s

Chanzo cha picha, Getty Images

Iliyochapishwa

Muda wa kusoma: Dakika 9

Mwasi Haroun, mkazi wa Salasala, Dar es Salaam, amepikia kwa kuni na mkaa kwa zaidi ya miongo miwili. Kila asubuhi huanza siku yake kwa kuwasha moto jikoni kwa ajili ya familia yake, na mchana hadi jioni huendelea kuwasha moto kwa ajili ya kukaanga samaki anaouza kama shughuli yake kuu ya kipato.

Ndani ya nyumba yake, moshi mzito hujaa; macho kuwashwa hutokwa na machozi, na kifua kubana pamoja na kikohozi kimekuwa sehemu ya maisha ya kila siku.

Kama wanawake wengi nchini Tanzania, hasa vijijini, aliamini hali hiyo ni sehemu ya kawaida ya maisha isiyoepukika.

“Kwangu niliona ni jambo la kawaida. Ukipika kwa kuni lazima macho yawashe na kifua kibane. Lakini kadiri miaka ilivyokwenda nilianza kupata shida zaidi za macho na kupumua,” anasema Mwasi mwenye umri wa miaka 51.

Simulizi yake si ya kipekee. Ni picha ya maisha ya mamilioni ya Watanzania wanaoishi ndani ya moshi kila siku, bila kutambua kwamba changamoto wanayoiona ya kawaida ni tishio la muda mrefu la afya ya umma.

Kwa mujibu wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024–2034, takribani watu 33,000 hufariki dunia kila mwaka nchini Tanzania kutokana na athari za uchafuzi wa hewa ya ndani unaosababishwa na matumizi ya nishati chafu za kupikia kama kuni na mkaa.

Hivi si vifo vya ghafla vinavyoonekana hadharani. Ni vifo vya kimya kimya, vinavyotokea jikoni, ndani ya nyumba na pembeni ya majiko ya kuni na mkaa kila siku.

Idadi hii inapiku baadhi ya magonjwa makubwa, ikiwemo UKIMWI, ambao kwa mujibu wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) ulisababisha takribani vifo 24,000 mwaka wa 2023–2024.

Moshi unavyokuua taratibu

s

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

“Kupika ni jambo ambalo wengi wetu hulichukulia kuwa la kawaida; unawasha jiko na mara moja unapata nishati ya kuandaa chakula,” ilieleza blogu ya Mabadiliko ya Tabianchi ya Umoja wa Mataifa. “Hata hivyo, kwa mamia ya mamilioni ya watu duniani, kupika bado ni shughuli yenye hatari kubwa.”

Kwa miaka mingi nchini Tanzania, kuni na mkaa vilionekana zaidi kama mjadala wa uharibifu wa mazingira. Kwa mujibu wa Mkakati wa Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Misitu 2021-2031, takriban hekta 469,420 za misitu hupotea kila mwaka kutokana na shughuli za kibinadamu, ikiwemo ukataji miti kwa ajili ya kuni na uchomaji mkaa.

Hata hivyo, athari za matumizi ya kuni na mkaa haziko katika mazingira pekee. Kiuchumi na kijamii pia kuna gharama kubwa. Katika maeneo mengi ya vijijini, utafutaji wa kuni kwa ajili ya kupikia hutumia wastani wa saa sita kila siku, hali inayopunguza muda wa shughuli za kiuchumi na maendeleo ya familia. Zaidi ya hapo, wanawake hukumbana na changamoto za kiusalama wakiwemo vitendo vya ukatili wanapokwenda kutafuta kuni misituni, huku watoto wanaowasaidia wazazi wao wakipoteza muda wa masomo.

Licha ya athari hizo, wataalamu wa afya wanasema mjadala wa kuni na mkaa haukamiliki bila kuangazia kile kinachotokea ndani ya nyumba hewa inayovutwa kila siku na wanawake na watoto kutokana na moshi wa kupikia.

Mtaalamu wa afya, Dkt. Andrew Balankumye, anasema bado watu wengi hawajui kuwa moshi wa mkaa unaweza kusababisha kifo cha ghafla pamoja na magonjwa sugu ya muda mrefu.

“Mkaa unapowaka hutoa hewa ukaa (kaboni monoksaidi). Gesi hii ikiingia mwilini hushindana na oksijeni (hewa safi) kwenye damu. Matokeo yake mwili na ubongo hukosa oksijeni ya kutosha na mtu anaweza kupoteza maisha kimyakimya,” anasema.

s

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Anafafanua kuwa katika damu kuna chembe nyekundu zinazobeba oksijeni, lakini hewa ukaa hushikamana nazo kwa nguvu zaidi kuliko oksijeni, hivyo kuzuia usafirishaji wa hewa muhimu mwilini. Badala ya damu kubeba oksijeni, huanza kubeba sumu. “Ndiyo maana watu wanaweza kulala wakiwa na jiko la mkaa ndani ya nyumba iliyofungwa na wasiamke tena,” anaeleza. Wengine hufariki ghafla, wengine taratibu.

Mtaalamu wa magonjwa ya upumuaji na mfumo wa hewa Tanzania, Dkt Aden Mpangile anasema kukaa jikoni kwa saa moja ni sawa na kuvuta sigara 300 kama unapikia nishati ya kuni au mkaa

“Unaweza usione madhara leo ila baada ya miaka unaweza kujikuta ukiugua mfumo wa upumuaji, kushindwa kupumua kwa chanzo cha leo, “anasema Mpangile.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa watu milioni 2.9 hufariki dunia kila mwaka kutokana na magonjwa yanayohusishwa na uchafuzi wa hewa majumbani unaosababishwa na matumizi ya nishati zisizo safi kama kuni na mkaa.

Athari kubwa zaidi huonekana katika magonjwa ya moyo yanayochangia 32% ya vifo hivyo, yakifuatiwa na kiharusi (23%), maambukizi ya njia ya hewa na mapafu kama nimonia (21%), ugonjwa sugu wa mapafu (COPD) (19%) na saratani ya mapafu (6%). Takwimu hizi zinaonesha kuwa matumizi ya nishati chafu ya kupikia si suala la mazingira pekee, bali pia ni tishio kubwa kwa afya ya umma.

Wanawake na watoto ndiyo waathirika wakubwa zaidi kwa sababu hutumia muda mwingi karibu na majiko ya kupikia. Kwa Mwasi, uhalisia huo hauhitaji maelezo ya kitaalamu zaidi.

“Nikitoka jikoni macho lazima yawe mekundu sana. Kikohozi ni kawaida kwangu. Sikujua kama wengi tunaishi kwenye hatari ambayo hatuijui,” anasema.

Kuni na mkaa bado vinatawala majiko Tanzania

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Licha ya ushahidi huo wa athari zake, kuni na mkaa bado vinatawala majiko ya Watanzania. Kwa mujibu wa takwimu za serikali, karibu asilimia 90 ya kaya hutumia kuni au mkaa kama chanzo kikuu cha nishati ya kupikia. Kati ya hizo, asilimia 63.5 hutumia kuni na asilimia 26.2 hutumia mkaa.

Nishati safi kama gesi, umeme na biogesi bado zinabaki kuwa chaguo la wachache. Takwimu za Benki ya Dunia zinaonyesha kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia Tanzania yaliongezeka kutoka asilimia 1.5 mwaka 2010 hadi asilimia 6.9 mwaka 2021, kiwango ambacho bado ni kidogo ikilinganishwa na wastani wa dunia unaozidi asilimia 70.

Sababu kuu zinazotajwa ni gharama, upatikanaji na mazoea ya muda mrefu. Vijijini, kwa mfano, kuni hupatikana bila malipo ya moja kwa moja, huku mijini mkaa ukinunuliwa kidogo kidogo kulingana na uwezo wa kipato cha kaya.

Utafiti mmoja wa kulinganisha gharama na athari za kiafya za nishati za kupikia unaonyesha tofauti kubwa kati ya kuni, mkaa na gesi. Mhadhiri na mtaalamu wa nishati safi, Gerutu Bosinge, anasema walichobaini katika utafiti huo: “Kwenye kuni, familia ya watu watano hutumia takriban kilo sita kwa siku, sawa na takriban tani 2.3 kwa mwaka. Kiasi hicho huchangia uzalishaji wa hewa chafu unaozidi tani 3.3 kwa mwaka,” anasema.

Anaongeza: “Kwa mkaa, matumizi ya wastani ni takriban kilo tatu kwa siku, sawa na takriban tani 1.2 kwa mwaka, na huzalisha hewa chafu inayozidi tani 11 kwa mwaka. Hii ina athari kubwa kiafya kwa taifa. Lakini kwa gesi, matumizi ni takriban nusu kilo kwa siku bila athari kubwa za hewa ukaa zinazolingana na kuni na mkaa.”

Hata hivyo, wataalamu wanaonya kuwa gharama ya sasa ya kutumia kuni na mkaa inaweza kuonekana ndogo ukilinganisha na gharama za kiafya zinazolipwa baadaye.

Mtaalamu wa magonjwa ya upumuaji na mfumo wa hewa nchini Tanzania, Dkt. Aden Mpangile, anasema hata muda mfupi wa kukaa jikoni kwenye mazingira ya moshi mzito unaweza kuwa na athari kubwa kiafya kwa muda mrefu.

“Unaweza usione madhara leo, lakini baada ya miaka unaweza kujikuta ukiugua magonjwa ya mfumo wa upumuaji au kushindwa kupumua vizuri kutokana na athari zilizoanza polepole,” anasema Mpangile. Anaongeza kuwa kukaa jikoni kwa takriban saa moja kwenye moshi wa kuni au mkaa kunaweza kuwa na athari sawa na kuvuta sigara mamia ya sigara kwa siku.

Vita dhidi ya kuni na mkaa na mapinduzi ya nishati safi

S

Chanzo cha picha, URT

Kutokana na ukubwa wa changamoto ya matumizi ya nishati zisizo safi, Serikali ya Tanzania kupitia ajenda ya upatikanaji wa nishati safi Afrika ilizindua Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024–2034.

Mkakati huo uliozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan mwaka 2024 unalenga kufikia angalau asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034. Tayari, Serikali inasema mabadiliko yameanza kuonekana, ingawa safari bado ni ndefu.

Mkakati huo unalenga kubadilisha mfumo mzima wa upikaji nchini kupitia matumizi ya gesi ya kupikia (LPG), umeme, gesi asilia, biogesi, bayoethanoli, majiko banifu, pamoja na mkaa mbadala unaotokana na mabaki ya kilimo kama miwa, mpunga, maranda ya mbao na pumba.

Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita Serikali imegawa majiko banifu 200,000 yenye ruzuku, umeanza mpango wa majaribio wa majiko ya umeme 480 kupitia bili ya umeme kwa kushirikiana na TANESCO, pamoja na kusambaza mitungi ya gesi ya LPG zaidi ya 450,000 kwa bei ya ruzuku.

Shule ya Sekondari ya Wasichana ni moja ya taasisi 453 nchini, zinazonufaika na uunganishwaji wa miundombinu ya nishati safiya kupikia chini ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA). Mkuu wa shule hiyo, Mwl. Flora Nusu ameeleza mbali na kuondoa athari za kiafya, nishati mbadala inaokoa muda uliokuwa ukipotea katika kutafuta kuni, na pia kupunguza gharama za uendeshaji kwa asilimia 40.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia katika Wizara ya Nishati, Nolasco Mlay, kiwango cha matumizi ya nishati safi kimeanza kuongezeka katika miaka ya hivi karibuni.

“Mwaka 2021, takriban asilimia 6.6 ya Watanzania walikuwa wanatumia nishati safi ya kupikia. Leo, takriban asilimia 28.6 tayari wameanza kutumia nishati safi,” anasema.

Hata hivyo, tofauti kubwa kati ya lengo la asilimia 80 na kiwango cha sasa inaonesha ukubwa wa changamoto iliyopo, hususan katika maeneo ya vijijini ambako gharama na upatikanaji bado ni kikwazo kikuu.

Serikali pia imeongeza juhudi kupitia mikutano ya kikanda na kitaifa ya nishati safi, ikizileta nchi za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Malawi mwaka ulipita kwenye kongamano la nishati safi na juma lililopita limefanyika kongamano lingine, pamoja na kutoa ruzuku ya dola milioni 10.1 ili kuboresha upatikanaji wa nishati hiyo na kuongeza uhamasishaji kwa wananchi.

Vita ambayo Tanzania haiwezi kuipoteza

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Takwimu zinaonyesha kuwa bado takriban asilimia 20 tu ya kaya nchini Tanzania ndizo zinazofikiwa na suluhisho la nishati safi ya kupikia, hali inayoacha sehemu kubwa ya wananchi wakiendelea kutegemea kuni na mkaa.

Inakadiriwa kuwa ili kuzalisha tani moja ya mkaa, kati ya tani 10 hadi 12 za magogo hukatwa. Kwa mujibu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), takriban hekta 46,606 za misitu huharibiwa kila mwaka kutokana na mnyororo wa uzalishaji wa mkaa na matumizi ya kuni.

Dar es Salaam pekee hutumia zaidi ya nusu ya mkaa wote unaozalishwa nchini Tanzania, kwa mujibu wa ripoti ya The Potential and Optimal Strategies for Charcoal Sub-Sector Development in Tanzania ya mwaka 2019. Wakati huo huo, tathmini za Global Forest Watch zinaonyesha kuwa Tanzania ilipoteza takriban hekta milioni 3.48 za misitu kati ya mwaka 2001 na 2024, ambapo mwaka 2024 pekee ilipoteza hekta 271,000.

Wataalamu wa mazingira wanasema changamoto ya upatikanaji wa miundombinu ya nishati safi vijijini imechangia kwa kiasi kikubwa kuendelea kwa matumizi ya kuni na mkaa.

Hata hivyo, sekta ya mkaa bado ni chanzo muhimu cha mapato kwa maelfu ya wananchi. Takwimu zinaonyesha kuwa mapato ya sekta hiyo yaliongezeka kutoka dola milioni 1.3 mwaka 2023 hadi dola 2.9 milioni mwaka 2025.

Hii inaifanya vita dhidi ya kuni na mkaa kuwa ngumu zaidi, kwa sababu ni vita inayogusa uchumi, ajira, mazingira na afya kwa wakati mmoja.

“Nauza mkaa kwa miaka saba sasa. Mkaa ndio maisha yangu, naendesha familia, nasomesha watoto. Nikiacha nitaishije?” anauliza Seko Urio.

Hata hivyo, wataalamu wanaonya kuwa gharama ya kutofanya mabadiliko ni kubwa zaidi kuliko faida ya muda mfupi ya sasa. Kila mwaka maelfu hupoteza maisha, maelfu huugua, na mamilioni wanaendelea kuishi katika hatari isiyoonekana ya uchafuzi wa hewa majumbani.

Mkaa na kuni, janga la kimya la dunia

a

Chanzo cha picha, Getty Images

Matumizi ya kuni na mkaa si changamoto ya Tanzania pekee. Kwa mujibu wa Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), suala la kupika kwa kutumia nishati zisizo safi ni changamoto ya dunia nzima inayohitaji suluhisho la pamoja.

Kwa mujibu wa Shirika la Nishati Duniani (IEA) pamoja na Benki ya Dunia, zaidi ya watu bilioni 2.1, bado wanategemea nishati zisizo safi za kupikia, wengi wao ni kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Wataalamu wa afya wanasema hali hii ni janga la kimya kimya linaloendelea kuathiri maisha ya mamilioni ya watu kila siku. Shirika la Afya Duniani linakadiria kuwa, zaidi ya watu 800,000 barani Afrika hufariki kila mwaka kutokana na uchafuzi wa hewa ya ndani unaosababishwa na matumizi ya nishati chafu za kupikia, ikiwemo mkaa na kuni.

Hata hivyo, baadhi ya nchi barani Afrika zimeanza kuonyesha njia ya mabadiliko. Kenya imepiga hatua kubwa katika matumizi ya nishati safi ya kupikia, ambapo zaidi ya theluthi ya kaya tayari zinatumia nishati safi, huku serikali na sekta binafsi zikisaidia upatikanaji wake kupitia mifumo bunifu ya usambazaji na ruzuku.

Ghana imeongeza upatikanaji wa gesi ya kupikia kupitia mfumo wa kurahisisha ugawaji wa mitungi kwa wananchi, Ethiopia ikitumia nguvu kubwa ya umeme wa maji kuongeza matumizi ya nishati safi vijijini, na Senegal nayo imepunguza utegemezi wa kuni mijini kupitia sera za ruzuku ya gesi.

Kwa Tanzania, inayolenga kuhakikisha angalau kaya 8 kati ya 10 za watanzania zinatumia nishati safi ifikapo 2034, mifano hii inaleta funzo muhimu kwamba; changamoto ya nishati safi ni ya dunia, lakini kasi ya suluhisho ndiyo inayoamua ni nchi gani zinapunguza madhara mapema zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *