Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba amesema Serikali inatafuta suluhisho la kuporomoka kwa bei za mazao ya biashara yanayouzwa nje kwa kusaka soko kwa nchi washirika ili kumaliza kilio cha wakulima wa mazao hayo ikiwemo dengu, tumbaku na chai.
Akitaja sababu za kuporomoka kwa bei amesema vita vya Ukraine na Russia, kupaa kwa bei ya mafuta, mzozo wa Mashariki ya kati, Uviko19 na uhaba wa fedha za kigeni yote yamechangia kuathiri mnyororo mzima wa usafirishaji duniani.
Kauli hiyo ameitoa baada ya kupokea kilio cha kuporomoka kwa bei ya dengu kutoka kwa wananchi leo Jumapili, Mei 31, 2026 alipokuwa akizungumza na wananchi wa Itigi, mkoani Singida ambapo awali alikagua maendeleo ya ujenzi wa Barabara ya Itigi-Makongorosi.
“Nimepokea hoja ya kuporomoka kwa bei ya dengu, mazao haya ambayo soko lake ni la nje maeneo mengi huwa yanaathiriwa na matukio yanayotokea hasa katika miaka hii mitano ambayo inaathiri usafirishaji wa bidhaa na soko lazima lipate madhara. Matatizo yanaletwa na bima kupaa, hatari kwa wanunuzi na meli kusafiri.
“Mazao mengine kama chai, tumbaku kule Tabora kote kuna shida. Kama minyororo wa usafirishaji umeathirika na soko pia litaathirika. Sisi kama Serikali tunaendelea na mazungumzo na baadhi ya nchi washirika wetu wakubwa wa biashara za mazao tutaenda kurejea katika hali nzuri,” amesema.
Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba akipokea taarifa ya utekelezaji wa ujenzi wa Barabara ya Makongolosi–Rungwa–Itigi–Mkuiwa, sehemu ya Noranga (Doroto)–Itigi (Mlongojii), kutoka kwa Mkurugenzi wa Miradi wa Wakala ya Barabara Tanzania (Tanroads), Mhandisi Japherson Nnko, wakati wa ziara ya kukagua mradi huo wenye urefu wa kilomita 25 unaojengwa katika Halmashauri ya Itigi, Wilaya ya Manyoni mkoani Singida kwa gharama ya Sh29.6 bilioni, Mei 31, 2026. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Amesema jitihada zinaendelea kuhakikisha bei zisizidi kushuka zaidi ya viwango hadi wakulima wakafilisika.
Akitolea mfano wa jitihada za kuwaponya wakulima amesema kufutwa kwa uuzwaji wa lumbesa unaowanyonya wakulima, adha kujenga maghala mengi kuwapunguzia wakulima mzigo wakusafirisha mazao kwa umbali mrefu kutafuta soko.
Awali, Mbunge wa Itigi, Yohana Msita amesema kuporomoka kwa bei ya dengu kunawaumiza wakulima huku wakiomba msaada wa Serikali.
“Wananchi wanaomba kujengewa barabara ya urefu wa kilomita 260 kuwekewa lami kutoka Itigi hadi Makongorosi ambayo tayari Serikali imeanza kuweka jitihada ya kuwekewa lami kilomita 25,” amesema.
Aidha, wananchi wa Itigi wamelia na wanyama wasumbufu kuharibu mazao huku wakiomba tembo hao wadhibitiwe.
Akijibu hoja hizo, Dk Mwigulu amewaambia wakazi wa Itigi kitendo cha kubadilisha badilisha wabunge kinakwamisha maendeleo ya ujenzi wa miradi kama barabara ya kwenda Mbeya.
“Barabara ya kwenda Mbeya inawezekana wananchi hamjajua siri kwa nini inachelewa namna hii. Mnabadili wabunge kila leo mnaleta mpya sasa mkishaleta mpya sio kila mmoja anajua kila ofisi,” amesisitiza.
Katika hatua nyingine, kiongozi huyo ameendelea kusikitishwa na tabia ya wagonjwa kuambiwa wakanunue dawa kwenye maduka ya mtaani akihoji maduka hayo yanatoa wapi dawa hizo.
Amesema dawa lazima zinunuliwe mahususi katika eneo husika huku zikifuatiliwa minyororo wake kuanzia zinaponunuliwa hadi kufika hospitalini.
Dk Mwigulu amekuwa akisisitiza kukomeshwa kwa tabia hiyo kupitia vyombo na mamlaka za Serikali pamoja na suala zima la migogoro ya ardhi.
“Ardhi kila ninakopita ni changamoto wakati maeneo mengine ni makusudi tu. Katika karne hii tumeshatoka kwenye kutunza mafaili kwa njia ya makaratasi unatoaje hati kwa watu wanne? Hili jambo la ardhi litatugombanisha sisi kama ndugu,” amesema huku akisisitiza mipango bora ya matumizi ya ardhi.
Amefichua kwamba serikalini tayari utaratibu unaendelea wa kuangalia namna bora ya kushughulikia suala hilo kabla halijagawa wananchi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego amesema wanaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kulingana na fedha zinazopelekwa.