Dkt. Rahman alikuwa akiwania nafasi hiyo na Balozi wa Cyprus katika Umoja wa Mataifa, Andreas S. Kakouris, katika uchaguzi uliofanyika mapema hii leo kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani.

Kaulimbiu ya urais wake ni “Kurejesha Imani, Kusimamia Mabadiliko: Umoja wa Mataifa unaowaletea Matokeo Watu Wote,” akiahidi kuimarisha mfumo wa ushirikiano wa kimataifa katika kipindi ambacho dunia inakabiliwa na migogoro, mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la pengo la usawa na changamoto za maendeleo.

Baada ya kuchaguliwa, Dkt. Rahman atachukua nafasi ya Rais wa sasa wa Baraza Kuu, Annalena Baerbock wa Ujerumani, na kuongoza shughuli za chombo hicho kikuu cha kutunga sera za Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Miongoni mwa majukumu yake makuu yatakuwa kuongoza mjadala mkuu wa viongozi wa dunia wakati wa wiki ya ngazi ya juu ya Baraza Kuu mwezi Septemba, pamoja na kusimamia kazi za kamati sita za Baraza Kuu, ikiwemo Kamati ya Tano inayoshughulikia bajeti ya kawaida ya Umoja wa Mataifa.

Picha ya UN/Eskinder Debebe Katibu Mkuu António Guterres (kushoto) na Rais wa Baraza Kuu Annalena Baerbock (kulia), pamoja na Khalilur Rahman, Rais mteule wa kikao cha 81 cha Baraza Kuu.

Pongezi kutoka kwa Mkuu wa UN

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amempongeza Dkt. Rahman kwa ushindi wake na kusema uzoefu wake mkubwa wa kisiasa na kidiplomasia ni dhamana ya mafanikio kwa Baraza Kuu na Umoja wa Mataifa kwa ujumla.

Guterres amesema Dkt. Rahman anachukua nafasi hiyo katika kipindi kigumu cha mahusiano ya kimataifa, akibainisha kuwa dunia inakabiliwa na migogoro, mgawanyiko, ongezeko la ukosefu wa usawa na changamoto za tabianchi, huku maendeleo kuelekea Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) yakisuasua.

“Tunahitaji diplomasia, mazungumzo na ushirikiano zaidi ili kurejesha imani katika mfumo wa kimataifa,” amesema Katibu Mkuu, akiahidi kumpa Rais mteule ushirikiano wake kamili katika kutekeleza majukumu yake.

Kikao cha 81 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kinatarajiwa kuanza rasmi Septemba 8, kabla ya mjadala mkuu wa viongozi wa dunia utakaofanyika baadaye mwezi huo.

Picha ya UN/Eskinder Debebe Picha pana ya Jumba la Baraza Kuu wakati Khalilur Rahman (kwenye skrini), Rais mpya aliyechaguliwa wa kikao cha 81 cha Baraza hilo akizungumza katika kikao cha jumla cha 85 Baraza Kuu.

Mchakato wa kumpata Rais wa Baraza Kuu 

Kwa mujibu wa utaratibu wa Umoja wa Mataifa, urais wa Baraza Kuu huzunguka kati ya makundi ya kikanda, na kikao cha 81 kilikuwa zamu ya kundi la nchi za Asia.

Mfumo huo wa mzunguko unalenga kuhakikisha uwakilishi wa usawa wa kijiografia katika uongozi wa chombo hicho chenye wanachama wote 193 wa Umoja wa Mataifa. 

Makundi hayo ni Afrika, Asia-Pasifiki, Ulaya Mashariki, Amerika ya Kusini na Karibiani, pamoja na Ulaya Magharibi na nchi nyingine.

Kwa kawaida, nchi za kundi husika hukubaliana juu ya mgombea mmoja. Hata hivyo, mwaka huu nchi za Asia ziliwasilisha wagombea wawili, Dkt. Khalilur Rahman wa Bangladesh na Balozi Andreas S. Kakouris wa Cyprus, hali iliyosababisha kufanyika kwa uchaguzi rasmi wa kura za siri katika Baraza Kuu.

Rais wa Baraza Kuu huchaguliwa kwa kipindi cha mwaka mmoja na jukumu lake ni kuongoza vikao vya Baraza Kuu, kusimamia mjadala mkuu wa viongozi wa dunia na kusaidia kujenga mwafaka kati ya mataifa wanachama kuhusu masuala muhimu ya kimataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *