
Dar es Salaam. Wakati Rais Samia Suluhu Hassan akianza ziara ya siku tatu nchini Russia kesho kuanzia Juni 3 hadi 5, 2026, wafanyabiashara na wazalishaji wa Tanzania wametakiwa kuelekeza macho yao katika fursa mpya za biashara zinazopatikana katika soko la Taifa hilo, hususan kwa bidhaa za kilimo na mifugo.
Taarifa ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) inaonesha kahawa, parachichi, mbegu za kakao, karafuu, maua, nyama na matunda ni miongoni mwa bidhaa za Tanzania zenye uwezo mkubwa wa kuongeza mauzo katika soko la Russia katika miaka ijayo.
Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, kati ya mwaka 2026 na 2030, fursa ya biashara ya kahawa Russia inatarajiwa kufikia thamani ya Dola 3.8 milioni za Marekani (Sh9.9 bilioni), huku parachichi likikadiriwa kuwa na fursa ya Dola 1.8 milioni (Sh4.5 bilioni).
Kwa jumla, Tanzania ina nafasi ya kuongeza mauzo ya bidhaa zake Russia yenye thamani ya Dola 14 milioni (Sh37 bilioni) katika kipindi hicho.
Fursa hizo zinakuja wakati Tanzania ikiendelea kuongeza uzalishaji wa mifugo na bidhaa zake. Takwimu za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zinaonesha uzalishaji wa nyama za aina mbalimbali umeendelea kuongezeka, hali inayoweza kusaidia nchi kunufaika zaidi na mahitaji yanayoongezeka katika soko la Russia.
Hata hivyo, pamoja na uwepo wa fursa hizo, kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Russia bado hakijaakisi uwezo halisi uliopo.
Takwimu za TanTrade zinaonesha kuwa, kati ya mwaka 2021 na 2025, Tanzania iliuza bidhaa Russia zenye thamani ya Dola 29 milioni, huku ikiagiza bidhaa kutoka Taifa hilo zenye thamani ya Dola 253 milioni (Sh75 bilioni).
Pengo hilo linaashiria umuhimu wa kuongeza uzalishaji wenye tija, kuboresha ubora wa bidhaa na kuimarisha mikakati ya kutafuta masoko ya nje.
Mchambuzi wa masuala ya siasa na maendeleo, Magabilo Masambu amesema ziara ya Rais Samia ni hatua muhimu katika kuendeleza diplomasia ya uchumi, inayolenga kutumia uhusiano wa kimataifa kukuza biashara, uwekezaji na maendeleo ya kiuchumi.
Amesema pamoja na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Russia, ziara hiyo inafungua fursa za kutafuta masoko mapya ya bidhaa za Tanzania, kuvutia uwekezaji na kuimarisha ushirikiano katika teknolojia na maarifa.
Mchambuzi wa diplomasia na siasa za kimataifa, Amani Gonde amesema ziara hiyo ni muhimu kwa kuimarisha nafasi ya Tanzania katika uhusiano wa kimataifa na kuendelea kujenga ushirikiano wa muda mrefu na Russia.
Mchambuzi wa masuala ya kijamii, Noel Shao amesema ziara hiyo inaonesha dhamira ya Tanzania ya kupanua ushirikiano wake na mataifa mbalimbali kwa kuzingatia masilahi ya kiuchumi, uwekezaji, teknolojia na upatikanaji wa masoko.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, ziara hiyo ni ya pili kufanywa na Rais wa Tanzania nchini Russia tangu ziara ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, mwaka 1969.
Akiwa nchini humo, Rais Samia atafanya mazungumzo rasmi na Rais wa Russia, Vladimir Putin, pamoja na kushiriki katika Jukwaa la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg (SPIEF), linalowakutanisha viongozi wa Serikali, wafanyabiashara, wawekezaji na taasisi za fedha kutoka sehemu mbalimbali duniani.