
Wakati pesha ya kutoshuka daraja ikizidi kupanda, Mbeya City imesema ili kukwepa aibu hiyo haitakuwa na mzaha katika mchezo wowote ikianza na Simba Juni 17 kuhakikisha inabaki salama Ligi Kuu Bara.
Pia imesisitiza kuwa kutokana na umuhimu wa mchezo huo ambao utachezwa saa 8 mchana katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, tayari imekamilisha mipango yote ndani na nje ya uwanja kummaliza Mnyama.
Akizungumza jijini Mbeya, Ofisa Habari wa timu hiyo, Gwamaka Mwankota, amesema mchezo huo ni muhimu kwao licha ya ugumu katika hesabu na malengo kwa pande zote.
Amesema kutokana na uhitaji wao wa pointi tatu ili kujinasua nafasi za chini, uongozi umeendeleza utaratibu wa ndani kuhamasisha wachezaji wanapambana kushinda mchezo huo, huku benchi la ufundi likifanya kazi ili kutimiza malengo.
“Simba wanapambania ubingwa, Mbeya City tunakwepa kushuka daraja au kucheza ‘play off’, uongozi umeshakamilisha mipango na mengine yanaendelea,” amesema Mwakonta.
“Kuelekea mchezo dhidi ya Simba Jumatano kampeni yetu ni ushindi kuanzia Mtibwa Sugar hadi TRA United tutakapohitimisha ligi, lakini kaulimbiu yetu ni usimkatie tamaa mwanaume.”
Kuhusu utaratibu wa mashabiki na wadau kushuhudia mechi hiyo, Mwankota amesema kwa kutambua nguvu ya wadau nje ya uwanja wameweka kiingilio cha Sh5,000.
Amesema mkakati wao ni kutopoteza mchezo wowote kati ya minne iliyobaki akitamba kuwa wamejipanga na matarajio yao ni kubaki salama bila kucheza mchujo wala kushuka daraja.
“Niwaombe mashabiki kuja kwa wingi. Huu mchezo tunautaka na tunajua thamani yake kwa sasa. Tuko tayari kukabiliana na wapinzani hao dakika 90 ziweze kuamua,” amesema ofisa huyo.