
Kinda wa Azam FC, Feisal Othman amejiunga na United FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Falme za Kiarabu (UAE) inayonolewa na kiungo wa zamani wa Juventus na Italia, Andrea Pirlo.
Mchezaji huyo anayecheza nafasi ya kiungo, amesajiliwa na klabu hiyo baada ya kufanya vizuri katika majaribio aliyofanya klabuni hapo kwa muda wa miezi miwili.
Chanzo cha karibu na mchezaji huyo kimelithibitishia gazeti hili kuwa kiungo huyo ataitumikia United FC msimu ujao.
“Feisal ameshamalizana na United FC lakini kwa sasa vipengele vya kimkataba ni siri kwa vile bado klabu yake ya Azam haijatoa taarifa rasmi,” kimefichua chanzo hicho.
Ofisa Mtendaji Mkuu Msaidizi wa Azam FC, Rashid Seif, amesema kuwa bado mchezaji huyo ni mali yao kwa vile hakuna mazungumzo yoyote yaliyofanyika na klabu inayotajwa kumnyakua.
“Ni kweli Feisal Othman alikuwa anafanya majaribio na hiyo klabu na sisi kama waajiri wake tunasubiria ripoti ya hayo majaribio.
“Kuhusu kusaini sio kweli maana hadi sasa sisi kama Azam FC hatuna taarifa yoyote na tunamngojea mchezaji arudi,” alisema Rashid Seif.
Feisal mwenye umri wa miaka 16, ni zao la kikosi cha vijana cha Azam FC na msimu huu alipandishwa katika kikosi cha wakubwa na Kocha Mkuu wa Azam, Florent Ibenge.
Anamudu vyema kucheza nafasi ya kiungo mkabaji na kiungo wa kushambulia.