Wakati Marekani na Iran zikionekana, kwa mujibu wa vyombo vya habari, kuwa karibu kufikia makubaliano ya kuongeza muda wa usitishaji mapigano uliokubaliwa mwezi Aprili kati ya nchi hizo mbili na kuanza mazungumzo ya amani kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, jeshi la Israel leo Jumapili limeshambulia maeneo katika mji mkuu wa Lebanon yaliyotajwa kuwa na uhusiano na Hezbollah.

Shambulio hilo lililofanyika katika eneo la Dahiya, ngome ya kihistoria ya harakati za Kishia za Lebanon zinazoungwa mkono na Iran, linaripotiwa kuua watu wasiopungua watatu na kuwajeruhi wengine 16, kwa mujibu wa mamlaka za afya za Lebanon.

Shambulio wakati mbaya kabisa

Katika taarifa yake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amelaani vikali mashambulizi hayo ya Israel dhidi ya Beirut.

Aesema “Mashambulizi haya yamefanyika licha ya kuwepo kwa usitishaji mapigano na katika kipindi ambacho Marekani na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zinatarajiwa kufikia makubaliano yatakayofungua njia ya suluhisho la amani kwa mzozo huu” .

Kauli hiyo ya mkuu wa Umoja wa Mataifa inaangazia hatari kwamba kuongezeka tena kwa mapigano ya kijeshi kunaweza kuhatarisha mchakato wa kidiplomasia unaoendelea wa kumaliza vita vilivyoanza mwishoni mwa Februari, wakati Marekani na Israel ziliposhambulia vituo vya kijeshi na vya nyuklia vya Iran.

Baadaye, Tehran ilijibu kwa mashambulizi kadhaa yaliyolenga maslahi ya Marekani katika eneo la Ghuba ya Uajemi.

Kwa siku kadhaa sasa, vyombo vya habari vya kimataifa vimeripoti kuhusu rasimu ya makubaliano inayojumuisha kufunguliwa tena kwa mlango bahari wa Hormuz, njia muhimu kwa biashara ya nishati duniani, kuondolewa kwa vizuizi vya Marekani dhidi ya bandari za Iran, na kuongezwa kwa muda wa usitishaji mapigano uliokubaliwa wakati wa majira yachipukizi.

Masuala nyeti zaidi yanayohusu mpango wa nyuklia wa Iran, vikwazo vya kiuchumi na mfumo wa usalama wa kikanda yanatarajiwa kujadiliwa katika mazungumzo ya baadaye.

© UNHCR/Dar al-Mussawir Moshi unainuka juu ya vitongoji vya makazi huko Tiro, kusini mwa Lebanon, kufuatia shambulio la anga la Israel.(Kutoka Maktaba)

Uchumi wa dunia uko hatarini

Kwa António Guterres, suala hili linakwenda mbali zaidi ya Lebanon au hata uhusiano kati ya Marekani na Iran.

“Mzozo huu una athari kubwa na za kuharibu uchumi wa dunia,” amekumbusha leo Jumapili.

Tangu kuanza kwa vita hivyo, usumbufu wa usafirishaji katika Mlango bahari wa Hormuz njia ya kimkakati ambayo hupitisha takriban robo ya biashara ya mafuta yanayosafirishwa kwa njia ya bahari duniani pamoja na kiasi kikubwa cha gesi asilia iliyoyeyushwa na mbolea umesababisha kupanda kwa gharama za usafirishaji na bei za vyakula katika maeneo mbalimbali duniani kote.

Wito wa mwisho wa kujizuia

Akitambua hali nyeti ya wakati huu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa mwisho kwa pande zote zinazohusika.

“Nazihimiza pande zote kuonesha kiwango cha juu kabisa cha kujizuia katika kipindi hiki muhimu,” amesema.

Kauli hiyo inaakisi hali halisi ya mazungumzo yanayoendelea, yamefikia hatua inayoweza kutoa matumaini ya kupatikana kwa makubaliano, lakini bado ni dhaifu kiasi kwamba yanaweza kuvurugwa na mlipuko wowote mpya wa ghasia katika maeneo mbalimbali ya mzozo huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *