
Mradi husika uko chini ya Mradi wa Pamoja wa Zanzibar au ZJP unaotekelezwa kuanzia 2025 hadi 2027 kwa ubia baina ya serikali ya Zanzibar na shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira UNEP kwa ufadhili wa Norway.
Ukiunga mkono maudhui ya siku ya baharí mwaka huu ambayo ni Tafakari upya: Zaidi ya ulimwengu tunaoufahamu, kuelekea uhusiano mpya na bahari yetu, mradi unahusisha upandaji wa mikoko na ufugaji bora wa nyuki ambapo mizinga ya nyuki inafungwa kwenye mikoko ili kuepusha ukataji holela wa miti hiyo kwa ajili ya shughuli mbali mbali ikiwemo kuni.
Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania Susan Ngongi Namondo akizungumzia mradi huo unaolenga kupatia mafunzo wanajamii 70 wakiwemo wanawake na vijana anasema,
“Kwa mtazamo wangu, programu hii ni muhimu sana kwa sababu sote tunafahamu kwamba mabadiliko ya tabianchi yanatuathiri vibaya. Hata hivyo, ili jamii zijitolee kikamilifu na kushiriki katika kukabiliana na changamoto hizi, zinahitaji pia kupata manufaa ya kiuchumi. Hapa Bumbwini, eneo hili lina umuhimu mkubwa kwa mikoko. Kwa uelewa wangu, mikoko ilikuwa imeharibika kutokana na baadhi ya wanajamii kuvuna miti kwa ajili ya kutengeneza mkaa na matumizi mengine. Lakini kupitia mradi huu, wamepata njia mbadala ya kujipatia kipato, ambayo ni ufugaji wa nyuki. Sasa wanaanza kuzalisha asali, jambo ambalo linawapa motisha zaidi ya kutoharibu mikoko.”
Akaendelea zaidi akisema, “Lakini nina matumaini kwamba serikali itaongeza juhudi zaidi za kuunga mkono jamii kama hizi ili kuhakikisha kwamba asali yao inapatikana kwenye meza za kifungua kinywa katika hoteli zote za Zanzibar.”
Kwa kuunganisha uhifadhi wa mikoko na shughuli za ufugaji nyuki zinazozalisha kipato, mpango huu umeimarisha usimamizi wa rasilimali za asili unaofanywa na jamii huku ukifungua fursa mpya za kiuchumi kwa wananchi. Maryam Abdallah ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar.
“Wenzetu wa UNEP wametusaidia programu ambapo tunawashajihisha vijiji vyetu tumeanzia kwa mfano katika Bumbwini ambapo wao wamepewa elimu, lakini wamepewa na nyenzo katika kuzalisha asali, ufugaji wa nyuki na kuzalisha asali. Kwa kweli hiyo ni ajira tosha kwa upande wao pamoja na jamii, lakini sio ajira ya wao itainua kipato chao, lakini vile vile itainua uchumi wa nchi.”
UNEP inasema mradi huu unaonesha jinsi ushirikiano katika kulinda mikoko unavyochangia kuwa na bahari yenye afya zaidi, jamii za pwani zilizo imara zaidi, na uwezo mkubwa wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa vizazi vya sasa na vijavyo. Clara Makenya Mwakilishi wa UNEP nchini Tanzania anafafanua jukumu lao.
“Kazi yetu kubwa ambayo tumeifanya kwa kweli ni kuleta kwa pamoja hao wadau ili kuweza kuwezesha si tu utunzaji wa mazingira lakini pia kuwezesha kipato cha wanajamii. Na hiyo ndio kazi kubwa ambayo tunaiangalia kwamba mwisho wa siku ile kwa ajili ya kutunza mazingira, inabidi wadau wa aina tofauti tofauti waweze kuja. pamoja na kufanya hayo yote.”