MUSOMA: MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege (TAA) imefanya majaribio ya kutua na kuruka katika Viwanja vya Ndege vya Musoma na Shinyanga.

Majaribio hayo yamefanyika jana Juni 12,2026 na kufanywa kutumia ndege ya Kampuni ya Ndege Tanzania(ATCL).

Akizungumza katika hafla za majaribio hayo katika mikoa ya Mara na Shinyanga kuliko na viwanja hivyo, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema majaribio ya viwanja hivyo ni hatua muhimu katika mchakato wa udhibiti wa ubora wa miundombinu kabla ya kuanza kutumika .

“Mafanikio ya majaribio haya yanathibitisha kwamba kazi iliyofanyika inakidhi viwango vinavyohitajika vya kitaifa na kitaifa vya usalama, ubora na uendeshaji .Ni ishara ya utayari wa viwanja kuanza kutoa huduma katika usalama unaohitajika,” alieleza Profesa Mbarawa.

Kuhusu Kiwanja cha Ndege cha Musoma ambacho kimegharimu Sh bilioni 46, Profesa Mbarawa amesema kitasaidia kuchochea sekta ya utalii kwa kurahisisha ufikiaji wa vituo vya utalii vilivyopo katika mkoa wa Mara na maeneo ya jirani.

“Kuvutia uwekezaji katika sekta ya biashara,kilimo, mifugo, uvuvi na viwanda ,uharaka wa kusafirisha watu na mizigo, kuongeza jira na kipato kwa wananchi na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Mkoa wa Mara na maeneo mengine ya Tanzania ,” amefafanua .

Pia, ameeleza kuwa kutokana na uboreshaji huo, uwezo wa kiwanja hicho umeongezeka na kuwezesha kiwanja kupokea ndege kubwa zenye uwezo wa kubeba abiria 72 hadi 80.

“Hili ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na uwezo wa zamani ambapo kiwanja kilikuwa na uwezo wa kupokea ndege zenye uwezo wa kubeba abiria 42 ,” ameongeza.

Ameitaka   ATCL kuhakikisha maandalizi ya kuingiza kiwanja hicho kwenye safari zake yanafanyika hataka ambapo amesema Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Peter Ulanga amemhakikishia kuwa safari zitaanza mwezi ujao.

Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Abdul Mombokaleo amesema Aprili mwaka 2021 serikali ilianza kutekeleza mradi huo wa ukarabati na upanuzi wa kiwanja hicho.

Amesema kazi zilizofanyika katika mradi ni pamoja na ukarabati wa barabara ya kuruka na kutua kwa ndege kutokea urefu wa mita 1600 za changarawe hadi 1705 za kiwango cha lami .

“Ujenzi wa barabara mbili za maungio , ujenzi wa maegesho mapya ya ndege yenye uwezo wa kuhifadhi ndege kubwa za bombadier Q4 100 4 kwa wakati mmoja na ujenzi wa maegesho tengefu yenye mita za mraba 2800,” alifafanua.

Kwa upande wa Kiwanja cha Ndege cha Shinyanga, ameagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ambao ndio wanaotekeleza mradi huo kuhakikisha ujenzi wa kiwanja hicho unakamilika kwa asilimia 100 kufikia Septemba Mosi, mwaka huu ili ndege za abiria zianze kutua.

Aidha, mradi huo wa upanuzi na ukarabati wa uwanja umefikia asilimia 98 ambao umegharimu Sh bilioni 45.

Ameongeza kuwa kukamilika kwa kiwanja hicho ni kichochezi muhimu cha maendeleo kwa kuvutia utalii, uwekezaji katika sekta ya madini, kilimo, viwanda, biashara na kuimarisha usafirishaji wa kikanda na kimataifa, kupunguza muda wa kusafiri na kuongeza ajira na kipato kwa wananchi .

“Baada ya maboresho haya ndege ya bombadier Q400 au ATR 70 zinaweza kuja hapa ambazo zinaweza kubeba abiria kati ya 76 mpaka 80,” amesema.

Akielezea mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Abdul Mombokaleo amesema Aprili 2023, serikali ilianza kutekeleza mradi huo

Amesema fedha zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali likiwemo jengo la abiria linaloweza kubeba abiria 250,000 kwa mwaka, barabara ya kuruka na kutua ndege, njia ya maungio, maegesho ya ndege, maegesho ya magari, kituo cha umeme na uzio wa usalama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *