Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) Gianni Infantino amesema, taasisi hiyo haiwezi kutatua ‘masuala ya kijiopolitiki’, licha ya kuendelea kuandamwa na mashinikizo kimataifa ya kuitaka isimamishe uanachama wa Israel kutokana na vita vya kinyama na mauaji ya kimbari unayoendelea kufanya utawala huo wa kizayuni dhidi ya Wapalestina wa Ghaza, ambayo hadi sasa yameshateketeza roho za watu zaidi ya 65,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Kupitia taarifa aliyotoa siku ya Alkhamisi, Infantino “amegusia umuhimu wa kuimarishwa amani na umoja kwa muktadha wa kinachoendelea huko Ghaza.”

“Kama FIFA, tunatumia mchezo wa soka kuwaleta watu pamoja,” amedai Infantino na kuendelea kusema: “fikra zetu zipo kwa wale wanaoendelea kuteseka maeneo mbalimbali yaliyokumbwa na machafuko, lakini kwa sasa ujumbe mahususi ni umoja na amani.”

Rais huyo wa shirikisho la soka duniani ameendelea kusema, FIFA haiwezi kutatua masuala ya kijiopolitiki, lakini ina wajibu wa kukuza mchezo wa soka ulimwenguni, kwa kuandaa nyenzo za kuunganisha watu.

Infantino ametoa maelezo hayo katika kile kinachoonekana kama uamuzi wa kutetea uamuzi wa kutojadili suala la kutengwa Israel katika mkutano wa baraza la shirikisho hilo uliofanyika jana Alkhamisi.

Siku ya Jumatano Makamu wa rais wa FIFA Victor Montagliani alitangaza kuwa Muungano wa Vyama vya Soka vya Ulaya UEFA  ndio unaopaswa kutoa uamuzi kuhusu Israel.

Ikumbukwe kuwa, mnamo mwaka 2022, shirikisho hilo la soka duniani liliifungia Russia kushiriki mashindano ya kombe la dunia la soka yaliyofanyika nchini Qatar baada ya kuanzisha vita dhidi ya Ukraine, lakini hadi sasa imeshindwa kuchukua hatua dhidi ya Israel.

Hii ni katika hali ambayo, mnamo mwezi uliopita wa Septemba, tume ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa ilitangaza rasmi kuwa utawala wa kizayuni wa Israel unafanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina huko Ghaza…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *