Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi amesema kuwa Marekani ina jukumu la kuhakikisha utekelezwaji wa hati ya maelewano (MoU) ya makubaliano itakayosainiwa na Tehran na Washington ikijumuisha kusitishwa mashambulizi ya Israel dhidi ya Lebanon.

Mwanadiplomasia huyo mkuu amebainisha haya jana Jumatatu alipozungumza kwa simu kwa nyakati tofauti na Rais Joseph Aoun wa Lebanon na Spika wa bunge la nchi hiyo Nabih Berri.

Araghchi amesema, mashambulizi dhidi ya Lebanon yalipaswa “kusitishwa kikamilifu”. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ametoa kauli  hii wakati alipokuwa akiwafahamisha viongozi wa Lebanon kuhusu vifungu vya MoU, hasa vile vinavyohusiana na Lebanon.

Marekani na utawala ghasibu wa Israel zilianzisha mashambulizi yasiyo  na msingi dhidi ya Iran tarehe 28 Februari. Sambamba na hilo, utawala wa Israel ulishadidisha mashambulizi yake ya kikatili dhidi ya Lebanon na kukiuka mapatano ya usitishaji vita na Beirut, na mapatano ya usityishaji mapigano yaliyofikiwa kati ya Tehran na Washington ambayo pia yanahusu Lebanon.

Jamhuri ya Kiislamu inasisitiza kwamba, usitishaji vita wowote na Marekani unapaswa kuhusisha pande zote, ikiwa ni pamoja na Lebanon, ili kurejesha amani na usalama katika kanda hii.

Siku ya Jumapili, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilitangaza kuwa Makubaliano hayo yamekamilika na yatatiwa saini rasmi nchini Uswizi siku ya Ijumaa.

Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran Sayyid Abbas Araghchi alisisitiza juhudi za Jamhuri ya Kiislamu ya kusitisha uchokozi dhidi ya Lebanon.

Alikariri kuwa Marekani ina jukumu la kutekeleza kwa “uaminifu” hati hiyo ya maelewano na kwamba: Washington ambayo ni mshirika mkubwa wa utawala wa Israel inapasa kuishinikiza pakubwa Tel Aviv ili isitishe mashambulizi yake dhidi ya Lebanon.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *