
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Iran amesema adui alishindwa kufikia malengo yake yoyote kupitia vita viwili, akionya kwamba makosa yoyote ya kimahesabu yatakabiliwa na hasira kali ya Jeshi la Iran.
Meja Jenerali Amir Hatami ametoa matamshi hayo leo Jumanne mjini Tehran, siku moja baada ya Iran na Marekani kutangaza kuwa zimekamilisha makubaliano ya awali ya kukomesha vita vilivyoanza mwishoni mwa Februari.
“Adui alisema katika malengo yake ya kimkakati kwamba alitaka kuilazimisha Iran ijisalimishe, alitaka kuiangamiza Jamhuri ya Kiislamu, na bila aibu alizungumzia kubadilisha ramani ya Iran,” Hatami amesema na kuongeza: “Hii leo, hakuna hata moja ya malengo haya ambalo limetimizwa.”
Marekani na Israel zilianzisha vita vya uchokozi dhidi ya Iran mnamo Februari 28 na kumuua Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei na kushambulia vituo vya nyuklia, taasisi za kiraia kama shule, hospitali na misikiti.
Iran ilijibu kwa mawimbi yasiyopungua 100 ya mashambulizi ya kulipiza kisasi kwa jina la Operesheni Ahadi ya Kweli 4.
Jenerali Hatami amezungumzia uchokozi wa hapo awali, akisema kwamba wakati wa vita vya siku 12, mnamo Juni 2025 na uchokozi wa hivi karibuni wa Marekani na Israel, adui aliomba mwenyewe kusitisha mapigano.
“Taifa la Iran sit u kwamba halikukubali kujisalimisha, lakini pia mmeona katika kesi ya Lebanon kwamba Iran imelazimisha irada na matakwa yake kwa adui,” amesema Meja Jenerali Amir Hatami.
Kamanda wa Jeshi la Iran pia amepuzilia mbali madai ya adui ya kwamba ameibuuka na ushindi wa kijeshi, akiashiria ulinzi wenye nguvu wa Jeshi la Wanamaji la Iran katika umbali wa kilomita 600 za Bahari ya Oman. Ameeleza kuwa meli za kivita za adui zilizoingia katika maji ya Iran zilishambuliwa na vikosi vya majini vya Jeshi na Walinzi wa Mapinduzi na vitengo vya anga.
“Adui alitaka kutekeleza mpango wa kufungua tena Lango-Bahari la Hormuz, lakini alipigwa na makombora ya meli na ndege zisizo na rubani za Iran. Tuliona jinsi moto ulivyowawakia, na kwa maoni yangu, walitwangwa,” Hatami amesema.