Dar es Salaam. Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) Tanzania, limeingia makubaliano na taasisi kumi za elimu ya juu kwa ajili ya kuwajengea uwezo vijana na kuchochea maendeleo endelevu.

Ushirikiano huo uliotiwa saini mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, unalenga kurasimisha na kuongeza nguvu katika programu mbalimbali za wanafunzi, uendelezaji wa ubunifu, mijadala ya kimkakati na ushirikiano wa karibu kati ya sekta ya maendeleo na taaluma.

Vyuo na taasisi zilizosaini makubaliano hayo ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Chuo Kikuu cha Mzumbe, Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT).

Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Chuo cha Ufundi Arusha (ATC), Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine Tanzania (SAUT), Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Afrika ya Nelson Mandela (NM-AIST).

Kwa mujibu wa UNDP, Tanzania huzalisha karibu wahitimu 60,000 kila mwaka, lakini bado vijana wengi hukabiliwa na changamoto ya kuingia katika soko la ajira kutokana na ukosefu wa uzoefu wa kazi na uhusiano mdogo kati ya taasisi za elimu na waajiri.

Mkataba huo wa mashirikiano (MoUs) unatarajiwa kuweka mfumo thabiti wa muda mrefu utakaosaidia kuziba pengo kubwa lililopo sasa kati ya kile kinachofundishwa darasani (nadharia) na uhalisia uliopo katika soko la ajira lililojaa ushindani mkubwa.

Mkakati huo mkubwa unatekelezwa chini ya Programu ya UNDP ya Kukuza Vipaji vya Vijana inatajwa kuwa kiunganishi muhimu kinachokutanisha vyuo vikuu, taasisi za maendeleo ya kimataifa, na wadau wa sekta binafsi nchini.

Kupitia ushirikiano huo, wanafunzi na wahitimu wa hivi karibuni watapata fursa adhimu za kupata mafunzo ya vitendo, ushauri wa kitaalamu kutoka kwa wabobezi wa tasnia mbalimbali, pamoja na kuwezeshwa katika mawazo yao ya kibunifu ili kugeuzwa kuwa fursa za kiuchumi.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini mwishoni mwa wiki, Mwakilishi Mkazi wa UNDP Tanzania, Shigeki Komatsubara amesema vijana wanahitimu vyuo vikuu wakiwa na elimu ya kitaaluma lakini bila uzoefu wa kutosha unaohitajika katika mazingira ya kazi.

Amesema dunia ya sasa inabadilika kwa kasi kutokana na maendeleo ya teknolojia, ubunifu na mabadiliko ya uchumi, hali inayohitaji vijana kuwa na uwezo wa kubadilika na kujifunza ujuzi unaohitajika katika soko la ajira.

“Mpito kutoka chuoni kwenda kwenye dunia ya kazi haupaswi kuachwa kwa bahati. Vijana wanapaswa kuhitimu wakiwa na zaidi ya shahada pekee; wanahitaji uzoefu, mwanga wa mwelekeo wa maisha yao na uwezo wa kukabiliana na changamoto za dunia ya sasa,” amesema Komatsubara.

Amesema ushirikiano unakusudia kuimarisha nafasi ya vyuo vikuu katika kuchangia maendeleo ya Taifa kupitia tafiti, ubunifu na utatuzi wa changamoto mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Ofisa utumishi na Meneja wa Maendeleo ya Vipaji UNDP, Veronika Sigalla amesema lengo kubwa ni kutengeneza njia salama na zenye uhakika zitakazowawezesha vijana wetu kuvuka salama kutoka katika mifumo ya elimu kwenda kwenye ajira rasmi, ujasiriamali, na nafasi za uongozi.

“Tunawasaidia kuwajengea uwezo wanafunzi wanaotoka chuoni ili waweze kushindana kwenye soko la ajira la sasa, pia kuhakikisha waajiri wanapata wafanyakazi walioandaliwa ipasavyo” amesema.

Amesema wanazo programu mbalimbali kama Funguo huku lengo ikiwa ni kuwajengea vijana uwezo wa ajira, ubunifu, uongozi na ujuzi wa vitendo unaoendana na mahitaji ya soko la ajira la sasa.

UNDP inaamini kuwa kupitia ushirikiano huo, wanafunzi wataweza kupata mazingira bora ya kujifunza kwa vitendo na kujiandaa mapema kwa maisha baada ya kuhitimu masomo yao.

Akizungumza kwa niaba ya taasisi zilizoshiriki hafla hiyo, Naibu Mkuu wa Taaluma, Utafiti na Ushauri wa chuo cha IAA, Grace Temba amesema ushirikiano utaongeza fursa kwa wanafunzi kuunganisha maarifa ya darasani na mazingira halisi ya kazi.

“Vyuo vina jukumu kubwa la kutoa maarifa ya kitaaluma, lakini ushirikiano wa namna hii unasaidia kuwaunganisha wanafunzi na uzoefu wa vitendo, ushauri wa kitaalamu na fursa pana zaidi zinazoweza kuwasaidia katika maisha yao ya baadaye,” amesema.

Mbali na hafla ya utiaji saini, tukio hilo pia lilihusisha maonesho ya ubunifu yaliyoandaliwa na vijana na wanafunzi wanaoungwa mkono na UNDP, walipata nafasi ya kuonesha miradi mbalimbali ya kiteknolojia, biashara bunifu na mawazo yanayolenga kutatua changamoto za maendeleo nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *