiga penalti ya tano katika mchezo huo wa fainali dhidi ya Paris Saint-Germain (PSG).

Akizungumza baada ya mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Arteta amesema uamuzi wa mpangilio wa wapigaji penalti ulifanywa kwa kuzingatia maandalizi na mazoezi yaliyofanyika kabla ya mechi.

Meneja wa Arsenal, Mikel Arteta wakati akitoka kuvishwa medali ya mshindi wa pili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya timu yake kupigwa kwa mikwaju 4-3 ya penalti katika fainali hiyo dhidi ya PSG. Picha na Mtandao

“Tulikuwa tumejiandaa na kufanya mazoezi kwa ajili ya wakati kama huu,” amesema Arteta alipoulizwa sababu ya Gabriel kuwa mpigaji wa tano wa penalti.

Mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Puskas Arena, Budapest, Hungary iliamriwa kwa mikwaju ya penalti baada ya dakika 120 za muda wa kawaida kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Arsenal ndio ilikuwa ya kwanza kupata bao katika mchezo huo kupitia kwa Kai Havertz mnamo dakika ya sita lakini PSG wakasawazisha katika dakika ya 65 kwa bao la Ousmane Dembele.

Beki wa Arsenal, Gabriel Magalhães wakati akitulizwa na Mbrazil mwenzake Maquinhos wa PSG baada ya kukosa mkwaju wa penalti katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya PSG, Mei 30, 2026. Picha na Mtandao

Pamoja na PSG kuonyesha kiwango bora na kulishambulia lango la Arsenal kama nyuki, hakukuwa na mabao ya ziada ndipo mikwaju ya penalti ikatumika kusaka mshindi.

PSG penalti zao nne zikawekwa kimiani na Goncalo Ramos, Desire Doue, Achraf Hakimi na Lucas Berardo huku Nuno Mendes akikosa.

Penalti tatu za Arsenal zikafungwa na Viktor Gyokeres, Gabriel Martinelli na Declan Rice huku Eberechi Eze na Gabriel Magalhaeis wakikosa.

Beki wa Arsenal, Gabriel Magalhães akionekana kuuzunika baada ya kukosa mkwaju wa penalti katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya PSG, Mei 30, 2026. Picha na Mtandao

Kwa kutwaa taji hilo, PSG inakuwa timu ya pili katika historia kutetea ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya ikifuata nyayo za Real Madrid ambayo ilikuwa ya kwanza kufanya hivyo.

Arsenal imeshindwa kufikia malengo yake baada ya kushindwa na PSG katika mchezo wa fainali uliokuwa na ushindani mkubwa, huku matokeo ya mikwaju ya penalti yakichangia kuamua hatma ya timu hizo.

Licha ya maumivu ya kutotwaa ubingwa huo, Arteta amewatetea wachezaji wake akisisitiza kuwa walifuata mpango uliowekwa na benchi la ufundi kabla ya mchezo.

Matokeo ya leo yameikumbushia Arsenal majonzi ya msimu wa 2005/2006 ambao ilikosa ubingwa wa mashindano hayo kwa kufungwa na Barcelona kwa mabao 2-1 katika fainali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *