Budapest, Hungary. PSG imetwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2025/2026 baada ya leo Jumamosi, Mei 30, 2026 kuibuka na ushindi wa mikwaju ya penalti 4-3 dhidi ya Arsenal.

Mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Puskas Arena, Budapest, Hungary iliamriwa kwa mikwaju ya penalti baada ya dakika 120 za muda wa kawaida kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Arsenal ndio ilikuwa ya kwanza kupata bao katika mchezo huo kupitia kwa Kai Havertz mnamo dakika ya sita lakini PSG wakasawazisha katika dakika ya 65 kwa bao la Ousmane Dembele.

Pamoja na PSG kuonyesha kiwango bora na kulishambulia lango la Arsenal kama nyuki, hakukuwa na mabao ya ziada ndipo mikwaju ya penalti ikatumika kusaka mshindi.

PSG penalti zao nne zikawekwa kimiani na Goncalo Ramos, Desire Doue, Achraf Hakimi na Lucas Berardo huku Nuno Mendes akikosa.

Penalti tatu za Arsenal zikafungwa na Viktor Gyokeres, Gabriel Martinelli na Declan Rice huku Eberechi Eze na Gabriel Magalhaeis wakikosa.

Kwa kutwaa taji hilo, PSG inakuwa timu ya pili katika historia kutetea ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya ikifuata nyayo za Real Madrid ambayo ilikuwa ya kwanza kufanya hivyo.

Matokeo ya leo yameikumbushia Arsenal majonzi ya msimu wa 2005/2006 ambao ilikosa ubingwa wa mashindano hayo kwa kufungwa na Barcelona kwa mabao 2-1 katika fainali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *