Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Afya, Dk Florence Samizi amesema zaidi ya asilimia 27 ya watoto wa kike hushindwa kwenda shule kutokana na kukosa mahitaji ya hedhi ikiwemo taulo za kike.

Kutokana na hali hiyo, amewataka wadau kushirikiana kuhakikisha wanawawezesha watoto wa kike kupata mahitaji hayo, ili wasikose masomo au kuacha shule kabisa.

Dk Samizi ameyasema hayo wilayani Kibondo,Mkoa wa Kigoma jana, wakati wa hafla maadhimisho ya Siku ya Hedhi Duniani, yaliyoambatana na kukabidhi taulo za kike zaidi ya 7,200 wilayani humo, iliyofanywa na Kampuni ya Softcare.

Amesema ukosefu wa taulo za kike na elimu sahihi kuhusu afya ya hedhi umekuwa ukiathiri kwa kiasi kikubwa mahudhurio ya wanafunzi wa kike shuleni, hali inayochangia kudorora kwa maendeleo yao ya kielimu.

Amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha watoto wa kike wanapata mahitaji hayo muhimu, ili kuwawezesha kusoma katika mazingira salama na yenye staha.

Aidha, ametoa wito kwa jamii, wazazi na walezi kushiriki kikamilifu katika kuwasaidia watoto wa kike kupata mahitaji ya msingi ya hedhi pamoja na kuwapa elimu sahihi itakayowawezesha kujitunza kipindi hicho.

Amesema msaada huo unatarajiwa kusaidia kuongeza mahudhurio ya wanafunzi wa kike shuleni na kupunguza changamoto zinazowakwamisha kufikia ndoto zao za kielimu katika Wilaya ya Kibondo na maeneo mengine ya Mkoa wa Kigoma.

Taulo hizo zimetolewa na kampuni ya software na zitakabidhiwa kwa zaidi ya shule 13 wilayani humo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja Masoko na Mawasiliano wa Doweicare Technology Limited Tanzania inayozalisha taulo za Softcare, Lucia Msami, amesema msisitizo wao ni hedhi salama, huduma za uzazi na usafi ni haki ya msingi kwa kila mwanamke na msichana.

“Softcare tunaamini kuwa hedhi salama, huduma za uzazi na usafi ni mahitaji ya msingi kwa kila mwanamke na msichana. Kupitia taulo za kike za Softcare, tunaendelea kusaidia familia za Kitanzania kwa bidhaa bora za usafi na huduma binafsi,” amesema.

Amesema moja ya changamoto inayoikabili jamii ni matumizi ya pedi zisizofaa au katika maeneo yenye upungufu wa maji safi, jambo linaloweza kusababisha athari za kiafya.

Tangu mwaka 2022, amesema kampuni hiyo imewafikia zaidi ya wanafunzi 50,000 kupitia elimu ya afya ya hedhi na kampeni za uhamasishaji na kuwasaidia zaidi ya wanawake 300,000 waliopata huduma katika hospitali mbalimbali nchini.

Amesema wametoa taulo za watoto katika kituo cha afya cha  Malagarasi na Hospitali ya Wilaya ya Kibondo kwa muda wa miezi mitatu, lengo kuwasaidia wajawazito wanaoenda kujifungua.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *