Akihutubia kikao cha 62 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Uswisi leo Juni 15, Bi. Dabo, amesema zaidi ya raia 1,000 wameuawa katika mashambulizi ya droni kati ya Januari na Mei 2026. Vifo hivyo vinawakilisha takribani asilimia 80 ya vifo vyote vya raia vilivyohusishwa na mzozo na kurekodiwa na Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa mwaka huu.

“Sudan haiwezi kusahaulika,” Bi. Dabo amewaambia wajumbe, akibainisha kuwa Vikosi vya Jeshi la Sudan na Rapid Support Forces (RSF) ambavyo ni vikosi vya waasi,  vimehusika katika mashambulizi ya droni yaliyolenga mara kwa mara miundombinu ya kiraia. Amesema mashambulizi takribani 16 yalilenga vituo vya afya na mengine 33 yalilenga masoko katika miezi mitano ya kwanza ya mwaka huu, ikiwemo shambulio dhidi ya Hospitali ya Kufundishia ya Ed Daein, jimboni Darfur Mashariki, lililosababisha vifo vya zaidi ya raia 60.

Haijawahi kushuhudiwa

Naibu Kamishna Mkuu huyo pia ameonya kuwa ukatili wa kingono umefikia “viwango visivyowahi kushuhudiwa kwa ukubwa na ukatili wake,” ukiwemo ubakaji wa makundi, mateso ya kingono na utumwa wa kingono. Tangu kuanza kwa vita, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu imerekodi zaidi ya waathirika 830 wa ukatili wa kingono nchini Sudan, ingawa idadi halisi inaaminika kuwa kubwa zaidi kutokana na changamoto za kuripoti matukio hayo.

Akielezea Sudan kama eneo lenye mgogoro mkubwa zaidi wa kibinadamu duniani kwa sasa, Bi. Dabo amesema watu milioni 34 wanahitaji msaada wa dharura huku zaidi ya milioni 14 wakilazimika kuyahama makazi yao. Ameutaka ulimwengu kuongeza shinikizo la kidiplomasia ili kufanikisha usitishaji wa mapigano kwa misingi ya kibinadamu na hatimaye kufikiwa kwa amani ya kudumu, akisisitiza kuwa, “Jumuiya ya kimataifa inapaswa kuchukua hatua za haraka kulinda wananchi wa Sudan na kuzuia mgogoro huu usisambae zaidi.”

© WFP/Asma Achahboun Wakimbizi wa Sudan wapanga foleni kupokea chakula katika eneo la usambazaji huko Adre, mji wa Chad kwenye mpaka na Sudan.

IOM yataka msaada zaidi kwa wachadi waliorejea kutoka Sudan

Wakati huohuo Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM) limetoa wito wa kuongezwa kwa msaada zaidi kwa raia wa Chad 400,000 waliorejea kutoka Sudan tangu kuzuka kwa vita nchini humo miaka mitatu iliyopita.

Kwa mujibu wa takwimu za mfumo wa ufuatiliaji wa watu waliotawanywa  DTM, idadi hiyo imefikiwa mapema kuliko ilivyotarajiwa, ikionesha kuongezeka kwa athari za kibinadamu za mgogoro huo katika maeneo ya mashariki mwa Chad.

Akizungumza baada ya kutembelea mpaka wa Adré, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa IOM anayesimamia Usimamizi na Mageuzi, Sung Ah Lee, amesema wanawake na watoto wengi waliwasili baada ya safari ndefu na ngumu, huku wakihitaji ulinzi, huduma za afya na msaada wa muda mrefu.

Asilimia kubwa ya waliorejea ni wanawake na watoto

Takwimu za IOM zinaonesha kuwa asilimia 58 ya waliorejea ni wanawake na asilimia 69 ni watoto. Wengi wao wamepokelewa katika majimbo ya Ouaddaï, Wadi Fira na Sila, ambako wanakabiliwa na uhaba wa makazi, maji safi, huduma za afya na mahitaji mengine muhimu.

IOM imekuwa ikitoa msaada wa makazi, maji, usafi wa mazingirafedha taslimu na huduma za afya ya akili kwa waliorejea na jamii zinazowahifadhi. Hata hivyo, shirika hilo linaonya kuwa msaada wa dharura pekee hautoshi tena na linataka uwekezaji zaidi katika ajira, miundombinu na mipango ya kuimarisha maisha ya waliorejea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *