
Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni, jumla ya wagonjwa 19 wa Ebola wamethibitishwa nchini humo, vikiwemo vifo viwili.
Wagonjwa watano wamepona na kuruhusiwa kutoka hospitalini, wakati wagonjwa 12 bado wanaendelea na matibabu. Aidha, watu 415 wanafuatiliwa baada ya kukutana na wagonjwa, huku zaidi ya watu 300 wakimaliza kipindi cha ufuatiliaji cha siku 21 bila kuonesha dalili za ugonjwa huo.
UN yaongeza msaada wa kukabiliana na Mlipuko
Kwa mujibu wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO, ingawa mlipuko huo umejikita katika wilaya mbili pekee, zikiwemo maeneo ya mji mkuu Kampala, Uganda bado inakabiliwa na hatari kubwa kutokana na mpaka wake wa zaidi ya kilomita 800 na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Serikali ya Uganda imetangaza kupeleka wahudumu 80 wa afya mashariki mwa DRC kusaidia kudhibiti mlipuko na kuzuia maambukizi kuvuka mipaka. Chini ya uratibu wa Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa, mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaendelea kusaidia utekelezaji wa mpango wa taifa wa kukabiliana na Ebola.
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP imesafirisha tani 33 za misaada kwenda Bunia nchini DRC, huku Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia watoto UNICEF, na Uhamiaji IOM na la Wakimbizi UNHCR zikisaidia katika utoaji wa taarifa za kinga, uchunguzi mipakani, ufuatiliaji wa wagonjwa na huduma kwa wakimbizi. Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa na washirika wake wameomba dola milioni 15.8 kufadhili shughuli za kukabiliana na Ebola nchini Uganda hadi mwezi Agosti, huku pengo la ufadhili la dola milioni 12.7 bado likisalia.
Wiki hii, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, alitembelea Uganda na kupongeza juhudi za pamoja za serikali, Umoja wa Mataifa na washirika katika kudhibiti mlipuko huo.