
Video ya UNFCCC inaanza na taswira kutoka jimbo la Masvingo nchini Zimbabwe Iikionesha ardhi iliyokauka na kupasuka kutokana na ukame mkali, moja ya athari mbayá za mabadiliko ya tabianchi.
Katibu Mtendaji wa UNFCCC Simon Stiell akizungumza akiwa mjini Bonn, Ujerumani, anasema madhara hayo hayajasalia tu kwenye ardhi bali yamebisha hodi kwenye viwanja vya mpira wa miguu ujulikanao pia kama soka
Anasema kuelekea fainali za Kombe la Dunia la FIFA 2026, matukio ya kusimamishwa kwa mechi kutokana na joto kali yanazidi kushuhudiwa akitaja chanzo ni pamoja na nishati kisukuku kama vile petroli, makaa ya mawe ambayo upatikanaji wake ni lazima kuchimba ardhi kitendo kinachotoa hewa chafuzi kwa mazingira.
“Sote tunatazama mchezo, lakini unasimamishwa kwa sababu kuna joto kali mno. Ni joto kwa wachezaji, kwa mashabiki, kwa kila mtu. Joto linaongezeka na linaendelea kuongezeka. Hii si bahati mbaya. Haya ni matokeo ya mabadiliko ya tabianchi. Sayari yetu inaendelea kupata joto baada ya zaidi ya karne moja ya matumizi ya nishati kisukuku kama makaa ya mawe, petroli na gesi. Nishati hii inabakisa joto angani, na sasa tunahisi madhara yake kila mahali.”
Kauli hiyo inaungwa mkono na video kutoka maeneo mbalimbali duniani zinazoonesha athari za mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo ukame mkali nchini Zimbabwe, mioto ya misitu huko Nepal na katika msitu wa Amazon nchini Brazil.
“Viwanjani, kuanzia ngazi za juu za soka la kimataifa hadi kwenye viwanja vya kijamii, joto kali linaongeza uchovu, linafanya maamuzi kuwa magumu na linaweka wachezaji na mashabiki katika hatari zaidi.”
Anasema madhara hayo hayaishii kwenye michezo pekee bali pia yanagusa sekta muhimu kama kilimo na uhakika wa kupata chakula.
Kutoka Guatemala video zinaonesha mashamba ya mahindi yanayokabiliwa na changamoto za hali ya hewa, jambo ambalo kwa mujibu wa UNFCCC linaweza kupunguza mavuno na kuongeza bei za vyakula duniani.
“Mabadiliko ya tabianchi yanayoendeshwa na matumizi ya nishati kisukuku yanaongeza gharama za maisha kwa mabilioni ya watu katika kila nchi.”
Katika miji mbalimbali duniani, ikiwemo Bishkek nchini Kyrgyzstan na maeneo ya viwanda nchini India, uchafuzi wa hewa unaendelea kuwa changamoto kubwa inayohusishwa na matumizi ya nishati ya mafuta ya kisukuku. Hata hivyo, Stiell anasema kuna suluhisho.
“Habari njema ni kwamba tunajua jinsi ya kukabiliana na janga la tabianchi. Tunapaswa kuachana na utegemezi wa nishati kisukuku na kuharakisha matumizi ya nishati safi.”
Picha kutoka Syria na Cambodia zinaonesha wahandisi wakifunga paneli za sola na mifumo ya umwagiliaji inayotumia nishati jadidifu, hatua ambazo UNFCCC inazitaja kuwa sehemu ya majawabu ya kupunguza uzalishaji wa hewa chafuzi.
Stiell anasema sekta ya michezo nayo inaanza kuchukua hatua kwa kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuhamasisha matumizi ya nishati safi.
“Michezo ndiyo nguvu kubwa zaidi inayowaunganisha watu duniani, na soka ndiyo mchezo mkubwa zaidi duniani. Wapenzi wa soka wakizungumza kwa sauti moja kulinda mchezo huu dhidi ya madhara ya mabadiliko ya tabianchi kama joto kali, inaweza kuleta mabadiliko makubwa. Hili si suala la kuokoa michezo pekee, bali ni kulinda dunia ambayo michezo na sisi sote tunategemea.”
Amehitimisha kwa kuwataka watu kukumbuka kuwa kila mara wanapoona mapumziko ya mchezo au mechi ikicheleweshwa kutokana na joto kali, hiyo ni ishara ya madhara ya mabadiliko ya tabianchi, na kwamba mustakabali wa michezo na dunia kwa ujumla unategemea maamuzi yanayofanywa sasa kuhusu matumizi ya nishati na mazingira.