Moshi ulikuwa bado unafuka kwenye mabaki ya makazi yaliyopo Mbumbulu yaliyoteketea, wakati Ngizwe Mchunu, alipoweka wazi msimamo wake.

Akiwa amesimama katikati ya majivu na vifusi vya rondavel (aina ya nyumba za jadi) zilizokuwa makazi ya mke wake wa tatu, Nqobile “Floda” Mthimkhulu, pamoja na watoto wao akitazama ardhi iliyoteketea, mali za familia yake, vitabu vya watoto vya shule na hali yao ya usalama vilikuwa vimegeuka majivu. Mwanamume huyo anayejitambulisha kama ‘Rais wa Taifa la Amabhinca’ alikaza uso na kutuma ujumbe kwa yeyote aliyewasha moto huo.

Shambulio hilo lilitekelezwa kwa mpangilio uliotia hofu. Wanaume watatu wasiojulikana walifika kwenye makazi hayo huko Mbumbulu, eneo lililo chini ya Mamlaka ya Kijadi ya Cele, kusini mwa Durban katika Jimbo la KwaZulu-Natal, wakimuulizia Mchunu kwa jina.

Mchunu hakuwapo nyumbani. Alikuwa Johannesburg. Mkewe, Floda pia hakuwa nyumbani bali Cape Town. Watu pekee waliokuwa nyumbani ni mfanyakazi wa ndani na watoto wa familia hiyo.

Wageni hao waliondoka pasipo kufanya chochote. Hata hivyo, muda mfupi baada ya kuondoka kwao, familia iligundua jambo la kutisha. Rondavel zilikuwa zimeanza kuwaka moto.

Nyumba kubwa na rondavel (majengo yenye umuhimu mkubwa wa kitamaduni) zilikuwa zimeteketea. Baadaye, Mchunu na Floda walipofika eneo la tukio walikuta magofu matupu.

Swali lililokuwa midomoni mwa raia wengi wa Afrika Kusini lilikuwa moja: Nani aliyefanya jambo hilo na kwa sababu gani?

“Matatizo ya muda mrefu hayawezi kumalizwa kwa usiku mmoja,” Mchunu aliliambia gazeti la Daily Sun.

“Kuna watu hapa nchini Afrika Kusini ambao sisi ni adui wao. Hao wanajua tunapoishi kwa sababu hakuna mgeni ambaye angekuja moja kwa moja kutafuta nyumba yangu ili aichome moto,” alisema.

Siku chache kabla ya moto huo, Mchunu alikuwa mstari wa mbele katika maandamano kupinga wahamiaji yaliyofanyika katikati ya Jiji la Durban.

Harakati zake za ‘Amabhinca Nation’ zinaungana na kundi la ‘March and March’ linaloongozwa na aliyekuwa mtangazaji wa redio, Jacinta Ngobese-Zuma. Kwa pamoja walikuwa wakiratibu maandamano ya mfululizo katika miji mikubwa ya Afrika Kusini (Durban, Johannesburg, Pretoria hadi KuGompo City (zamani East London) wakitaka raia wa kigeni wasio na nyaraka halali waondoke nchini humo kabla ya Juni 30, 2026.

Maandamano hayo yalikuwa na mvutano mkubwa, yalijaa watu wenye hasira na kwa kadiri siku zilivyokwenda yalizidi kuwa ya hatari.

Katika matukio mawili jijini Johannesburg, waandishi wa habari wa ‘Our City News’ walioshuhudia maandamano hayo waliripoti matukio ya vurugu.

Ilionekana kuwa mgogoro huo ulihamia moja kwa moja kwenye mlango wa nyumba ya Ngizwe Mchunu.

Huku wafuasi wake wakijitokeza kumuunga mkono, miongoni mwao akiwemo mwanasiasa mkongwe wa MKP na mshirika wake wa zamani Bonginkosi Khanyile, pamoja na Mwenyekiti wa ActionSA katika jimbo la KwaZulu-Natal, Zwakele Mncwango, kulikuwa pia na sehemu kubwa ya wananchi waliokataa kumpa Mchunu faida ya kuaminiwa bila masharti.

Hata katika kipindi alipopatwa na janga hilo nyumbani kwake, Ngizwe Mchunu hakuweza kukwepa mabishano.

Wakosoaji wake walijaa kwenye mitandao ya kijamii bila kuwasilisha ushahidi wowote, wakidai huenda alipanga tukio la moto kutafuta huruma na michango ya kifedha.

Mchunu alijibu madai hayo katika podikasti ya Durban Network, akisema: “Hakuna mtu anayeamka asubuhi akaamua kuchoma nyumba yake mwenyewe, hata awe amelewa kiasi gani.”

Akizungumza na ‘Daily Sun’ aligusa imani za utamaduni wa Kizulu: “Katika utamaduni wangu, moto ni laana. Kamwe siwezi kuchoma nyumba yangu kwa sababu ya kutafuta michango… Wanaofurahia wanaweza kufurahia na wanaonihurumia wanaweza kufanya hivyo. Mimi sitaacha kupambana.”

Hata hivyo, madhara ya moto huo hayakuishia katika maisha yake binafsi pekee. Jumatatu, Mei 12, 2026, Mahakama ya Durban ilikaa kwa kile kilichotarajiwa kuwa siku muhimu katika kesi ya muda mrefu inayomkabili Bonginkosi Khanyile, ambaye anashtakiwa kwa uchochezi, vurugu na kukiuka masharti ya COVID-19 kuhusiana na machafuko ya Julai 2021.

Mchunu alikuwa ametajwa kama shahidi katika kesi hiyo. Badala yake, mawakili wa Khanyile waliieleza mahakama kuwa Mchunu hakuweza kufika kwa sababu nyumba yake ilikuwa imechomwa moto mwishoni mwa wiki iliyopita. Kesi ikaahirishwa hadi siku nyingine. Nyumba iliyoteketea moto ilikatiza mwenendo wa haki mahakamani.

Mchunu ni mtu ambaye maisha yake yamekuwa yakigongana mara kwa mara na mfumo wa sheria wa Afrika Kusini, taasisi za kisiasa na makundi ya kiraia.

Kwa takribani muongo mzima amekuwa akiishi katikati ya migogoro, akipokea mashambulizi ya kisiasa na kijamii. Hata hivyo, ameendelea kujitokeza upande wa pili akiwa amejeruhiwa lakini hajasalimu amri.

Ili kuelewa kwa nini kuchomwa kwa nyumba yake kulilitikisa taifa, ni lazima kwanza umwelewe mtu huyo.

Ngizwe Mchunu alizaliwa Desemba 5, 1980 huko Nkandla, jimbo la KwaZulu-Natal, eneo la vijijini alikozaliwa Rais wa zamani, Jacob Zuma.

Ni zao la Afrika Kusini ambalo katika vipindi fulani elimu rasmi haikuwafikia watu wengi kwa urahisi. Ni mtu aliyejifunza kupitia uzoefu wa maisha na malezi aliyopata ndani ya sekta ya habari, badala ya madarasa na vitabu vya shule.

Alipata umaarufu kitaifa kama mtangazaji wa Ukhozi FM ya Shirika la Utangazaji la Afrika Kusini (SABC), kituo cha redio kinachosikilizwa zaidi barani Afrika kwa idadi ya wasikilizaji.

Sauti yake ikawa sehemu ya maisha ya kila siku katika mamilioni ya nyumba za KwaZulu-Natal. Lakini safari yake ndani ya kituo hicho ilimalizika kwa mgogoro, akituhumiwa kukiuka sera za usiri kwa kusambaza hadharani taarifa za ndani za kituo hicho.

Badala ya kutoweka na kusahaulika, Mchunu alijenga jukwaa lake. Septemba 2019 alianzisha redio ya mtandaoni ya Ngizwe Mchunu FM, hatua iliyokuwa ya ujasiri, ya kujitegemea na iliyolenga kuonyesha kuwa angeweza kuendelea kusimama hata baada ya kukataliwa na taasisi kubwa.

Kufungwa kwa shughuli nchini humo kutokana na COVID-19 kuanzia mwaka 2020 na kuendelea kulimgeuza kuwa mtu mwenye ushawishi zaidi kuliko awali.

Kama watu wengine duniani, alibanwa ndani ya mazingira ya vizuizi vya janga hilo, lakini tofauti ilikuwa katika nguvu ya mawasiliano na hadhira iliyokuwa imezoea mtindo wake wa maoni yasiyochujwa.

Alijitangaza kupitia Facebook na TikTok. Akajulikana kwa migogoro ya waziwazi na wasanii, kauli za kisiasa zilizokuwa zikichochea mabishano na msimamo mkali kuhusu uhamiaji.

Mwaka 2026 alidaiwa kujiunga na mtandao wa Podcast and Chill with MacG, hatua iliyopanua zaidi ushawishi wake katika ulimwengu wa kidijitali.

Katikati ya yote hayo; maandamano, kesi mahakamani, mapambano ya kisiasa na nyumba iliyochomwa moto anasimama kuwa mtu ambaye kwa wakati mmoja anaonekana kama nabii kwa wafuasi wake na mchochezi kwa wakosoaji wake. Mtu anayependwa na mamilioni ya watu, huku akichukiwa kwa kiwango hicho hicho na mamilioni wengine.

Moto wa Mbumbulu haukuwa tu shambulio la kuchoma nyumba binafsi. Kulingana na unayemuuliza, ulikuwa ni ama jaribio la kumtisha na kumnyamazisha mtu anayechukuliwa kuwa mtetezi wa wananchi wa kawaida au ni matokeo yasiyoepukika ya miaka ya kauli kali na uchochezi uliokuwa umefikia hatua ya kuwaka moto halisi.

Ili kuelewa ni simulizi ipi kati ya hizo mbili iliyo karibu zaidi na ukweli, ni lazima kurudi nyuma kwenye matukio yaliyomjenga Ngizwe Mchunu; kwenye machafuko ya Julai 2021 yaliyoitikisa Afrika Kusini na safari iliyomfikisha kusimama mbele ya magofu ya nyumba yake asubuhi ya Jumapili ya Mei, 2026.

Fuatilia sehemu ya pili ya mfululizo wa makala haya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *