MASHABIKI wa Simba wana kiu ya ubingwa kama ilivyo kwa viongozi wa klabu hiyo, lakini kocha wao, Steve Barker ameweka wazi msimamo mpya kuhusu usajili.

Simba tayari imeanza mchakato wa usajili na inadaiwa kuwa imeshawasajili wachezaji watatu wa ndani, wakiwemo viungo wawili na beki mmoja, wote wazawa, kwa lengo la kukiongezea nguvu kikosi hicho ili kiendelee kufanya makubwa kama kilivyofanya katika mechi 15 za mzunguko wa pili.

Akizungumza na Mwanaspoti, Barker amesisitiza hawataki kubahatisha katika usajili wa wachezaji wapya na benchi la ufundi kwa kushirikiana na viongozi litahakikisha wachezaji watakaosajiliwa wana uwezo wa kuongeza thamani zaidi ya waliopo kwa sasa.

Barker, raia wa Afrika Kusini, ameongeza Simba haitafanya mabadiliko makubwa ya kikosi, bali itasajili wachezaji wachache watakaokuja kuungana na wale waliofanya vizuri msimu huu unaomalizika.

“Mimi si shabiki wa kila dirisha la usajili kusajili wachezaji wengi. Napenda kufanya mambo kwa hesabu kulingana na mahitaji tuliyonayo. Ni kweli tutasajili wachezaji mwisho wa msimu huu, lakini ni wale am-bao tutaridhika kuwa watakuja kutuongezea kitu,” alisema Barker.

“Tuna timu nzuri, na wachezaji wengi wameonyesha uwezo mkubwa. Tunachotaka kufanya ni kuonge-za upana wa kikosi chetu. Wachezaji watakaokuja lazima wawe tayari kwa ushindani mkubwa na wale watakaowakuta.

“Kuna maeneo machache tutayaongezea nguvu, lakini sitalazimisha mabadiliko makubwa ya kikosi. Tutafanya usajili wa kimkakati zaidi. Kazi hiyo tumeshaianza muda mrefu kwa sababu kuna ulazima wa kufanya mambo mapema, lakini waliopatikana hadi sasa siwezi kuweka wazi majina yao.”

Kocha huyo aliyeshinda tuzo ya Kocha Bora wa Mwezi Mei aliongeza eneo la ushambuliaji ndilo litaka-lopewa kipaumbele zaidi, huku akihitaji muda wa kutosha kufuatilia maendeleo ya mabeki wake wa kati waliokuwa majeruhi.

“Eneo muhimu sana ni kwenye robo ya mwisho ya uwanja (eneo la ushambuliaji). Tutaweka nguvu kubwa hapo. Lakini unajua tuna mabeki wetu wawili wazuri, Nangu Wilson na Hamza Abdulrazack. Tunafuatilia kwa karibu maendeleo yao na tunataka kupata uhakika wa kupona kwao. Hilo pia ni eneo muhimu sana.”

BAFANA BAFANA YAMNYIMA RAHA

Juzi usiku, timu ya taifa ya Afrika Kusini (Bafana Bafana), ilipoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya wenyeji Mexico katika mechi ya ufunguzi wa fainali za Kombe la Dunia na Barker alisema matokeo hayo yalimnyima raha, huku akieleza kuwa uzoefu mdogo uliwaangusha.

“Tulianza mchezo kwa presha ya chini sana. Tulikuwa timu ya pili kwa kiwango kwa sehemu kubwa ya mchezo. Hayakuwa matokeo mazuri kwetu kabisa, lakini tunayapokea. Nadhani vijana waliathiriwa na ukosefu wa uzoefu wa kucheza mechi kubwa kama hizo. Tuna timu imara na naamini tutarudi kwa nguvu katika mechi zijazo,” alisema Barker.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *