
KOCHA Mkuu wa Azam, Florent Ibenge ametoa tathimini ya kikosi chake hata kama kitaukosa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, hakipo mbali kutwaa taji la pili ndani ya misimu michache kutoka huu unaomalizikia.
Azam imebakisha mechi nne kumaliza msimu huu wa Ligi Kuu Bara, ikiwa nafasi ya tatu na pointi 55, juu yake zikiwa Simba iliyo nafasi ya pili na pointi 61 wakati vinara wa msimamo ni bingwa mtetezi Yanga iliyokusanya pointi 63.
Ibenge ameiongoza Azam kwa msimu wa kwanza ikitoa upinzani kwa vigogo hao wawili lakini ikashindwa kupasua katikati ya timu hizo mbili ambazo zimekuwa zikiachiana ubingwa huo wa ligi tangu msimu wa 2014–2015 ambapo Yanga imebeba mara saba na Simba nne.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ibenge alisema hata kama Azam itaukosa ubingwa msimu huu lakini timu hiyo haipo mbali kupata taji la pili la ubingwa huo kutokana na uwekezaji unaoendelea kwenye kikosi hicho.
Ibenge alisema Azam ni timu kubwa ambayo inaendelea kujiimarisha kisayansi katika kutengeneza uimara wa kikosi chake cha kwanza lakini pia kuwa na mfumo mzuri wa kuzalisha na kulea wachezaji wachanga.
“Sioni shida ya Azam labda niseme inawezekana tukaukosa ubingwa msimu huu lakini naweza kutamka kwamba, timu hii haipo mbali kurudi tena kuchukua ubingwa wa ligi ya hapa, ndani ya misimu michache kutoka huu itarudia historia hii,” alisema Ibenge ambaye anaiongoza Azam kwa msimu wake wa kwanza.
“Hii ni timu kubwa hapa Tanzania, imefanya uwekezaji mkubwa kuanzia miundombinu lakini pia rasilimali watu, ukiangalia kuna uongozi imara unaoendelea kutenegeneza kikosi cha kwanza imara kwa hesabu kubwa za baadaye.
“Unaweza pia kuangalia namna mfumo mzuri uliotengenezwa kwa ajili ya soka la vijana, unaona sikupata wakati mgumu kuamua kuwachukua wachezaji vijana kutoka timu za vijana za hapa na kuwapandisha, wapo wengine wanafanya vizuri timu zingine.”
Kauli hiyo ya Ibenge inakuja wakati ambao Azam imepita misimu takribani 11 tangu ichukue ubingwa wa ligi kwa mara ya kwanza msimu wa 2013-2014 ikimaliza bila kupoteza mchezo wowote.
Aidha Ibenge raia wa DR Congo, ameweka wazi kwamba licha ya ligi ya msimu huu kubakiza mechi nne lakini kuna ugumu mkubwa kwa kikosi chake kubeba akiona kinahitaji kusubiri zaidi anguko la timu zingine.
“Msimu huu ni vigumu kuweza kuchukua ubingwa, sawa nakubaliana na wengi kwamba kimahesabu tuna nafasi hiyo lakini kiuhalisia kuna ugumu mkubwa, naona kama tutahitaji kutegemea zaidi anguko la timu zingine huku na sisi tukitakiwa kushinda kila mchezo.
“Tunatakiwa kuendelea kuimarisha kikosi chetu, kuna hatua kubwa tumepiga msimu huu, sio rahisi sana kujenga timu imara yenye kushinda mataji ndani ya msimu mmoja, nafurahia kuwa hapa kwa kuwa naamini kila kitu kinapita njia sahihi kwenye ukuaji,” alihitimisha Ibenge.