
Miongoni mwa yale yanayofanywa na jamii ni pamoja na kushirikiana na wadau mbalimbali kuokota taka zikiwemo karatasi na makopo ya plastiki ambayo hutupwa na watu baada ya kununua bidhaa madukani na kuyatupa kutoka nchi kavu kwenda ziwani.
Juhudi hizi ni namna moja wapo ya utekelezaji wa yale yaliyokusudiwa wakati wa kutengwa kwa Siku ya Mazingira Duniani ambayo mwaka huu inasema “Sasa kwa ajili ya Tabianchi” (Now For Climate).
Maadhimisho ya kimataifa yasiku hii yanafanyika jijini Baku nchini Azerbaijan, yam waka huu yameweka msisitizo mkubwa kuhusu uhifadhi wa mifumo ya ikolojia na hatua za haraka za tabianchi, hususan kuchukua hatua dhidi ya ishara ambazo dunia inatuma kwa wanadamu kuhusu uharibifu wa mazingira.
Maadhimisho haya yanakuja kipindi kifupi baada ya Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria na serikali za nchi zote zinazozunguka ziwa hilo pamoja na wadau, kuzindua kwa hatua ya awali Ripoti ya Hali ya Ziwa Victoria kuelekea maadhimisho ya kwanza ya ziwa hilo yaliyofanyika jijini Mwanza tarehe 21 Mei mwaka huu. Ripoti hiyo imeonesha kuwepo kwa kiwango kikubwa cha uchafuzi wa maji katika maeneo mbalimbali ya ziwa na fukwe zake, ikiwemo uwepo wa kemikali hatarishi kama zebaki, taka ngumu, plastiki, pamoja na maji taka yanayotiririka kutoka kwenye makazi ya watu na viwandani.
Usimamizi wa fukwe na changamoto ya upatikanaji wa samaki
Kuhusu hali halisi ya upatikanaji wa samaki ziwani, baharia wa Kikundi cha Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) katika mwalo wa Luchelele, Funga Gavana, amebainisha kuwa kupungua kwa samaki kwa sasa kunatokana na ongezeko kubwa la watu wanaojihusisha na uvuvi kulinganisha na zamani, huku akielezea mikakati ya usafi na usimamizi wa mwalo huo.
“Kuhusu wananchi kutupa taka ziwani hilo tumekwisha toa angalizo, pia watu wasiwe wanaogelea ziwani, waoge nyumbani na sasa hivi usafi unafanyika kwa kila siku ambapo kuna mtu ambaye tumemteua kwa ajili ya kuwa anasafisha mwalo.”
Wananchi waongoza mabadiliko ya uhifadhi wa mazingira
Kwa upande wao, wakazi wa eneo hilo wameeleza namna walivyobadili mifumo yao ya maisha baada ya kupata miongozo kutoka kwa viongozi wao ili kuzuia uharibifu wa chanzo hicho cha maji. Mkazi wa kata hiyo, Veronica Lufunga, amebainisha mabadiliko hayo akisema,“Kutupa uchafu hatutupi ziwani, na kuoga hatuogei pale ziwani, tunachota maji tunakuja kuogea nyumbani. Kufua, tunachota maji tunakuja kufulia nyumbani.”
Veronica ameeleza kuwa jamii imepokea kwa furaha na kujifunza kutoka kwenye miongozo hiyo ya serikali, huku akiwaasa wakazi wengine kulinda ziwa liwe safi kwa sababu wakati mwingine huchafuka hadi kukosekana kwa sehemu salama ya kuchota maji.
Naye Jesca Paul, mkazi mwingine wa Luchelele aliyekuwa akiteka maji, amesisitiza umuhimu wa kila mwanajamii kuwa imara katika kufanya usafi wa ziwa ili kulinda viumbe hai na kupata maji yaliyo safi na salama kwa matumizi ya nyumbani.
“Hapa cha msingi ni kuwa imara tu katika kufanya usafi katika ziwa letu, ili tuendelee kuwa na mazingira safi, tupate maji yaliyo safi na salama, nawasihi tu wanajamii wenzangu, tuendelee kufanya usafi katika maji yetu ili tupate maji salama,” ameeleza Jesca Paul.
Jesca ameongeza kuhusu hatua binafsi anazochukua anapokutana na taka ziwani kama vile chupa za plastiki,“Kwa kweli nitajisikia vibaya, hatua nitakayochukua ni kuanza kufanya usafi ili nipate maji safi.”