
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, ameelezea muundo wa makubaliano tarajiwa kati ya Iran na Marekani na kusisitiza kwamba diplomasia inakusudia kuimarisha mafanikio ya Jamhuri ya Kiislamu katika uwanja wa vita.
Katika mahojiano ya televisheni jana Ijumaa, mwanadiplomasia huyo mkuu aliitambua Jamhuri ya Kiislamu kama upande pekee ulioshinda katika uchokozi usio na sababu wa Marekani na Israel dhidi ya Iran, akisema matokeo ya uchokozi huo yameonyesha “mafanikio makubwa ya kimkakati.”
“Iran ndiyo mshindi wa vita hivi, na watu wa Iran ndio washindi halisi wa uwanja huu,” amesema Sayyid Araqchi.
Araqchi amekumbusha kuwa ushindi huo umepatikana, licha ya wavamizi wote wawili kumiliki na silaha za kisasa, pamoja na uwezo wa silaha za nyuklia, lakini wamezuiwa na Iran kufikia malengo yao.
“Kwa kawaida, baada ya ushindi kama huo, ni muhimu kuuimarisha kupitia makubaliano au maelewano,” amesema Sayyid Abbas Araqchi.
Ameongeza kuwa: Juhudi za kidiplomasia zinazolenga kuimarisha ushindi huo, na sasa ziko katika hatua za mwisho na zimetokana na hati ya makubaliano yenye vifungu 14 ambavyo vimejadiliwa kwenye vyombo vya habari. Amesisitiza kwamba hati hiyo bado inaweza kubadilika hadi itakapoidhinishwa kwa mara ya mwisho na kwamba maelezo yake yatatangazwa baada ya kukamilika.
Ameongeza kuwa mali zinazozuiliwa za Iran zitatolewa baada ya kusainiwa mkataba wa makubaliano, akiongeza kuwa mchakato wa kusaini makubaliano unaweza kufanyika katika muundo wa kidijitali katika kipindi cha siku moja au mbili.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa mada nyeti, likiwemo suala la nyuklia linalohusisha urutubishaji wa madini ya uranium na uranium iliyorutubishwa kwa kiwango cha juu, zimeahirishwa hadi hatua ya pili.