Magonjwa yanayozua wasiwasi mkubwa ni pamoja na mafua ya ndege, homa ya nguruwe ya Afrika, ugonjwa wa midomo na miguu, Funza wa vidonda wa ulimwengu mpya au New World Screwworm, pamoja na magonjwa yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu kama Ebola, Nipah na virusi vya Hanta au hantavirus.

Kwa mujibu wa FAO, sekta ya mifugo inategemewa na zaidi ya watu bilioni moja duniani, hivyo kulinda afya ya wanyama ni muhimu kwa uhakika wa chakula, biashara na uchumi. 

Mkurugenzi Msaidizi Mkuu wa FAO anayesimamia Afya ya Wanyama, Dkt. Thanawat Tiensin, amesema, “Athari za milipuko hii zinaenda mbali zaidi ya afya ya wanyama. Husababisha usumbufu katika uzalishaji wa kilimo, biashara na utalii, kuhatarisha maisha ya watu na wakati mwingine afya ya binadamu.”

FAO imeeleza kuwa kuongezeka kwa usafirishaji wa wanyama, watu na bidhaa pamoja na changamoto za mazingira kumeongeza kasi ya kuenea kwa magonjwa hayo kuvuka mipaka. 

Shirika hilo limeongeza kuwa mafua ya ndege yamesababisha kupotea kwa zaidi ya ndege wa kufugwa milioni 633 duniani, huku ugonjwa wa midomo na miguu na homa ya nguruwe ya Afrika zikiendelea kusababisha hasara kubwa za kiuchumi.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Beth Bechdol, amesema, “Uzoefu unaonesha kuwa kinga na maandalizi ni nafuu zaidi na yenye matokeo bora kuliko kusubiri hadi mlipuko utokee. Uwekezaji katika mifumo ya afya ya wanyama ni njia muhimu ya kulinda maisha, kuimarisha biashara na uhakika wa chakula.”

FAO inaendelea kushirikiana na nchi wanachama na wadau mbalimbali kuimarisha uwezo wa kuzuia, kugundua mapema na kudhibiti milipuko ya magonjwa ya wanyama kupitia Programu ya Ushirikiano wa Kimataifa wa Magonjwa ya Wanyama ya Mipakani (GPP-TAD).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *