
Katika utafiti uliochapishwa mnamo Juni 11, muungano wa watafiti unabainisha kwamba lengo kuu zaidi la Mkataba wa Tabianchi wa Paris huenda likavukwa ndani ya miaka minne ijayo.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Wakati wimbi jipya la joto likijiandaa kuikumba Ulaya, muungano wa kimataifa wa wanasayansi 73 wanaoongoza katika masuala ya hali ya hewa umechapisha taarifa mpya kuhusu takwimu muhimu kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa na athari za shughuli za binadamu katika jarida la kisayansi la Earth System Science Data siku ya Alhamisi, Juni 11. Kulingana nao, ongezeko la joto duniani litafikia 1.5°C juu ya viwango vya kabla ya viwanda ifikapo mwaka wa 2030, katika kipindi cha miaka minne tu. Hiki ni kizingiti kilichowekwa na mataifa katika Mkataba wa Paris kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa, uliosainiwa mwaka wa 2015.
Sababu: uzalishaji wetu wa gesi chafu unafikia viwango vya rekodi. Gesi hizi hujikusanya angani na kunasa kiwango kinachoongezeka cha joto Duniani. Matokeo yake, mwaka jana halijoto ya dunia iliongezeka kwa zaidi ya 1.39°C ikilinganishwa na karne iliyopita. “Kiwango cha ongezeko hili la joto linalosababishwa na shughuli za binadamu kwa sasa ni nyuzi joto 0.27 kwa kila muongo mmoja.” “Hii ni kasi isiyo ya kawaida,” anaonya Aurélien Ribes, mtafiti katika mamlaka ya utabiri nchini Ufaransa, Météo France. “Tukifikiria mwenendo wa sasa, tunafikia takriban 1.5°C karibu 2030.”
“Kwa hivyo hakuna muda mwingi uliobaki,” anaongeza Pierre Friedlingstein wa CNRS. “Bajeti ya kaboni iliyobaki ni karibu tani bilioni 130 za CO2. Hicho ndicho kiasi cha uzalishaji tunachoweza kutoa katika siku zijazo ili kubaki sambamba na kikomo cha ongezeko la joto cha 1.5°C. Ni sawa na miaka mitatu ya uzalishaji wa CO2 kwa kiwango cha sasa.”
Robo tatu ya uzalishaji huu unatokana moja kwa moja na matumizi yetu ya mafuta ya visukuku: mafuta, gesi, na makaa ya mawe. Kwa hivyo watafiti wanatoa wito wa kuimarishwa kwa juhudi za kuziondoa katika muongo huu muhimu ili kupunguza ongezeko la joto duniani.