Leo Juni 15, Hispania itatupa karata yake ya kwanza kwenye Kombe la Dunia la mwaka huu.

Watawakaribisha DUNIANI wawakilishi wa Afrika, Cape Verde, kwenye mchezo wao wa kwanza wa kundi H, mjini Atlanta, nchini Marekani.

Mchezo huu utaanza saa moja kamili usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

Kwenye makaratasi sio mchezo mgumu kwa Hispania, lakini mpira kama mpira, uwanjani huwa kuna matokeo tofauti.

Mwaka 2010 Hispania ilikutana na Uswisi kwenye mchezo wa kwanza wa kundi.

Na kwenye makaratasi hali ilikuwa hivi hivi lakini uwanjani ikawa tofauti na Hispania wakapoteza 1-0.

Kwa hiyo mchezo huu sio wa kuubeza hata kidogo, chochote kinaweza kutokea.

Na kama itatokea Hispania wakapoteza mchezo huu basi huo utakuwa ukamilifu wa utabiri ikiashiria moshi mweupe kwao.

Hii ni kwa sababu sio tu wanapewa nafasi kubwa ya kushinda mchezo huu, bali mashindano yenyewe kwa ujumla.

Hispania ni timu yenye mizania sahihi ya kikosi kuanzia golini hadi safu ya ushambuliaji.

Uchambuzi wa ubora wa kikosi chao nitaufanye huko mbele, lakini kwanza tuangalie mgongano huu wa ajabu wa matukio.

Hadi sasa tayari kuna matukio kumi yametokea, yenye mfanano wa moja kwa moja na yale yaliyotokea mwaka 2010.

1. Kundi la Kombe la Dunia

Mwaka 2010 Hispania walipangwa kundi H.

Mwaka 2026 Hispania wamepangwa tena kundi H.

2. Barcelona

Mwaka 2010 kikosi cha Hispania kilikuwa na wachezaji nane kutoka Barcelona.

Mwaka 2026 tena kikosi cha Hispania kina wachezaji nane kutoka Barcelona.

3. Real Madrid

Mwaka 2010 Real Madrid ilimaliza msimu bila taji lolote.

Mwaka 2026 Real Madrid tena umemaliza msimu bila taji lolote.

4. Atletico Madrid

Mwaka 2010 Atletico Madrid ilipoteza fainali ya Copa Del Rey.

Mwaka 2026 Atletico Madrid imepoteza tena fainali ya Copa del Rey.

5. Shakira

Mwaka 2010 Shakira ndio alikuwa mwimbaji wa wimbo rasmi wa Kombe la Dunia.

Mwaka 2026 Shakira tena ndio mwimbaji wa wimbo rasmi wa Kombe la Dunia.

6. Marcel Bielsa

Mwaka 2010 Marcel Bielsa akiwa kocha wa Chile, nchi inayozungumza kihispaniola, alikutana na Hispania kwenye hatua ya makundi.

Mwaka huu, akiwa na Uruguay nchi inayoongea Kihispaniola, Bielsa tena anakutana na Hispania kwenye hatua ya makundi.

7. Jose Mourinho

 Mwaka 2010 Jose Mourinho alijiunga na Real Madrid.

Mwaka 2026 Jose Mourinho amejiunga tena na Real Madrid.

8. Mechi ya ufunguzi

Mwaka 2010 mechi ya ufunguzi ilikuwa kati ya Afrika Kusini na Mexico, na ilifanyika Juni 11.

Mwaka 2026 mechi ya ufunguzi ni Afrika Kusini na Mexico na imefanyika Juni 11.

9. Mabingwa wa Ulaya

Mwaka 2010 Hispania walishiriki Kombe la Dunia wakiwa mabingwa wa Ulaya.

Mwaka 2026 Hispania wanashiriki Kombe la Dunia wakiwa mabingwa wa Ulaya.

10. Javier Aguirre

Mwaka 2010 Javier Aguirre alikuwa kocha wa Mexico akiichukua timu baada ya kupitia kipindi kibaya cha mfululizo wa matokeo yasiyoridhisha kuelekea Kombe la Dunia.

Mwaka 2026 Javier Aguirre amekuwa tena kocha wa Mexico akiichukua timu baada ya mfululizo wa matokeo mabaya kuelekea Kombe la Dunia.

Tuje kwenye kikosi

Hispania wanaingia kwenye mashindano haya wakipewa nafasi kubwa ya kuwa mabingwa.

Wakichagizwa na rekodi nzuri ya kutopoteza mchezo wowote ndani ya mechi 30 zilizopita, Hispania ina kikosi imara kilichochanganya wachezaji wenye uzoefu na chipukizi wenye uwezo wa ajabu.

1. Sayansi imetabiri

Wataalamu wa Opta, kampuni kubwa zaidi ha takwimu za michezo, wakitumia kompyuta zenye uwezo wa hali ya juu (supercomputers) wamewapa Hispania uwezekano wa asilimia 16.1 wa kuwa mabingwa.

2. Kikosi chenye mizania

Kikosi cha Hispania chini ya mtaalamu Luis de la Fuente, kina uwiano mzuri na uliotimia na kukamilika.

Silaha yao ni uchezaji asilia wa kumiliki mpira wakiwa na mashambulizi hatari ya kujibu.

Hii inwafanya wawe wagumu sana kujilinda dhidi yao.

3. Mawinga wasumbufu

Ushirikiano wa hatari wa mawinga wenye kasi na uwezo mkubwa, Lamine Yamal na Nico Williams, ni hatari kwa afya za safu ya ulinzi ya timu zingine.

3. Msingi imara wa timu

Kikosi cha Hispania kinaundwa na msingi imara wa wachezaji wenye daraja la Dunia katika safu ya kiungo chini ya mshindi wa Ballon d’Or, Rodri, ambaye hudhibiti mwnendo wa mchezo na kuleta uzoefu usio na kifani kutoka ngazi ya juu zaidi ya mpira.

4. Umaliziaji hatari

Katika mashindano yao yaliyopita, Hispania walifunga mabao mengi kuliko timu zote, ikidhihirisha utajiri mkubwa wa wamalizia nafasi ndani ya kikosi badala ya kumtegemea mchezaji mmoja tu.

5. Mafanikio kwenye Olimpiki

Wachezaji wengi kikosini walikuwemo kwenye kikosi kilichoshinda medali ya dhahabu ya olimpiki.

Hii imesaidia kujenga utajiri wa tabia ya kuzoea kushinda na kuambukiza kwa kila wachezaji wapya wanaingia kwenye timu.

6. Muunganiko wa hali ya juu wa kimbinu

Shukrani kwa utamaduni wa Hispania kama taifa wa mchezo wa nafasi, (juego de posición), kikosi chao hucheza kwa muunganiko wa hali ya juu na uelewa asilia wa upigaji pasi wa pembatatu na kutumia mianya.

Wakati tukiwa tumeshawona wakubwa kama Brazil, Ujerumani na Uholanzi…leo ni zamu ya kuwaona Hispania.

Je moshi mweupe utawaka leo?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *