
NYOTA wa zamani wa Yanga na kwa sasa Rais wa klabu ya AFC Leopards, Boniface Ambani, amemzungumzia mshambuliaji Yves Koutiama anayehusishwa na Yanga, akimuelezea kuwa straika mwenye uwezo mzuri wa kufunga.
Koutiama, raia wa Burkina Faso ni kati ya washambuliaji hatari huko Kenya baada ya kuifungia Polisi mabao 10 akiwa alijiunga nayo kwenye dirisha dogo akitokea UFSA na ndiye aliyemaliza kama kinara wa mabao wa timu hiyo katika ligi msimu wa 2025/26.
Nyota huyo mwenye uwezo wa juu aliiwezesha Polisi kumaliza nafasi ya tatu na pointi 55, inadaiwa kuwa tayari ameshamalizana na Yanga na ataitumikia timu hiyo msimu ujao wa ligi, huku mabosi wa timu hiyo wakisema kuwa wamemsajili kwa ajili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ambani ambaye alikuwa mchezaji mahiri wa Yanga miaka kadhaa iliyopita na kuibuka mfungaji bora msimu wa 2008/2009 akifunga mabao 18 amesema kuwa mshambuliaji huyo ni bora lakini atatakiwa kuwa makini sana na ligi ya Bongo.
“Ninachoweza kusema anasifa za kuwa mshambuliaji hatari, unajua wakati mwingine kiwango cha mchezaji hutegemea mambo mengi sana uwanjani lakini kwa nilivyomuona ni mshambuliaji mzuri, anaweza kuwa msaada kwa timu yoyote ambayo itamuamini na kumpa nafasi shida ni presha ya atakapokwenda na alipo sasa,” alisema Ambani huku akionyesha kuwa hana taarifa kama mchezaji huyo mwenye miaka 27 amejiunga na Yanga.
Akizungumza kwa mtazamo wa uzoefu wake, Ambani alieleza kuwa tofauti kati ya straika wa kawaida na straika wa kiwango cha juu ipo kwenye akili ya mchezo, nidhamu na uwezo wa kuendelea kufunga kila msimu bila kupungua kiwango. Alibainisha kuwa kufunga mabao ni matokeo ya ufahamu wa nafasi, kusoma mchezo mapema pamoja na kuwa na utulivu mkubwa wakati wa kumalizia nafasi za kufunga.
“Straika mzuri haangalii msimu mmoja au mechi moja. Anachojali ni muendelezo wake kila wiki, kila mwezi na kila mashindano. Hiyo ndiyo inamfanya kuwa tofauti na wengine,” alisema Ambani.
Ambani alisema kuwa mchezaji anaweza kuwa na msimu mmoja bora unaovutia macho ya wengi lakini changamoto kubwa huwa ni kurudia kiwango hicho msimu unaofuata na kuendelea kuwa na athari sawa katika kila mchezo anaocheza.
Aliongeza kuwa katika ligi za ushindani kama Tanzania, washambuliaji wanahitaji kuwa na nidhamu ya hali ya juu, mazoea ya kujituma kila siku, pamoja na uwezo wa kukabiliana na presha na matarajio makubwa.
Mshambuliaji huyo atakuwa mchezaji wa pili kwa miaka ya hivi karibuni kujiunga na Yanga baada ya awali Stephen Aziz KI kufanya hivyo na kufanya mambo makubwa na timu hiyo ikiwa ni pamoja na kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu wa 2023/2024 akifunga mabao 21.
Ambani ambaye alifunga jumla ya mabao 24 msimu wa 2008/2009, alisema mshambuliaji huyo anatakiwa kukubaliana na mazigira haraka kama anataka kuwa bora kwenye timu atakayojiunga nayo.
Yanga inajiweka sawa baada ya washambuliaji wake wawili, Prince Dube na Laurindo Depu kushindwa kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa pamoja na Ligi Kuu Bara. Depu ana mabao sita kwenye timu hiyo kwa sasa huku Dube akiwa amefunga mabao tisa ligi ikiwa imebakiza michezo minne imalizike