Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi, Mkuu wa usafirishaji na logistiki wa UNICEF, Jean-Cedric Meeus, amesema kila dola ya ziada inayotumika kusafirisha mizigo ni dola inayopungua kwa ajili ya kununua vifaa vinavyookoa maisha ya watoto.

“Kilichoanza kama usumbufu wa njia za usafirishaji kinaweza kugeuka kuwa janga la kibinadamu,” amesema Meeus, akiongeza kuwa UNICEF inalazimika kufanya maamuzi magumu kuhusu ni watoto gani wapate msaada kwanza.

UNICEF imesema gharama za kusafirisha chanjo kutoka India kwenda Ethiopia, Nigeria na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC zimeongezeka kwa asilimia 50 hadi 70. Aidha, gharama za kusafirisha chakula tiba kutoka Kenya kwenda Somalia, Sudan Kusini na DRC zimepanda kwa asilimia 30.

Shirika hilo pia limeeleza kuwa bandari kadhaa za Afrika, ikiwemo Dar es Salaam, Mombasa, Beira, Conakry na Abidjan, zinakabiliwa na ucheleweshaji mkubwa wa mizigo, hali inayowaathiri zaidi watoto katika nchi zinazotegemea njia hizo za usafirishaji.

Kwa mujibu wa UNICEF, usumbufu huo unaweza kuchelewesha utoaji wa vifaa muhimu kwa kipindi cha miezi minne hadi sita. “Kwa mtoto aliye katika mazingira ya dharura, kuchelewa kwa chanjo au huduma za lishe kunaweza kuwa tofauti kati ya maisha na kifo,” amesema Meeus.

Licha ya changamoto hizo, UNICEF imesisitiza kuwa itaendelea kutafuta njia mbadala za usafirishaji ili kuhakikisha misaada muhimu inawafikia watoto wanaohitaji zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *