YANGA inaendelea na maandalizi ya kuimarisha kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao, huku straika wa raia wa Kenya, Moses Shumah, akitajwa kuwa miongoni mwa wachezaji wanaofuatiliwa kwa karibu.
Shumah, anayekipiga katika klabu ya Power Dynamos ya Zambia ameonyesha kiwango bora msimu huu baada ya kufunga mabao 20 kwenye Ligi Kuu Zambia.
Straika huyo mwenye umri wa miaka 23, amevutia macho ya viongozi wa Yanga ambao tayari wameanza kufanya mazungumzo ya awali huku wakifuatilia kwa kina uwezo wake wa kuhimili presha ya kucheza katika klabu kubwa.
Mabao hayo 20 yamemwezesha kuvunja rekodi ya Mkenya mwenzake, Jesse Were, aliyewahi kufunga mabao 18 akiwa Zesco United.
Pia amelingana rekodi ya mshambuliaji wa DR Congo, Idriss Mbombo, aliyefunga mabao 20 mwaka 2018 wakati akiichezea Nkana.
“Tumeshafanya mazungumzo naye na tumeridhishwa na uwezo wake wa kufunga. Tunachokiangalia kwa sasa ni uwezo wake wa kuhimili presha ya kucheza katika klabu kubwa kama Yanga,” amesema mmoja wa viongozi wa klabu hiyo.
“Kama tutajiridhisha, tutafanya hatua zinazofuata. Bado ana mkataba, lakini tunaamini tunaweza kufikia makubaliano kwa sababu anatamani kucheza Yanga.”
Yanga kwa sasa ipo kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara ikiwa kileleni kwenye msimamo na pointi 60 zikiwa ni mbili mbele ya Simba iliyopo katika nafasi ya pili zikiwa zimebaki mechi tano msimu wa 2025/26 umalizike.