Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amezihimiza jumuiya za kimataifa kutoa usaidizi unaohitajika ili kudhibiti mlipuko. Pia amelihimiza nchi “kutoweka vikwazo vya usafiri kwa DRC, ili kuhakikisha msaada wa kiafya na kibinadamu unaweza kufikia kiwango kinachohitajika.”  

Ebola inaweza kutibika ikiwa wagonjwa watapata huduma za afya mapema – Profesa Janabi

Naye Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika, Profesa Mohamed Janabi, amesema ametiwa moyo na kazi inayofanywa na wahudumu wa afya walioko mstari wa mbele katika jimbo la Ituri. Akiwa Bunia, DRC, Profesa Janabi amesema “WHO na washirika wake wanafanya kazi kwa karibu chini ya uongozi wa serikali ya DRC ili kuokoa maisha na kumaliza mlipuko huo wa Ebola.”

Ameongeza kuwa “kupona na kuruhusiwa kwa wagonjwa watano wa Ebola, ambao wote ni wahudumu wa afya kutoka DRC waliopata maambukizi wakati wakihudumia jamii zao, ni ishara ya matumaini.” 

Juhudi za WFP kupambana na Ebola 

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP linaongeza kasi ya mapambano dhidi ya mlipuko wa ugonjwa wa Ebola huko Mashariki mwa DRC, kwa kusafirisha wahudumu wa afya, vifaa vya matibabu na misaada muhimu katika maeneo yaliyoathirika. Shirika hilo pia linaendelea kutoa msaada wa chakula na lishe kwa mamia ya maelfu ya watu walio hatarini, likiwemo kundi la wagonjwa wa Ebola na familia zao. 

Kwa mujibu wa Mkuu wa Ofisi ya WFP katika jimbo la Ituri, Olivier Nkakudulu, “kipaumbele chetu ni kuokoa maisha katika nyanja zote.” Amesema ukosefu wa chakula ulianza kabla ya Ebola, lakini ugonjwa huo unazidisha hali hiyo kwani watu wanaowekwa karantini wanahitaji msaada wa chakula ili kuzuia kusambaa kwa maambukizi. 

WFP inaonya kuwa mlipuko huu unatishia kuzidisha moja ya migogoro mikubwa zaidi ya njaa duniani, huku watu milioni 26.5 nchini DRC wakikabiliwa na uhaba wa chakula. Katika jimbo la Ituri pekee, zaidi ya theluthi moja ya wakazi wanakabiliwa na njaa kali, huku zaidi ya watu 500,000 wakiwa katika hali ya dharura ya ukosefu wa chakula. 

Ili kuimarisha mwitikio wake, WFP inahitaji dola milioni 26 katika kipindi cha miezi mitatu ijayo kwa ajili ya kuongeza huduma za usafirishaji na msaada wa chakula kwa zaidi ya watu 146,000 walioathiriwa na mlipuko wa Ebola katika jimbo la Ituri.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *