KAMA kuna jina jipya limezua mjadala mkubwa ndani ya Simba katika dirisha hili la usajili, basi ni lile la winga Ramadhan Salum ‘Chobwedo’ ambaye tayari ameshapewa mkataba wa miaka miwili akisubiri kutambulishwa rasmi.

Ikumbukwe kuwa, Yanga ilikuwa ya kwanza kuonyesha nia na kufanya mazungumzo na wasimamizi wa Chobwedo. Hata hivyo, kulikuwa na mvutano wa kiufundi ndani ya bodi ya Yanga ambapo baadhi ya viongozi walitaka afuatiliwe zaidi, jambo lililosababisha uamuzi kuchelewa.

Tangu atue TRA akitokea Mtibwa Sugar, amecheza mechi 18 kati 25 ambazo timu hiyo imecheza, huku akifikisha jumla ya dakika 1706, huku akifunga mabao 03.

SIMBA ILIINGILIA DILI

Baada ya kuondoka kwa Kibu Dennis kwenda Al-Nasr ya Libya mwezi Januari, Simba ilikuwa na uhitaji winga mzawa anayeweza kucheza kikosi cha kwanza. Walivamia dili hilo kwa kasi, wakaongeza dau, na kufanikiwa kusainisha mkataba wa awali ‘pre-contract’ tangu mwezi Mei.

Taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti kwamba nyota huyo ameshakubaliana kila kitu na Simba na tayari amesaini mkataba wa kuitumikia klabu hiyo kwa misimu miwili ijayo, lakini hadi sasa bado hajapokea fedha za usajili jambo linaloonyesha mchakato wake bado haujakamilika kwa asilimia 100. Hata hivyo, wakati mashabiki wakisubiri kuona hatma yake, ndani ya Simba yenyewe kumekuwa na mitazamo tofauti kuhusu uwezo wa winga huyo na kama kweli anastahili kuvaa jezi ya Msimbazi.

Chanzo cha ndani ya Simba kilieleza kuwa baadhi ya viongozi na watu wenye ushawishi kwenye masuala ya usajili wanaamini Chobwedo ni mchezaji wa kiwango cha kawaida ambaye bado hajafikia hadhi ya kuja kuwa tegemeo la Simba katika mashindano makubwa ya ndani na kimataifa.

Kundi hilo linaelezwa kuwa linaamini Simba inapaswa kutafuta winga mwenye uzoefu mkubwa zaidi na ambaye atakuja moja kwa moja kuongeza ushindani kwenye kikosi hicho badala ya kusubiri muda wa kumkuza.

Lakini upande mwingine wa mabosi hao una mtazamo tofauti kabisa. Wao wanaamini Chobwedo ana kipaji na anaweza kubadilika haraka akipata mazingira bora, benchi la ufundi lenye ubora na ushindani mkubwa wa ndani ya kikosi.

Wanaounga mkono usajili wake wanatolea mfano baadhi ya wachezaji ambao walipowasili Simba au Yanga walionekana wa kawaida, lakini baadaye wakawa nyota wakubwa kutokana na mfumo mzuri wa timu hizo.

Mjadala huo unakuja wakati Simba ikiendelea kujenga kikosi hicho kufuatia mabadiliko mbalimbali yanayotarajiwa kutokea kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa mashindano.

Katika siku za karibuni, Simba imekuwa ikihusishwa na majina kadhaa ya mabeki wa ndani na nje ya Tanzania miongoni mwao ni  Edmund John (Singida Black Stars),Abdulkarim Watambala (Vipers SC, Uganda),Iddi Nado (Azam FC).

Unaweza kusema kwamba, Simba bado iko kwenye chekecheo la kuchuja ni yupi mchezaji mkali atakaewafaa kwa pande zote mzawa na wakigeni ili kuongeza vyuma vitakavyowapa ushindi kwenye michuano ya msimu ujao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *