
Dar es Salaam. Makubaliano ya kusitisha vita kati ya Marekani na Iran yaliyothibitishwa na pande zote mbili yameibua matumaini mapya katika masoko ya nishati duniani.
Ripoti zilizoripotiwa na mashirika mbalimbali ya habari kutoka ukanda huo yakiwemo BBC, Shirika la habari la Mehr pamoja na ukurasa wa mawasiliano wa Rais wa Marekani Donald Trump, zinafafanua makubaliano hayo yalivyofikiwa.
Aidha, mataifa na wadau wakielekeza macho yao kwenye uwezekano wa kurejea kwa amani katika usafirishaji wa mafuta kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz, njia muhimu inayotumika kusafirisha mafuta na gesi asilia iliyoyeyushwa duniani.
Matumaini hayo, yanakuja baada ya Rais Trump, kutangaza kupitia mtandao wake wa Truth Social kuwa, “Makubaliano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yameafikiwa,” akisema pia ameridhia kufunguliwa kwa Mlango wa Hormuz na kuondolewa kwa zuio la majini la Marekani dhidi ya Iran.
“Mafuta yaanze kutiririka!” ameandika Trump, kabla ya kufafanua baadaye usafirishaji huo utaanza baada ya makubaliano kutiwa saini rasmi Juni 19, 2026.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Kazem Gharibabadi, amethibitisha kupitia televisheni ya taifa hilo makubaliano hayo yamekamilishwa na hafla rasmi ya kutiwa saini itafanyika nchini Uswisi Juni 19.
“Itatangazwa jioni hii kwamba mapigano na operesheni za kijeshi katika nyanja mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Lebanon, zitamalizika mara moja na kudumu,” amesema.
Mapigano hayo na kufungwa kwa mlango huo wa Hormuz kumesababisha bei ya mafuta kupanda duniani ikiwemo Tanzania.
Kupanda kwa mafuta kumechagiza gharama za vitu mbalimbali navyo kupanga kama nauli za usafiri wa ardhi na majini. Vyakula navyo maeneo mbalimbali vimepanda kutokana na gharama za usafirishaji.
Maumivu ya mafuta yalivyoibuka
Vita kati ya mataifa hayo vilianza baada ya mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran Februari 28, kabla ya Tehran kujibu kwa mashambulizi dhidi ya Israel na washirika wa Marekani katika eneo la Ghuba.
Hali hiyo ilisababisha kufungwa kwa Mlango-Bahari wa Hormuz, (njia nyembamba ya bahari iliyopo kati ya Iran na Oman, inayounganisha Ghuba ya Uajemi na Ghuba ya Oman. Ni eneo kuu la uchumi wa dunia unaopitisha takriban asilimia 20 ya usambazaji wa mafuta ghafi na gesi asilia (LNG) kwa matumizi ya kimataifa), kuhusu usalama wa usafirishaji wa nishati katika moja ya njia nyeti zaidi za biashara duniani.
Kwa mujibu wa takwimu za soko la mafuta duniani, kabla ya kuanza kwa vita vya Mashariki ya Kati mwishoni mwa Februari 2026, bei ya pipa moja ilikuwa ikiuzwa takribani Sh189,228. Vita vilipozidi kupamba moto na usafirishaji kupitia mlango huo kusitishwa, bei ilipanda hadi kilele cha takribani Sh358,800 kwa pipa Aprili.
Kufuatia makubaliano ya amani kati ya Marekani na Iran, bei ilianza kushuka na kufikia takribani Sh215,124 kwa pipa, hali iliyorejesha matumaini ya nafuu ya gharama za nishati duniani.
Licha ya pande hizo kukubaliana kusitisha mapigano Aprili 2026, mashambulizi ya mara kwa mara yaliendelea, hatua iliyopelekea kupanda kwa gharama za nishati ya mafuta duniani kote.
Saa chache kabla ya tangazo la makubaliano mapya yaliyofikiwa, mashambulizi ya Israel katika vitongoji vya kusini mwa Beirut, Lebanon, yakizua tena mashaka kuhusu mustakabali wa mazungumzo hayo.
Hata hivyo, Trump mwenyewe alikiri wasiwasi huo akisema mashambulizi hayo hayakupaswi kutokea, hasa katika kipindi ambacho pande hizo zinafikia makubaliano ya amani.
Matumaini yalivyorejea
Kabla ya Marekani na Iran kuthibitisha makubaliano hayo, Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, aliyekuwa akifanya kazi kama mpatanishi, alitangaza baada ya mazungumzo ya kina, pande hizo zimefikia makubaliano ya amani.
“Kufuatia mazungumzo ya kina, tuna furaha kutangaza kwamba makubaliano ya amani yamefikiwa kati ya Marekani na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran,” alisema Sharif.
Kwa mujibu wa Shirika la habari la Mehr, rasimu ya makubaliano hayo inajumuisha kusitishwa kwa mapigano kwa kudumu katika maeneo yote, ikiwemo Lebanon, kuondolewa kwa vikwazo dhidi ya mafuta na sekta ya nishati ya Iran na kufunguliwa kwa Mlango wa Hormuz ndani ya siku 30.
Aidha, ujumbe wa Rais Trump alioandika kuwa, “mafuta yaanze kutiririka” umeamsha matumaini hayo zaidi kwa wadau.
Hatua hiyo imeibua matumaini kuwa gharama za usafirishaji na usambazaji wa mafuta duniani utarudi katika hali yake ya kawaida, hivyo kuondoa shinikizo la gharama linaloendelea duniani kwa muda wa miezi kadhaa sasa.
Katika makubaliano hayo, Marekani imeahidi pia kutoweka vikwazo vipya wala kuongeza wanajeshi wake katika eneo hilo, hatua inayoashiria uwezekano wa kurejea amani ya kudumu.
Makubaliano hayo pia yanaripotiwa kujumuisha mpango wa kutoa msaada wa ujenzi na uwekezaji wa zaidi ya Sh787.5 trilioni kwa Iran, huku hatua za mwisho zikitarajiwa kupitishwa na azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Wadau wapongeza mwafaka huo
Makubaliano hayo yamepokelewa kwa matumaini na viongozi mbalimbali duniani, wakionesha uhitaji wa amani ya kudumu katika eneo hilo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan, amesema nchi yake inakaribisha makubaliano hayo na kutumaini mazungumzo yatakayofuata yataendelea kwa njia ya kujenga.
Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, amesema ana matumaini kuwa hatua hiyo itachangia kuleta amani ya kudumu katika eneo hilo, huku viongozi wa Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Italia wakisema ni fursa ya kurejesha utulivu wa kikanda na kusaidia uchumi wa dunia.