
Leo ni Alkhamisi 25 Mfunguo Tatu Dhulhija 1447 Hijria mwafaka na 11 Juni 2026.
Tarehe 25 Dhulhija inasadifiana na siku ya kuteremshwa Suratu Dahr ambayo inawahusu Imam Ali bin Abi Twalib, mkewe Bibi Fatimatu Zahra na watoto wao Hassan na Hussein (as).
Baada ya watukufu hao kuweka nadhiri ya kufunga swaumu siku tatu kwa ajili ya kukidhiwa haja zao na kuanza kutekeleza nadhiri hiyo, katika siku zote tatu za swaumu masikini, yatima na fakiri walikwenda nyumbani kwa Imam Ali (as) na kuomba chakula. Watukufu hao walitoa chakula chao kilichokuwa kimeandaliwa kwa ajili ya futari na kuwapa wahitaji hao kwa ajili ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu.
Hali hiyo iliendelea kwa siku tatu za kutimiza nadhiri ya swaumu na wakati huo ndipo iliporetemshwa Suratu Dahr ikipongeza na kubakisha hai tukio hilo. ***
Katika siku kama ya leo miaka 454 iliyopita sawa na tarehe 11 Juni mwaka 1572, alizaliwa Benjamin Jonson (Ben Johnson) mshairi na mwandishi wa filamu wa Uingereza.
Jonson kwa muda mrefu alikuwa mcheza tamthilia na rafiki wa Shakespare mwandishi maarufu wa Uingereza, ambapo urafiki wao ulikuwa na athari kubwa katika kukamilisha fasihi ya mshairi huyo.
Baadhi ya athari zilizoachwa na Benjamin Jonson ni Mwanamke Aliyezimwa’ pamoja na Historia ya Dunia. Malenga huyo Muingereza alifariki dunia mwaka 1637. ***
Siku kama ya leo miaka 171 iliyopita inayosadifiana na tarehe 11 Juni mwaka 1855, mwanga wa jua ulitambuliwa kwa kutumiwa njia za taaluma ya uchanganuzi na wigo wa rangi.
Jaribio hilo lilifanywa kwa mara ya kwanza katika historia ya utafiti mpya wa fizikia na wanasayansi wawili wa Ujerumani walioitwa Kirchhoff na Bunsen.
Si vibaya kuashiria hapa kwamba, mionzi ya jua katika hewa wakati wa mvua pamoja na kutokea upinde wa mvua wenye rangi mbalimbali, ni tukio la kuvutia ambalo linasababishwa na kuchanganuliwa nuru ya jua na matone ya maji mawinguni. Hata hivyo suala hilo mwanzoni lilifafanuliwa na wanasayansi wa Kiislamu kama vile Ibn Sina, Ibn Haitham na Qutbuddin Shirazi na baadaye kuthibitishwa na Kirchhoff na Bunsen. ****
Miaka 52 iliyopita katika siku kama ya leo sawa na tarehe 21 Khordad mwaka 1353 kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, alifariki dunia Daktari Muhammad Khazaeli, mwasisi wa Tasisi ya Kuongoza na Kuwasaidia Vipofu ya Iran.
Khazaeli alipokuwa mtoto alipoteza nguvu ya kuona kutokana na ugonjwa wa ndui, na alipata elimu katika shule maalumu ya vipofu. Dakta huyo kwa kutumia uwezo wake mkubwa wa kuhifadhi mambo, alipata mafanikio makubwa katika masomo yake na kufanikiwa kuhitimu shahada ya uzamilifu ya sheria katika Chuo Kikuu cha Tehran.
Dakta Khazaeli alifahamu vyema lugha ya Kiarabu, Kifaransa na Kiingereza na aliandika na kutafsiri vitabu mbalimbali.
Miongoni mwa masuala aliyojishughulisha nayo ni kupigania kupatiwa huduma muhimu vipofu katika uga wa kimataifa na alikuwa pia mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Mashariki ya Kati katika Baraza la kitaifa la kuwahudumia vipofu na Jumuiya ya Kimataifa ya Vipofu. ***