DAR ES SALAAM: Serikali imeanza safari ya kuondoa uchimbaji wa kubahatisha nchini baada ya kuweka mfumo utakaowezesha asilimia 10 ya makusanyo ghafi ya mapato ya madini kubaki kwenye Sekta ya Madini kwa ajili ya kugharamia utafiti na uwekezaji.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema hatua hiyo ni moja ya maamuzi makubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan katika kutatua changamoto za muda mrefu zinazowakabili wachimbaji wadogo, hasa ukosefu wa taarifa sahihi za kijiolojia, mitaji, teknolojia na mikopo rafiki.
Mavunde amesema Rais Samia amekuwa akisikiliza changamoto za wachimbaji na wadau wa Sekta ya Madini, na kwamba uamuzi wa kurejesha sehemu ya mapato ya madini kwenye utafiti unaonesha dhamira ya Serikali kuhakikisha ukuaji wa sekta hiyo unawanufaisha zaidi Watanzania.

Ameyasema hayo wakati wa hafla ya kupokea Ripoti ya Mapendekezo ya Kuwaendeleza Wachimbaji Wadogo wa Madini nchini, iliyopokelewa na kuzinduliwa rasmi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Alexander Mkumbo, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/2027, Wizara ya Madini itaanzisha Mfuko wa Utafiti wa Madini, ambapo asilimia 10 ya makusanyo ghafi ya mapato ya madini itabaki kwenye sekta kwa ajili ya kugharamia utafiti na uwekezaji.
Mavunde amesema utafiti ndiyo msingi wa uchimbaji wenye tija, kwa kuwa humsaidia mchimbaji kujua eneo lenye mashapo ya madini, kupanga uwekezaji, kuchagua teknolojia sahihi na kuandaa taarifa zinazoweza kumuwezesha kukopesheka kwenye taasisi za fedha.
Amesema changamoto kubwa kwa wachimbaji wengi wadogo siyo kukosa juhudi, bali kufanya kazi bila taarifa za uhakika kuhusu madini yaliyopo katika maeneo yao, jambo linaloongeza gharama, kupunguza tija na kuifanya miradi mingi kuonekana hatarishi mbele ya taasisi za fedha.

Mavunde amesema Serikali inataka kuona wachimbaji wadogo wakiondoka kwenye uchimbaji wa kubahatisha na kuingia kwenye uchimbaji unaoongozwa na taarifa sahihi, teknolojia, usalama na mipango inayoweza kuwasaidia kuongeza uzalishaji na kukua kibiashara.
Akizungumza wakati wa kupokea ripoti hiyo, Prof. Mkumbo amesema wachimbaji wadogo ni sehemu muhimu ya uchumi wa madini nchini kwa kuwa wanachangia takriban asilimia 40 ya mapato yatokanayo na shughuli za madini, huku wakitoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa maelfu ya Watanzania, wakiwemo vijana na wanawake.

Prof. Mkumbo amesema pamoja na mchango huo mkubwa, wachimbaji wadogo bado wanakabiliwa na changamoto za mitaji, teknolojia, gharama kubwa za utafiti, upatikanaji mdogo wa taarifa za kijiolojia, masoko na huduma za kifedha.
Amesema ripoti hiyo imekuja wakati muhimu kwa kuwa Serikali inaendelea kuweka mazingira ya kuwasaidia wachimbaji wadogo kuongeza tija, kupanua uzalishaji na kukua kutoka uchimbaji mdogo kwenda uchimbaji wa kati na hatimaye uchimbaji mkubwa unaomilikiwa na Watanzania.
Kwa upande wake, Mavunde amesema Wizara ya Madini inaendelea kutekeleza Mining Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri, ambayo inalenga kuongeza eneo lililofanyiwa utafiti wa kina kutoka asilimia 16 iliyopo sasa hadi asilimia 50 ifikapo mwaka 2030.

Amesema moja ya nguzo muhimu za dira hiyo ni kukuza na kuendeleza uchimbaji mdogo, kwa kutambua nafasi yake katika uzalishaji, ajira, mapato ya Serikali na ushiriki wa Watanzania kwenye uchumi wa madini.
Mavunde amesema Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa, STAMICO, kwa kushirikiana na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania, GST, imeendelea kutoa huduma za utafiti na uchorongaji kwa wachimbaji wadogo, ikiwemo matumizi ya mitambo 15 ya kisasa ya uchorongaji miamba.
Amesema huduma hizo zinawasaidia wachimbaji wadogo kupata taarifa za mashapo ya madini katika maeneo yao, kufanya maamuzi sahihi ya uzalishaji na kuongeza nafasi ya miradi yao kuaminika mbele ya taasisi za fedha.

Ripoti iliyozinduliwa imependekeza kuimarishwa kwa mifumo ya fedha kwa wachimbaji wadogo, kuongeza ushiriki wa benki na taasisi za fedha, kupanua upatikanaji wa taarifa za kijiolojia, kutumia teknolojia ya kisasa, kuimarisha masoko na kuongeza thamani ya madini ndani ya nchi.
Aidha, ripoti hiyo imependekeza uwezekano wa kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Madini utakaosaidia kuongeza upatikanaji wa mitaji kwa wachimbaji wenye maeneo yenye uwezo lakini wanaokosa dhamana, mitambo na nyaraka za kitaalamu zinazohitajika kupata mikopo.
Prof. Mkumbo amesema moja ya maeneo muhimu katika mapendekezo hayo ni kuwawezesha wachimbaji wadogo wenye uwezo kukua hadi kufikia uchimbaji wa kati na baadaye uchimbaji mkubwa unaomilikiwa na Watanzania.
Amesema mabadiliko hayo yatahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Wizara ya Madini, taasisi zake, sekta binafsi, taasisi za fedha, vyuo vikuu, taasisi za utafiti, vyama vya wachimbaji na wadau wa maendeleo.
Mavunde amesema Wizara itaendelea kujenga uaminifu kati ya wachimbaji wadogo na taasisi za fedha kwa kuimarisha utunzaji wa kumbukumbu za uzalishaji, elimu ya biashara ya madini, uchimbaji salama, utunzaji wa mazingira na matumizi ya taarifa sahihi za kijiolojia.
Amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua za kudumu katika kutatua changamoto zinazowakabili wachimbaji wadogo, ikiwemo huduma za utafiti kupitia STAMICO na GST, uratibu wa uanzishwaji wa Benki ya Wachimbaji Wadogo na elimu ya kuwasaidia wachimbaji kuendesha shughuli zao kwa mfumo rasmi zaidi.
Hatua hiyo inatarajiwa kuwaondoa wachimbaji wadogo kwenye uchimbaji wa kubahatisha na kuwaingiza kwenye uchimbaji unaoongozwa na taarifa sahihi, mitaji, teknolojia na masoko, ili mchango wao kwenye uchumi wa madini uongezeke zaidi.
Serikali imeweka fedha kwenye utafiti wa madini ili uchimbaji mdogo uwe na tija zaidi, upate nguvu ya kifedha na uchangie kwa ukubwa zaidi katika ukuaji wa uchumi wa taifa.